Mbeya Unity sio kinyonge! | Mwanaspoti

WAKATI Ligi Kuu ya Netiboli nchini ikitarajiwa kuanza Agosti 1 huko jijini Arusha, Mbeya Unity Queens imesema hawataenda kinyonge katika mashindano hayo, bali kupambania heshima ya Mkoa wa Mbeya kubeba ubingwa, huku ikilia na ukata.

Mbeya Unity ndio msimu wake wa kwanza kushiriki ligi hiyo baada ya kupanda daraja mwaka huu na kuungana na ndugu zao Mbeya Uwssa wanaomilikiwa na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbeya.

Mkurugenzi wa timu hiyo, George Mackona alisema kwa sasa wanaendelea kupitisha bakuli nyumba kwa nyumba kusaka japo nauli na gharama zitakazowawezesha kuishi Arusha kwa kipindi chote cha mashindano akieleza kuwa ndani ya uwanja wako fiti.

Alisema katika maandalizi yao, wamejitahidi kutimiza mahitaji ya benchi la ufundi kwa kufumua kikosi na kuongeza nyota 12 wapya na kukamilisha mahitaji ya wachezaji 17 wanaohitajika katika mashindano kikanuni na kwamba matarajio yao ni kufanya vyema.

“Tunahangaika kwa sasa tupate sapoti ya wadau ili kutuwezesha kusafiri na kushiriki vyema ligi hii, tumejipanga ndani ya uwanja kuhakikisha tunaipa heshima Mbeya, hatuendi kinyonge, nia ipo ya ushindi,” alisema Mackona.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Miraji Bugga alisema pamoja na ugeni walionao katika ligi hiyo, benchi la ufundi limejitahidi kuweka mipango imara na wachezaji wameonyesha dhamira ya kwenda kushindana kufanya vizuri.

“Tunaenda kupambana licha ya ugeni wetu hatuogopi yeyote bali lengo ni kuona kila mpinzani tunamheshimu, tutajitahidi kila mechi tupate ushindi kwakuwa kikosi tulichonacho kinaweza kufanya kazi,” alisema kocha huyo.

Related Posts