Diarra afichua siri, amtaja Aucho

KIPA namba moja wa Yanga, Djigui Diarra amesema kitendo cha uongozi wa timu hiyo kuendelea na ukuta wao uliofanya vizuri misimu mitatu mfululizo kinaendelea kuiweka timu hiyo sehemu salama huku akimtaja Khalid Aucho kuwa ndio mchezaji kiongozi katika eneo hilo.

Yanga licha ya kufanya vurugu sehemu mbalimbali ikiongeza nyota wapya imeendelea kubaki na Ibrahim Abdallah ‘Bacca’, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Attohoula Yao, Nickson Kibabage, Kibwana Shomari huku akitemwa Joyce Lomalisa na timu hiyo kumleta nchini Chadrack Boka kama mbadala.

Akizungumza na Mwanaspoti, Diarra alisema amefurahi kuona eneo analocheza limeendelea kuwa lilelile kutokana na kutofanyiwa mabadiliko makubwa huku akikiri kuwa hakuna ugumu kama kuanza upya eneo la beki, hivyo kutokuwa na mabadiliko kwake ni furaha huku akiweka wazi kuwa Yanga bado ipo sehemu salama.

“Ukuta imara na bora niliofanya nao kazi misimu mitatu mfululizo na tukawa bora haujapanguliwa ni jambo zuri kwangu naamini hata kwa benchi la ufundi hilo limenipa furaha na nguvu nikiamini kuwa tupo sehemu salama tukiongozwa na Aucho ambaye ndiye anaanza kupunguza makali kabla ya mpira kuvuka eneo lake,” alisema Diarra na kuongeza;

“Ulinzi unaanzia kwenye eneo la kiungo mkabaji ambalo linaongozwa vyema na Aucho ndio mhimili wa timu yetu, nafurahi kuona tutaendelea kuwepo pamoja ni mchezaji kiongozi uwanjani amekuwa akifanya kazi vizuri na kina Bacca ambao wananipa imani ya kuwa langoni.”

Diarra alisema uimara wa safu yao ya ulinzi unajengwa na kuelewana kwao vizuri na kujenga muunganiko mzuri hivyo kutovunjika kwa safu hiyo ni wazi wataendelea kuwa imara na kuwa na kikosi ambacho hakitakuwa na makosa mengi kwani kwa asilimia kubwa tayari wamejenga muunganiko bora.

Alisema kila mchezaji ndani ya Yanga bila kuangalia nafasi ana umuhimu na wamekuwa wakicheza kwa pamoja hivyo anaamini hata maingizo mapya yakiingia kwenye mfumo watakuwa na msimu mwingine bora na kufikia malengo ndani na kimataifa.

“Kuzungumzia ukuta sina maana kwamba wachezaji wengine hawana msaada, hapana, hata mdau yeyote wa soka akielezwa sehemu ambayo haitakiwi kufanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara atakwambia eneo la ulinzi, kwa ujumla Yanga ni bora na tumekuwa tukicheza kwa umoja kukaba na kushambulia pamoja na ndio maana hadi mabeki wanafunga,” alisema.

Related Posts