Mwanza. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa amekemea matukio ya mauaji na utekaji nchini, akitaka Serikali ifuatilie na kuwaweka wazi wahusika, ili wawajibishwe kisheria.
Ametoa kauli hiyo jana Julai 26, 2024 katika mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi wa KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria uliofanyika jijini Mwanza.
Askofu Malasusa amesema mauaji na utekaji ni matukio yanayolitia aibu Taifa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani.
“Nitoe pole kwa wote ambao wamepotelewa na ndugu, hasa watoto na wenye ulemavu na ualbino. Katika karne hii kuendelea kufikiri imani za kishirikina zinatusaidia kupata uongozi au utajiri ,nadhani ni kurudi nyuma sana,” amesema.
Dk Malasusa amesema, “lakini pia ni aibu kwa Taifa letu na Afrika, kwamba bado tupo katika zama za giza. Kwetu sisi Wakristo ni aibu kwa sababu Yesu, moja ya sifa yake ni nuru ya ulimwengu na sisi anatutuma kuwa nuru, kama bado tunatenda matendo ya giza ni aibu na inamuhuzunisha Kristo. Kwa hiyo ni matumaini yangu vitendo hivi havitajirudia, naomba tushirikiane kuvipiga vita,” amesema.
Mjumbe wa dayosisi hiyo, Emmanuel Lwankomezi akizungumzia vitendo vya mauaji na utekaji, amesema mbinu pekee ya kuvikomesha ni jamii kumgeukia Mungu.
“Tanzania ni nchi ambayo haina dini lakini tuna madhehebu mbalimbali, naamini haya mambo yote yanaweza kuisha tukimshika Mungu, hivyo basi niombe kila mtu kwa nafsi yake, vile vitendo vyote viovu vinavyotokea katika jamii vinaweza kuisha pale tutakapoimarisha maadili na kufundishwa namna ya kumfuata Mungu na kumwamini,” amesema Lwankomezi.
Mjumbe mwingine katika mkutano huo, Rosemary Kisaka ameiomba jamii kuacha tabia ya kuwaachia jukumu la malezi mabinti wa kazi, badala yake warudi nyuma na kuwalea watoto wao katika maadili mazuri.
“Naomba kina mama tuwalee watoto wetu katika uwazi na katika maadili mazuri, wengi wetu malezi ya watoto tumeacha kwa dada wa kazi, hivyo malezi ya mama yashikiliwe tutaweza,” amesema.
Matukio ya kutekwa, kupotea na kuuawa wananchi, wakiwamo watoto, yamekuwa yakiripotiwa katika maeneo kadhaa nchini.
Kutokana na yanayoendelea Julai 20, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na machifu kutoka mikoa mbalimbali nchini waliokutana Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, alikemea matukio hayo akiwataka viongozi hao wa kimila kusaidia kuyazuia kutoka ngazi ya chini.
Jeshi la Polisi mara kadhaa limesema linafanyia kazi matukio yanayoripotiwa, likieleza jitihada kubwa inafanyika katika kuyazuia kabla ya kutokea.
Askofu Malasusa pia amezungumzia migogoro inayojitokeza katika baadhi ya dayosisi na madhehebu mbalimbali, akikemea suala la ukabila na kuwataka viongozi wa dini kuachana nalo ili kupunguza migogoro.
“Usione mtu anayekupa changamoto ukaangalia kabila lake na kujipa majibu kuwa ni kwa sababu hii. Mungu hachagui mtu wa kumpitia kusema na wewe, kwa hiyo suala hilo likome kabisa kwa sababu litatutawanya na hatutabaki kanisa moja,” amesema.
Katika mkutano huo wajumbe 223 walishiriki uchaguzi na kumchagua Mchungaji Oscar Lema kuwa Askofu wa dayosisi hiyo kwa kura 121 dhidi ya mshindani wake, Mchungaji Stephano Ling’wa aliyepata kura 102.
Mchungaji Ling’wa ameshinda nafasi ya askofu msaidizi kwa kura 165 dhidi ya Mchungaji Mimii Mziray aliyepata kura 57.