Arusha. Mahakama ya Rufani imetupilia mbali shauri la maombi lililofunguliwa na Ombeni Kimaro, akiomba kuongezewa muda wa kufungua shauri la maombi ya marejeo ya hukumu iliyotolewa na hiyo ni baada ya kukataa sababu yake ya kuchelewa kufungua maombi hayo ya marejeo kuwa alikuwa akitibiwa ukichaa.
Katika shauri hilo Ombeni alikuwa akiomba aruhusiwe kufungua shauri la marejeo ya hukumu ya mahakama hiyo iliyotolewa Agosti 2, 2020 katika rufaa ya madai namba 33 ya mwaka 2017, aliyokuwa ameikata.
Katika rufaa hiyo, Ombeni alikuwa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu katika kesi ya ardhi iliyofunguliwa dhidi yake na Joseph Mishili kwa ajili ya huduma ya Catholic Charismatic Renewal.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake huo iliitupilia mbali rufaa yake hiyo, ndipo baada ya zaidi ya mwaka mmoja tangu hukumu hiyo ilipotolewa, akafungua shauri la maombi ya kuongezewa muda ili afungue shauri la maombi ya marejeo ya hukumu hiyo.
Katika shauri hilo la maombi ya madai namba 697/01/2022, alidai kuwa alichelewa kufungua shauri la marejeo ya hukumu hiyo kwa kuwa alipata ukichaa baada ya Mahakama hiyo kutupilia mbali rufaa yake hiyo na kwamba alikuwa akitibiwa tatizo hilo kwa mganga wa jadi kwa siku 446.
Hata hivyo mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa Julai 23, 2024 na Jaji Lameck Mlacha imetupilia mbali shauri hilo la Ombeni la kuongezewa muda kufungua shauri la marejeo ya hukumu rufaa ya mahakama hiyo; kutoka na kutokuridhika na sababu hiyo aliyoitoa Ombeni.
Jaji Mlacha amesema kuwa baada ya kupitia mwenendo na maelezo ya Ombeni, alibaini kuwa mlalamikaji huyo ameshindwa kuthibitisha kuwa alikuwa mgonjwa wa akili na kutibiwa na mganga wa kienyeji kama alivyoeleza mahakama.
Chanzo cha mgororo baina ya Ombeni na Joseph ni ardhi yenye ukubwa wa ekari mbili katika eneo la Ubungo pembezoni mwa Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama kuanzia kesi ya msingi, Ardhi hiyo ilikuwa inamilikiwa na Joseph aliyepewa na Honorina Mwakitosi mwaka 2000, kama zawadi.
Baada ya kupewa Ardhi hiyo Joseph alijenga kituo cha huduma za kidini ambapo Catholic Charismatic Renewal kiliendesha shughuli zake lakini mwaka 2005, Ombeni alichukua eneo la ukubwa wa mita 16.5 x 27 akajenga nyumba.
Ombeni alibomoa choo na tanki la Joseph hivyo kupelekwa mahakamani ambapo alikabiliwa na kesi ya ardhi namba 51/2010 katika Mahakama Kuu (Divisheni ya Ardhi) Dar es Salaam, ambapo aliamriwa kulipa fidia Sh50 milioni.
Baada ya hukumu hiyo Ombeni alikata Rufaa Mahakama ya Rufaa, rufaa ya Ardhi namba 33 ya mwaka 2017, lakini pia alishindwa na baadaye ndipo akarudi tena mahakamani baada ya zaidi ya mwaka mmoja, kuomba mahakama imuongezee muda wa kufungua maombi ya marejeo dhidi ya hukumu hiyo.
Katika kiapo chake kilichounga mkono maombi hayo Ombeni alidai kuwa alishtuka baada ya hukumu ya mahakama na kupata wazimu na kupoteza kumbukumbu na kwamba hakujua nini kilifuata.
Alidai kuwa alielezwa baadaye kuwa alipelekwa kwa mganga wa kienyeji mkoani Kilimanjaro ambaye alichukua muda kuhudhuria tatizo hilo na kuwa baada ya kupata ahueni Novemba 2022 na kumshirikisha wakili, alitayarisha na kuwasilisha ombi la sasa.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, mjibu maombi, Joseph akiwakilishwa na Wakili Julius Bundala, lakini Ombeni hakuwa na Wakili, badala yake alijiwakilisha mwenyewe.
Hivyo aliiomba Mahakama ichukue maelezo yake aliyoandika kwenye hati yake ya kiapo kuwa alipata mshtuko na matatizo ya akili na baada ya uamuzi wa Mahakama alipelekwa kwa mganga wa jadi (Moshi) alikokaa kwa miezi kadhaa.
Alidai kuwa alipatwa na hali hiyo Novemba 20, 2021 na hakujua lolote hadi alipopata tena akili Aprili, 2022 lakini aliendelea kutumia dawa hadi Agosti, 2022 kisha kwenda jijini Dar es Salaam kutuma maombi hayo.
Alipoulizwa na mahakama kuhusu vithibitisho vya usafiri na matibabu alidai kutumia usafiri binafsi hivyo hana tiketi na kuhusu matibabu alidai mganga hakuwa na maelezo ya dawa, hivyo hakuwa na hati yoyote ya kuthibitisha maelezo hayo.
