“Ni hali ya kustaajabisha” – ndivyo alivyokiita Amy Porter, msemaji wa Muungano wa chama cha Democratic nje ya Marekani, Democratic Abroad, DA, kile kilichotokea nchini Marekani wiki moja iliyopita. Tangu uamuzi wa rais Joe Biden kukabidhi kijiti cha uongozi kwa makamu wa rais Kamala Haris, Porter anasema muungano huo, unaokiwakilisha chama cha Democratic ulimwenguni kote, umeshuhudia ongezeko la usajili wa wapiga kura wapya na watu wa kujitolea wanaotaka kusaidia kampeni ya Harris.
Jambo ambalo pengine ni la kusisimua zaidi, aliiambia DW, wamekuwa na watu wa Ufaransa, Wafaransa, watu ambao si raia wa Marekani wakiwasiliana nao wakisema, “Ningependa kusaidia” kuhakikisha Harris anachaguliwa. Katika miongo kadhaa ya kufanya kazi ya kujitolea na muungano huo, Porter alisema amewahi kushuhudia hali hii kwa nadra sana.
Uasi miongoni mwa wapiga kura Wamarekani ughaibuni
Mpango wa serikali ya shirikisho la Marekani wa kusaidia masuala ya upigaji kura unakadiria kwamba kuna Wamarekani milioni 2.8 wanaoishi nje ya nchi ambao wana haki ya kupiga kura katika chaguzi za shirikisho. Mnamo mwaka 2016, kwa mujibu wa mahesabu ya mpango huo, ni asilimia 6.9 tu kati yao waliopiga kura.
Wafuasi wa chama cha Democratic wanatumai wanaona sasa fursa hiyo imechochewa na wengi, huenda wakashiriki uchaguzi wa Novemba 5. Muungano wa DA ulisema usajili wa wapiga kura nje ya Marekani kupitia njia ya barua umeongezeka mara tano katika kipindi cha siku tatu wiki hii, hadi kufikia 3,000 ikilinganishwa na kipindi kama hicho wiki iliyopita. Mchakato huu huwasajili wapiga kura wa vyama vyote, lakini muungano wa DA ulisema idadi ya wanachama wake wapya pia iliongeza mara tatu kutoka Jumatatu hadi Jumatano.
Na sawa na kile ambacho wachangishaji wa chama cha Democraticwamekishuhudia nchini Marekani, Porter alisema fedha kutoka kwa Wamarekani – raia wa kigeni hawaruhusiwi kuchangia kwa kampeni za uchaguzi wa Marekani – pia zinamiminika katika makasha ya muungano huo. “Huwa tunapata michango mara kwa mara, lakini huu umevuka viwango vilivyozoeleka, ” alisema.
Finland yapata joto la hamasa ya Kamala
Dana Freling aliasisi tawi la muungano wa Democratic Abroad, DA, nchini Finland baada ya Donald Trump kuingia madarakani mwaka 2017. Alisema ameshuhudia wimbi kama hilo la wafanyakazi wapya wa kujitolea katika siku za hivi karibuni, wakiwemo raia wa Finland ambao anasema wana wasiwasi kuhusu hulka ya rais wao wa zamani kuelekea jumuiya ya kujihami ya NATO. Finland ilijiunga na NATO mnamo 2023 baada ya Urusi kuivamia Ukraine na ina mpaka wa pamoja wa kilomita 1,340 na Urusi.
“Usalama wa kimwili hapa Finland unategemea jinsi rais wa Marekani atakavyouongoza muungano huu,” alisema. “Na tunahisi kwamba usalama wetu unategemea na jinsi rais anavyouunga mkono mtandao huu wa NATO.”
Soma pia: Obama na mkewe wamuunga mkono Harris kugombea urais
Ingawa sera ya nje haichukuliwi kuwa eneo mojawapo ambalo Harris ana nguvu, ameweka wazi bayana maoni yake kuhusu Urusi – katika mkutano wa kimataifa wa usalama mjini Munich, kwa mfano, ambako alithibitisha kuiunga mkono Ukraine na kuwahakikishia washirika kwamba “ahadi za utawala wa Biden kwa NATO zinabaki imara.”
Freling alisema ongezeko la ghafla ya uungwaji mkono kwa urais wa Harris limefuta uasi wa wapiga kura na hata kuwashawishi wafuasi wa chama cha Republican kama kaka yake anayeishi jimboni Texas wabadili tiketi zao. Anasema kaka yake alibadilika kutoka mtu aliyempuuzilia mbali Harris hadi kuamua kumpigia kura.