Rais wa Kenya anayekabiliwa na shinikizo William Ruto alitangaza teuzi nyingine kumi za serikali yake mpya pana siku ya Jumatano, akiongezea juu ya teuzi 11 zilizotangazwa siku chache mapema.
Ruto pia aliwajumlisha wanachama wanne wa ngazi ya juu wa upinzani kama sehemu ya baraza jipya la mawaziri. Mabadiliko haya kuelekea serikali ya umoja wa kitaifa nchini Kenya yanakuja huku kukiwa na shinikizo linaloendelea kutoka kwa waandamanaji vijana wa Gen Z wanaodai utawala bora.
Wakati uteuzi huu unatizamwa kama njia ya kujaribu kurudisha amani inayohitajika sana nchini, wengi wamemkosoa kiongozi huyo kwa kuchelewa na kutofanya vya kutosha.
Judy Achienga, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na afisa mipango katika shirika linaloongozwa na vijana la Siasa Place, anaamini kuwa Rais Ruto anajaribu kutuliza upinzani, ambao umeonyesha kuunga mkono maandamano hayo.
Soma pia: Rais Ruto wa Kenya aanza kuteua baraza jipya la mawaziri
Raila Odinga, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Orange Democratic Movement (ODM), amekuwa akisifu maandamano hayo.
“Lakini ni jambo la kufedhehesha kuona uteuzi huu. Kwa sababu maandamano haya hayaongozwi na upinzani, yanaongozwa na raia,” Achienga anafafanua.
Mwanaharakati wa vijana Claudia Wairigia wakati huohuo aliiambia DW kwamba anadhani Ruto anajizatiti “kuwavutia upande wake baadhi ya upinzani ili tu kusonga mbele na ajenda yake.”
Kamari ya Ruto
Wanachama wanne wa upinzani walioteuliwa, wakiwemo naibu viongozi wa chama cha ODM, wote ni washirika wa Odinga, ambaye Ruto alimshinda katika uchaguzi wa 2022.
Hassan Khannenje, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mkurugenzi wa taasisi ya HORN, anafikiri kwamba ingawa uteuzi huu unaweza kupunguza mivutano ya kisiasa miongoni mwa baadhi ya viongozi wakuu wa upinzani, huenda usizime maandamano, hasa kwa vile baadhi ya wateule hao pia wanakabiliwa na shutuma za ufisadi.
Soma pia: Rais wa Kenya avunja baraza lake la mawaziri baada ya wiki kadhaa za maandamano
Khannenje anaongeza kuwa uteuzi wa baraza la mawaziri pia hautaweza kumzuia Odinga kuendelea kuunga mkono maandamano hayo. “Lakini wakati huo huo, Odinga ana nia ya kuwa na ushawishi katika serikali kupitia washirika wa karibu.”
Sura mpya zahitajika sana lakini hazipo
Sambamba na uteuzi huo mpya, Ruto pia aliteua wajumbe sita wa baraza lake la mawaziri lililofutwa awali kwa ajili ya serikali mpya. Hili pia lilikosolewa vikali na wale waliokuwa wakiandamana mitaani na kuhimiza mabadiliko.
“Kama rais angesikiliza ushauri wa bure kutoka kwa Wakenya, hangeteua zaidi ya watu watatu kutoka baraza lake la mawaziri la zamani kwenye baraza jipya. Kuna ukabila mwingi,” mmoja wa waandamanaji, John Njoroge, aliiambia DW.
“Uteuzi huo unaonekana kuwa umeunganisha baadhi ya maeneo ya nchi,” mandamanaji mwingine, Lex Mulwa, aliongeza, na kubainisha hata hivyo kwamba hii haitatosha kukidhi matakwa ya waandamanaji wa Jenerali Z.
Wakati huo huo Khannenje anaona hali ya kufadhaika inayoongezeka miongoni mwa vijana wa Kenya licha ya hatua za hivi karibuni za Rais Ruto. “Wanahisi kuna watu wengi zaidi wenye vigezo. Kwa hiyo tatizo ni kurudisha watu hao hao.”
Soma pia: Rais wa Kenya aapa kuchukua hatua kali dhidi ya maandamano ya vurugu
Waandamanaji wa Gen Z wametaka mara kwa mara kuwepo na damu mpya katika safu ya uongozi wa juu wa Kenya:
“Sisi, kama Gen-Z, tunakataa uteuzi mpya. Hatutaki wazee katika baraza la mawaziri. Rais anapaswa kuwaondoa na kuteua mtu kutoka Gen Z,” mfanyabiashara na mandamanaji Peter Kariuki aliambia DW.
Ushirikishwaji zaidi au utashi wa kisiasa?
Uteuzi wa Ruto hata hivyo pia unaonekana kulenga kulifanya baraza jipya la mawaziri liwe shirikishi zaidi kikabila – hatua ambayo imekaribishwa na wengi.
“Rais alikuwa aliahidi kwamba serikali ijayo ingewakilisha vyema Kenya. Sasa, pia kuna watu kutoka Magharibi mwa Kenya na pwani,” anasema Khannenje.
Wengine wanahoji kuwa hii ni kufunika kombe ili mwanaharamu apite, wakisema kuwa Ruto ameshindwa kutimiza matakwa makuu ya waandamanaji ya uwajibikaji na umahiri.
“Wajumbe wa Baraza la Mawaziri wanapaswa kuteuliwa kwa kuzingatia sifa na si [kama] fadhila za kisiasa. Inasikitisha kuona rais hakuwa akiwasikiliza vijana,” alisema Achienga katika maoni yake.
Soma pia: Ruto auondoa kabisa muswada wa fedha 2024
Bunge la Kitaifa bado halijaidhinisha uteuzi mpya wa Ruto katika baraza la mawaziri, huku vikao vyake vikiwa vimepangwa kufanyika mapema Agosti. Khannenje anahisi kuwa serikali pia inajaribu kununua muda kwa njia hii. “Labda wanatumai Gen-Z waataishiwa morali, kwa sababu hawana uzoefu na uthabiti.”
Vuguvugu la “Occupy Parliament”, hata hivyo, linaendelea kuwashinikiza wabunge kufanyia kazi matakwa yao, bila dalili za kuacha.
“Naamini maandamano yataendelea,” anasema Achienga “Maadamu tuna ukatili wa polisi, miili iliyopotea, na vijana kutekwa.”