Dar es Salaam. Serikali imeagiza kufungwa Kanisa la Christian Life Church linaloongozwa na Mchungaji Domique Kashoix Dibwe maarufu Kiboko ya Wachawi, lililopo Buza Kwa Lulenge.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kanisa hilo kwenda kinyume cha taratibu za usajili.
Barua hiyo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia ya Julai 25, 2024 ambayo Mwananchi imeiona imewaelekeza Mwenyekiti wa Kanisa la Christian Life Church na Mchunga Dominique Kashoix Dibwe kufunga tawi la Kanisa hilo linaloendeshwa na Mchungaji Dibwe maarufu kwa jina la Kiboko ya Wachawi, lililopo eneo la Buza kwa Lulenge, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Imesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kufanya vitendo ambavyo ni kinyume na matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Namba 3 ya Mwaka 2019, vyenye athari ya kusababisha kanisa hilo kufutiwa usajili wake na kuondolewa kwenye Rejista ya Jumuiya za Kiraia zilizosajiliwa.
Miongoni mwa sababu za kufungwa kwake zimetajwa ni kutoa mafundisho yenye kuleta taharuki katika jamii na mahubiri ambayo ni kinyume na maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.
Madai mengine ni kutoa mahubiri yanayodhalilisha watu madhabahuni, kutoa mahubiri chonganishi na kuhamasisha waumini wa kanisa lake kuua watu kwa dhana au tuhuma za uchawi au ushirikina.
Barua hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha imetolewa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa imesema, madai hayo yanakwenda kinyume cha imani ya Kikristo, Katiba na kanuni za kanisa hilo, ikiwamo kuweka kiwango cha Sh500,000 kwa waumini kupata huduma ya maombezi.
Nakala za taarifa hiyo zimepelekwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Inspekta Jenerali wa Polisi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki.
“Kutokana na hali hiyo, kwa barua hii, unajulishwa kuwa unatakiwa kufunga mara moja shughuli na huduma zote zinazotolewa katika kanisa hiyo kabla ya tarehe 28/07/2024 (leo),” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Baada ya kusambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Serikali imeagiza kufungwa Kanisa hilo, baadhi ya vitu kanisani hapo vimeondolewa.
Akizungumza na Mwananchi lililofika kanisani hapo jana, Shabani Ramadhani ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Kidagaa, Kata ya Buza lilipo kanisa hilo, alisema ameona turubai na spika zikiondolewa kanisa, hivyo akahoji tatizo ni nini?
“Nikaambiwa imeletwa barua kutoka Dodoma kwamba huyu bwana shughuli yake hapa isitishwe mara moja,” alisema.
Ramadhani alisema majibu hayo alipewa na watu waliokuwa wakiondoa vitu hivyo wakieleza wahusika walipatiwa barua juzi.
“Leo watu hawakusali na taarifa hii naona ilitolewa kuanzia jana (juzi), tatizo kubwa ni kutoza watu hela, kusema anaua wachawi,” alisema.
“Lisemwalo lipo kama halipo laja, ukweli idadi ya watu imepungua nimepita pale mara mbili watu wanaondoa vitu, nimekutana na wale kina mama wanaofanya kazi pale wanalalamika watakwenda wapi,” alisema.
Alisema kutokana na idadi kuwa ya watu kanisani hapo, serikali ya mtaa ililazimika kuongeza ulinzi ili wanaoingia waingie na kutoka salama.
Juhudi za mwananchi kuzungumza na mchungaji huyo hakizukuzaa matunda.
Tofauti na siku zingine ambako watu huwa wengikanisani hapo, jana jioni walionekana wachache wakiendelea na kazi ya kutoa vifaa vya kanisa na kuvipakia kwenye gari maarufu Kirikuu.
Muumini mwanamke aliyefika kanisani hapo akiwa kwenye bodaboda aliambiwa hakuna ibada.
Hatua hiyo imechukuliwa takribani wiki mbili zimepita tangu Mwananchi lilipochapisha ripoti maalumu kuhusu baadhi ya manabii na makuhani kujipatia ukwasi mkubwa kutokana na kuwatoza waumini fedha ili wawaombee.
Pia wamekuwa wakijipatia fedha kwa kuwauzia bidhaa za upako na uponyaji za maji, chumvi, mafuta na vitambaa.
