Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imekazia uamuzi wake wa awali unaomuondolea mfanyabiashara Sauli Amon, maarufu S.H. Amon umiliki wa jumba la ghorofa nane alilojenga eneo la Kariakoo, Dar es Salaam.
Jumba hilo lipo katika kiwanja alichonunua nyumba awali.
Uamuzi huo unatokana na shauri la maombi ya marejeo alilolifungua S.H. Amon, akipinga hukumu ya Mahakama ya Rufani iliyobatilisha ununuzi wa nyumba ya awali, aliyoivunja na kujenga ghorofa hilo.
Katika uamuzi uliotolewa Aprili 22, 2024 na jopo la majaji Jacobs Mwambegele, Issa Maige na Gerson Mdemu, Mahakama imetupilia mbali maombi ya S.H. Amon, aliyewahi kuwa mbunge wa Rungwe ikieleza sababu alizotoa kuitaka Mahakama irejee na hatimaye kubadilisha hukumu hazikuwa na mashiko.
Mahakama imekubaliana na hoja za mawakili wa wajibu maombi kuwa sababu hizo hazikuwa miongoni mwa zinazoifanya mahakama irejee hukumu yake, bali zilikuwa sababu za rufaa.
Uamuzi huo umetolewa baada ya zaidi ya miaka 20 ya malumbano ya kisheria mahakamani kati ya S.H. Amon na wanafamilia waliokuwa wakimiliki nyumba ya awali, aliyoinunua na kuivunja.
Katika shauri la maombi ya marejeo namba 264/01 la mwaka 2022, mbali na wanafamilia, Amon alimuunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama mdaawa wa upande wa tatu.
Alidai hukumu ina makosa ya dhahiri yanayosababisha haki kutokutendeka kwa madai.
Amon alidai Mahakama haikuwa na mamlaka kuachana na kanuni iliyowekwa kuhusu kesi za mnunuzi wa mali katika mnada uliotangazwa na Mahakama, kuwa anapaswa kulindwa na sheria na kwamba, hawezi kuathirika au kulaumiwa kwa kasoro yoyote kwa aliye na mali inayopigwa mnada.
Pili alidai atapata hasara ya bei yote aliyonunulia nyumba ya awali na ya uwekezaji mkubwa alioufanya katika kiwanja hicho, pia kuwaruhusu wanaodai hisa ya 6/7 (wanafamilia) kunufaika na uwekezaji alioufanya bila kumfidia.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Amon aliwakilishwa na mawakili Julius Kalolo-Bundala, Samson Mbamba na Daniel Ngudungi. Wanafamilia waliwakilishwa na Dorah Mallaba na Ashiru Lugwisa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwakilishwa na Wakili wa Serikali Jesca Shengena.
Wakijibu hoja kwa nyakati tofauti Mallaba, Lugwisa na Shengena walidai sababu zote zilizotolewa na Amon kuomba hukumu ifanyiwe marejeo hazijakidhi vigezo bali ni hoja za rufaa.
Walidai hoja au malalamiko yake katika maombi mengine yalikuwa miongoni mwa sababu za rufaa na yaliamuriwa na Mahakama, hivyo haiwezi kuyafanyia marejeo.
“Mwombaji anachokiomba ni Mahakama kuangalia tena ushahidi, kudurusu kumbukumbu za mwenendo kuona kama kesi hiyo ilifunguliwa nje ya muda. Kuangalia ushahidi kwa mara ya pili kunaiondolea hoja sifa za kuwa sababu ya kufanya marejeo,” imeeleza Mahakama katika uamuzi.
“Hatuoni sababu katika malalamiko haya na tunakataa mwaliko wa kurejea hukumu yetu katika sababu hii.”
“Hatuwezi kugeuka na kuwa wapofu kwa kanuni ya kisheria iliyowekwa vema kwamba mashauri lazima yafike mwisho, ili kuwapa wadaawa fursa. Maombi haya yameshindwa na yanatupiliwa mbali kwa gharama,” imeamuru Mahakama.