Wakili Bundala alieleza mahakama kuwa maeneo mawili ambayo inahitaji umakini ni pamoja na kudai hukumu haikutolewa Februari 2, 2022 kama ilivyoonyeshwa kwenye notisi ya hoja na badala yake ilitolewa Agosti 2, 2021.
Kuhusu hoja ya usafiri, wakili alidai kuwa hati ya kiapo ya Ombeni haionyeshi tarehe aliyotoka Dar es Salaam kwenda Moshi na aliporudi, wala haelezi aina ya usafiri aliotumia.
Alidai Ombeni hakuambatanisha tiketi za basi na iwapo aliondoka kwa usafiri binafsi kama inavyodaiwa, awe ameambatanisha hati ya kiapo ya mmiliki wa gari iliyompeleka na lililomrudisha.
Kuhusu matibabu, alidai hakuwa jina la mganga wala kituo chake anachotumia kutibu watu wala majina ya ndugu zake waliompeleka kwa mganga wa kienyeji.
Wakili huyo aliendelea kudai kuwa hakuna hati ya kiapo inayothibitisha kuwa alipata matatizo ya akili mara baada ya kutangazwa kwa hukumu ya Mahakama.
Wakili Bundala alidai kuchelewa kwa siku 466 haikusababishwa na ugonjwa wowote kama inavyodaiwa ila ni uzembe wa Ombeni, huku akinukuu mashauri mbalimbali yaliyowahi kutolewa na Mahakama ya Rufani ili kuongeza msimamo wake kwamba hakuna sababu halali ya kuongeza muda na kuomba maombi yatupiliwe mbali.
Katika maelezo ya nyongeza, Ombeni alisisitiza mahakama kuwa alipata wazimu katika kipindi hicho hivyo siyo kweli kwamba alizembea.
Jaji Mlacha alieleza kuwa alipata muda wa kuchunguza kumbukumbu na kuzingatia mawasilisho ya wahusika, maombi ya kuongeza muda yanafanywa chini ya kanuni ya 10 ya Kanuni, inasomeka:
“Mahakama inaweza, kwa sababu nzuri itaonyeshwa, kuongeza muda uliowekwa na Kanuni hizi au kwa uamuzi wowote wa Mahakama Kuu au mahakama, kwa ajili ya kufanya kitendo chochote kilichoidhinishwa au kinachotakiwa na Kanuni hizi, “ amesema.
“Iwe kabla au baada ya kuisha wakati huo na kama kabla au baada ya kufanyika kwa kitendo hicho; na marejeo yoyote katika Kanuni hizi kwa wakati wowote kama huo itafasiriwe kama marejeo ya muda huo ulioongezwa.” (Msisitizo umeongezwa).
Jaji aliongeza kuwa kifungu hicho kilitafsiriwa na Jaji mmoja kuwa ni kwa uamuzi wa Mahakama kutoa nyongeza ya muda, lakini uamuzi huo ni wa kimahakama, na hivyo ni lazima utekelezwe kwa mujibu wa kanuni za busara na haki, na si kwa mujibu wa maoni binafsi.
Alifafanua kuwa inataka mwombaji atoe hesabu kwa muda wote aliochelewa,uchelewaji usiwe wa kupita kiasi,mwombaji aonyeshe bidi kusiwe na uzembe na mahakama kuhakikisha kuja hoja ya kisheria.
“Mwombaji katika kesi hii ametoa maelezo kuhusu kucheleweshwa kwake akisema alikuwa akihudhuria matibabu kutoka kwa mganga wa jadi kufuatia tatizo la kiakili,”alieleza Jaji
Jaji Mlacha alieleza swali linalofuata ni iwapo kumekuwa na ushahidi kuthibitisha kuwa mwombaji alikuwa mgonjwa kwa namna ilivyoelezwa, alipata msongo wa mawazo baada ya ukumu hiyo na kupelekwa kwa mganga wa kienyeji ambapo alikaa kwa siku 466 akipatiwa matibabu.
“Baada ya kupitia kumbukumbu na mawasilisho kwa makini, nimekubaliana na Wakili Bundala kwamba mwombaji ameshindwa kuthibitisha kuwa alikuwa mgonjwa katika kipindi kinachozingatiwa,” alieleza Jaji Mlacha
Jaji alifafanua kuwa ikiwa mwombaji alikuwa mgonjwa na alienda kutibiwa kwa mganga wa kienyeji alitakiwa kuleta ushahidi kwa viapo kuthibitisha na kuwa na viapo ikiwemo hati ya kiapo ya wakili wake wa zamani Methodius Tarimo, kuthibitisha kwamba alipata msongo wa mawazo baada ya kupata hukumu.
Nyingine ni hati za kiapo za wamiliki wa magari yaliyompeleka Moshi na kumrudisha, hati ya kiapo ya mganga wa kienyeji kuthibitisha kwamba alimhudumia, na hati ya viapo ya ndugu zake waliompeleka kwa mganga wa jadi.
“ Hii ina maana kwamba, madai hayo ya kuumwa kwa muda wa siku 466 yamebaki bila uthibitisho, hivyo naona ni uzembe na hadithi ya mwombaji inaonekana kama uongo,natupilia mbali maombi na gharama,” alieleza.