Takwimu zinaeleza kuwa Wastani wa umri wa kuishi kwa Mtanzania umeongezeka kutoka miaka 52 kwa takwimu za mwaka 2000 hadi kufikia miaka 66 mwaka 2022 huku wanawake wakitajwa kuishi muda mrefu kuliko wanaume.
Takwimu hizo zimetolewa Julai 27, 2024 jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo wakati akizungumzia utekelezaji wa dira ya maendeleo inayotarajiwa kumalizika mwaka 2025 ambapo amesema kuwa takwimu hizo zinaashiria mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Dira hiyo ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2000-2025.
“Lengo lilikuwa umri ufike miaka 68 ifikapo mwaka 2025 na kwenye takwimu za sasa wanawake wanaishi umri mkubwa zaidi wa miaka 68 ikilinganishwa na wanaume wanaoishi wastani wa miaka 64,” amesema Profesa Mkumbo.
Aidha amebainisha kuwa maandalizi yalianza kwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa dira ya Taifa ya maendeleo 2025 ambapo kazi hiyo ilifanywa na taasisi huru ya utafiti ya ESRF huku akisema kuwa taarifa ya tathmini hiyo imekuwa msingi wa uandaaji wa diira ya Taifa ya miaka 25 ijayo.
Ikumbukwe kuwa Waziri Mkumbo ndiye mgeni rasmi katika Kongamano la Pili la Kikanda la Kukusanya maoni kuhusu uandaaji wa dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 – 2050 linalofanyika jijini Arusha.