Nyumba hiyo ilikuwa inamilikiwa na wanafamilia saba kwa ubia, kila mmoja akimiliki chumba chake.
Mgogoro ulianza baina ya mmoja wa wamiliki hao, anayetajwa kwa jina la Tatu na mpangaji wake.
Tatu alimpangishia Mussa Kazuba chumba chake kwa matumizi ya kibiashara lakini baadaye walishindwa kuelewana kwa kile Kazuba alichodai Tatu alikiuka makubaliano.
Kazuba alipeleka malalamiko Baraza la Ardhi la Mkoa (wakati huo) akiomba arejeshewe Sh18 milioni alizokuwa amelipa kodi ya pango pamoja na riba iliyodaiwa ilifikia Sh15 milioni.
Baraza lilikubali madai yake na kutoa amri ya kupigwa mnada nyumba hiyo namba 113, kitalu namba 4 bloku namba 17.
Katika kutekeleza uamuzi wa baraza hilo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliamuru nyumba hiyo ikamatwe na kupigwa mnada.
Hilo lilifanyika Aprili 19, 2000 na Mei 13, 2001 ilinunuliwa na S.H. Amon kwa Sh105 milioni na alipewa hatimiliki namba 57275 iliyotolewa Machi 24, 2005, kwa jina la kampuni yake ya S.H. Amon Enterprises Co. Ltd.
Baada ya kuinunua aliwaondoa wanafamilia na wapangaji wengine waliokuwamo, aliivunja na kujenga ghorofa hilo.
Mwaka 2004 wanafamilia Hamis na dada zake Stumai na Hatujuani (walio hai), Neema na Mwajuma (marehemu kwa sasa) ambao yeye Hamis ni msimamizi wa mirathi yao, walifungua kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi wakipinga uuzwaji wa nyumba hiyo.
Katika kesi ya msingi ya ardhi namba 185 ya mwaka 2004, wadaiwa walikuwa S.H. Amon, S.H. Amon Enterprises Ltd, Kazuba na Kassim Ally Omar, msimamizi wa mirathi ya dada yao mwingine, Tatu Bushiri Pazi.
Wanafamilia waliiomba Mahakama itamke wao ndio wamiliki halali wa eneo hilo na kwamba, amri ya kukamatwa, kuuzwa, wao kuondolewa na nyumba kubomolewa haikuwa halali na kulikuwa na udanganyifu.
Mahakama Kuu katika hukumu iliyotolewa na Jaji Kakusulo Sambo, Machi 9, 2012 iliamua S.H. Amon Enterprises Ltd ndiye mmiliki halali.
Wanafamilia walikata rufaa namba 166 ya mwaka 2019, Mahakama ya Rufani wakiwakilishwa na Wakili Melchisedeck Lutema (marehemu), dhidi ya S.H. Amon na wenzake, wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu.
Mahakama ya Rufani ilitengua hukumu ya Mahakama Kuu Aprili 13, 2022, pamoja na mambo mengine ilisema nyumba yenye mgogoro iliyopigwa mnada ilikuwa ikimilikiwa kwa ubia na wanafamilia sita, huku Tatu aliyekuwa anadaiwa anamiliki 1/7 ya hisa katika nyumba hiyo.
Mahakama ilisema kuuzwa na kuhamishia umiliki wa nyumba kwa kampuni ya S.H. Amon haikuwa halali.
Ilisema mnunuzi alilijua hilo, na kwamba kiwango chochote cha uwekezaji alioufanya alifanya kwa hasara yake.
“Hatuwezi kuamuru kubomolewa jengo la sasa lililopo katika eneo hilo kwa kuwa hatuoni kosa lolote kwa jengo lenyewe. Kwa namna yoyote amri hiyo haitaunufaisha upande wowote na itakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Taifa,” ilisema Mahakama katika hukumu.
“Tunatengua na kutupilia mbali hukumu na amri ya Mahakama Kuu na kutamka kuwa warufani ni wamiliki halali wa eneo lenye mgogoro na uendelezaji wote uliofanyika kwa kiasi cha hisa 6/7”