BEKI aliyesajiliwa na kutambulishwa na Simba akitokea Coastal Union, Lameck Lawi ameanza rasmi mambo Ubelgiji, baada ya kufanya vipimo katika klabu ya K.A.A Gent inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Dili la Lawi kutua Simba lilikwama baada ya mabosi wa Coastal kuvunja biashara na Simba kwa madai ya kucheleweshewa malipo na mchezaji huyo kusafiri hadi Ubelgiji kwa ajili ya kuwania nafasi ya kusajiliwa na kama dili litatiki atakuwa Mtanzania wa tatu kucheza huko baada ya Mbwana Samatta na Kelvin John ‘Mbappe’ waliowahi kuzitumikia KRC Genk.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu, kutoka Ubelgiji, Lawi alisema vipimo vilikwenda vizuri na ameanza mazoezi ya kujiweka sawa akiwa na timu hiyo.
“Naendelea vizuri na tayari nimeanza kufanya mazoezi na timu hii nafikiri suala la mimi kuuzwa au kufanya majaribio wenye nafasi nzuri ya kuzungumza ni viongozi,” alisema Lawi na kuongeza;
“Mimi nafanya kazi yangu iliyonileta mara baada ya hatua ya kwanza ya kufanya vipimo kukamilika sehemu ya pili ni mazoezi ambayo sasa ndio naendelea nayo.”
Lawi ambaye msimu ulioisha alionyesha uwezo mkubwa eneo la beki wa kati na kuisaidia timu yake kumaliza katika nafasi ya nne na kupata nafasi ya uwakilishi katika Kombe la Shirikisho Afrika yupo nchini humo wiki sasa.
Wakati beki huyo akiwa Ubelgiji Simba ambayo inatajwa kumalizana naye dirisha hili la usajili inasubiri hatma ya kumnasa mchezaji huyo kutoka Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ambayo itakaa wiki moja kabla ya dirisha kufungwa.
Lawi anatajwa kusajiliwa Simba huku waajiri wake Coastal Union na wao wanasisitiza kuwa bado ni mchezaji wao.