SERIKALI kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo umesaini mkataba na Kampuni ya Railway Construction Engineering Group (CRCEG) kutoka China, kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mkataba huo una thamani ya Sh19.7 bilioni kabla ya VAT huku ukarabati ukitarajiwa kuchukua takriban miezi 12 ili kukamilika.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema licha ya kumpa mkandarasi miezi 12 lakini wamemuomba ikiwezekana akamilishe kwa miezi sita kutokana na uhaba uliopo wa viwanja nchini Tanzania hasa Dar es Salaam.
“Sawa tumempa miezi 12 lakini tumemuomba ndani ya miezi sita uwe umekamilika kwa sababu ya uchache wa viwanja.”
“Tumezungumza na mkandarasi kuwa tunauhitaji uwanja kukamilka mapema kwani Azam Complex ukija kufungwa itakuwa tabu kwa ligi kuchezwa hivyo tunauhitaji Uwanja wa Uhuru mapema,” alisema Msigwa.
Aliongeza kuwa, uwanja huu ukitumika ipasavyo utasaidia kupunguza matumizi ya Uwanja wa Benjamini Mkapa, lakini itatoa fursa ya kuandaa mashindano mengi na Tanzania kuwa wenyeji.
“Tuna uhakika wa wakandarasi tuliowapa kwa sababu tunawafahamu na tuna imani watafanya kitu kizuri, Uwanja wa Uhuru unaingiza watu elfu 23 lakini tunahitaji kupandisha hadi elfu 30.
Tutajadiliana na Mkandarasi wa Uwanja wa Uhuru kuondoa sehemu ya kukimbilia Riadhaa na kuongeza viti ili kuweza kupanda daraja kutoka tatu hadi mbili katika viwango vya Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA),” alisema Msigwa.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Suleiman Serera, alisema ukarabati huo utakuwa sehemu ya vyumba vya kubadilishia nguo, ukuta wa uwanja, ubao wa kuonyesha matokeo, mifumo ya sauti, sehemu ya kukimbia riadha, kamera za usalama na eneo la kuchezea (Pitch).
“Ukarabati huu ni muendelezo wa ujenzi wa viwanja hapa nchini ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2027 ambapo Tanzania tunatarajia kuwa wenyeji wa mashindano hayo.
“Inahitaji kuwa na miundombinu ya kutosha hivyo Tanzania tayari imeanza ukarabati wa baadhi ya viwanja ikiwemo New Amaan Complex visiwani Zanzibar na Benjamin Mkapa (Dar es Salaam).
“Serikali inaendelea kutengeneza baadhi ya vituo mbalimbali vya michezo na vipo viwanja muhimu vya ukarabati ikiwemo Uhuru, huo utatumika kufanyia mazoezi kwa timu zinazotaka,” alisema kiongozi huyo.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema jambo la kusaini mkataba kwa Wizara na CRCEG ni kubwa sana kwa sababu Uwanja wa Uhuru, una historia na kuahidi kushirikana na kusaidia kupata uwanja mazuri kwa ajili ya kutumika katika mazoezi.
“Ukarabati wa Uhuru utakuwa na faida kubwa sana kwetu, kwa sababu baada ya Afcon, utatumika kwa ajili ya timu kucheza michezo mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema Karia.