BAADA ya kukamilisha mchakato wa kubadili jina kutoka Fountain Gate Talents kuwa Songea United, uongozi umesema kwa sasa unahamia katika kusuka timu mpya kwa usajili bora ili kuisaka Ligi Kuu msimu ujao.
Timu hiyo yenye makazi yake mjini Songea, inatarajia kushiriki Championship msimu ujao ambapo awali ilijulikana kama FGA Talents na sasa itasomeka Songea United baada ya kukamilika kwa makubaliano ya pande zote.
Meneja wa timu hiyo, Shaibu Ibrahim alisema kwa sasa wanaendelea na usajili wa wachezaji na wapo ambao wamemalizana nao hivyo hadi kufikia Agosti 1 watakuwa wameanza kuingia kambini kujiandaa na msimu mpya.
Kuhusu hatma ya benchi la ufundi, meneja huyo alisema uongozi unaendelea kufanya majukumu yake kumpata kocha baada ya waliokuwa kwenye rada zao kutimkia timu nyingine akiwamo Mbwana Makata (Prisons) na Aman Josiah aliyeenda Geita Gold.
“Kwanza tumekamilisha mabadiliko ya jina la timu, ambapo msimu ujao tutatumia Songea United, kazi iliyopo kwa sasa ni usajili na tuko sehemu nzuri kwani wapo baadhi ya wachezaji tumemalizana nao.
“Matarajio yetu ni hadi Agosti 1 tuwe tumeingia kambini na suala la kocha tutamtangaza tutakapokuwa tumempata kwa sababu tuliowapata awali tayari wamejiunga na timu nyingine ila uongozi haujalala,” alisema Ibrahim.
Meneja huyo alisema usajili wao utazingatia uhitaji wa timu kulingana na ligi wanayoenda kushiriki, ambapo watachanganya kikosi ikiwa ni wazoefu, chipukizi na waliopandishwa ili kutengeneza ubora, kasi na ushindani.
“Wapo waliocheza Ligi Kuu, Championship na ambao wanajitafuta, tumeamua kufanya hivyo ili kupata ladha tofauti kwani ushindani utakuwapo na kila mmoja atakuwa na uwezo wake hivyo matarajio ni makubwa,” alisema meneja huyo.