Mwananchi wakati wa ufuatiliaji wa ripoti hiyo, lilifika katika kanisa hilo na kuhudhuria moja ya ibada za Jumapili, ambapo mwandishi alishuhudia mmoja wa watenda kazi wa kanisa hilo akitangaza “ili kumwona Kiboko ya Wachawi, muumini atatakiwa kutoa Sh500,000 ndipo afanyiwe maombezi.
“Kama una Sh500,000 nenda pale kaandikishe jina lako uende kumuona nabii,” alisema mtendakazi huyo ambaye jila lake ilikuwa vigumu kulipata.
Pia alitangaza “kila mtu anunue maji kwa Sh2, 000 ambayo yangeombewa na mchungaji.”
Baadhi ya waumini waliozungumza na Mwananchi walieleza changamoto wanazopitia ili kumuona kiongozi huyo wa dini.
“Nipo hapa tangu jana (siku alipohojiwa) nimelala hapa, tayari nimelipa Sh50,000, niliambiwa ningemuona leo lakini naambiwa niongeze hela hii niliyotoa nilikopa na hapa nina nauli peke yake,” alisema Upendo Ngowi (si jina halisi) mkazi wa mkoani Pwani.
Upendo alikuwa akibembeleza kwa walinzi ili amuone mchungaji huyo lakini aliambiwa akaongeze Sh300,000 apate fomu ya kumuona mtumishi.
Hata hivyo, alisema siku hiyo alikuwa amebakiwa na Sh10,000 za nauli ya kurudia nyumbani.
Mwananchi lilimtafuta mchungaji huyo kupitia simu ya mkononi bila mafanikio na hata alipotumiwa maswali kwa mtandao wa WhatsApp, hakuyajibu.
Hata hivyo, akihubiri katika ibada ya Jumapili Julai 14, 2024 baada ya habari hiyo kuchapishwa, Mchungaji ‘Kiboko ya Wachawi’ alisema amekuwa akisumbuliwa na waandishi wa habari wakimtaka ajibu madai yanayoelezwa na baadhi ya viongozi wa dini kuhusu huduma yake, lakini hakuwahi kuwajibu.
“Mungu ana maajabu yake, kati ya mtu anayesemwa na anayesema, mara nyingi Mungu anamuongezea anayesemwa ndicho kinachotokea hapa kwangu kila siku watu wanaongezeka,” alisema.
Alisema haiwezekani watu wakienda kusali kwao wanadai hawatapeliwi, lakini wakienda kanisani kwake wanasema anatapeli waumini.
“Wote wanaonisengenya wana wivu, kuna kitu hawana na wanatamani kufanya ninachofanya. Wanaonisema vibaya wanasema hivi… sisi wenye Mungu wa kweli na tuna mafundisho ya kweli, hatupati watu wa,kuwaambia, lakini huyu jamaa mjinga lakini ana watu wengi,” alisema.
“Hicho ulichonacho unajuaje kama ni cha Mungu kweli na kama kingekuwa cha Mungu kweli, basi watu wangewafuata. Nilisema waumini waliopo hapa ni walewale waliokuwa makanisani na misikitini juzi, si jambo la kuficha, nasema ukweli,” alisema.
“Hakuna mchungaji, kanisa, msikiti wenye hakimiliki ya kumiliki watu… watu wako? Nasema hivi kama umekaa kwenye kanisa au msikiti kwa muda mrefu hujapona shida zako toka njoo hapa, ninawakaribisha waumini wa makanisa yote waje kusali hapa na msiwe na wasiwasi na wakikulaani na sisi tutawalaani hapahapa,” alisema huku akishangiliwa na waumini.
“Kuna presha kubwa huko mitandaoni wachungaji wamekuwa wakali kwa waumini wao wakiwaambia kwamba yule mchawi msiende,” alisema.
Alisema presha inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii haifanyiki kwa bahati mbaya, wanajua wazi kabisa katika kipindi kifupi kijacho (makanisa) yanaenda kuwa tupu.
Aliwaeleza waumini anazindua kampeni ya wiki mbili kuanzia Julai 15, hivyo waumini wajipange.
“Mtaelewa kwa nini wanalalamika, wakienda kusali kwao hawatapeliwi mkija kusali hapa mnatapeliwa, mkienda kusali kwao mna akili lakini mkija hapa ninyi manyumbu, haina shida bora uitwe nyumbu lakini uwe na hela,” alisema.
Aliwaeleza kabla ya kuwa nabii, yeye alikuwa mfanyabiashara na muumini wa kanisa moja eneo la Boko, jijini Dar es Salaam baadaye akaacha na kuanzisha kanisa hilo.