Aliyeua watoto wawili na kuwatoa ubongo kisa mahari, kunyongwa

Musoma. Ni ukatili, ndivyo unaweza kuelezea kitendo alichokifanya Kitonyo Mwita, mkazi wa Musoma mkoani Mara, jinsi alivyowaua watoto wawili, kiini kikiwa ni kurudishiwa ng’ombe aliotoa kama mahari ya mwanaye.

Tafrani hiyo ilianzia pale mtoto huyo wa kiume alipofariki dunia muda mfupi baada ya kufunga ndoa na baba akamuomba mjane amuoe, alipokataa alimrudisha kwa wazazi wake na kutaka arejeshewe mahari.

Mwita aliyetekeleza mauaji hayo Agosti 18, 2018, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani lililoketi Musoma, wameyaita ya kikatili pale alipowaua Bhoke Magweiga (6) na Petro Magweiga (2) kwa kuwapasua mafuvu kwa nondo.

Katika hukumu ya rufaa waliyoitoa Julai 26, 2024, jopo la majaji hao Shaban Lila, Pantrine Kente na Leila Mgonja walisema adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa na Mahakama Kuu Musoma Oktoba 15, 2020 ilikuwa sahihi.

Shahidi wa nne wa upande wa jamhuri, Magweiga Mugendi aliiambia Mahakama kuwa mtoto wa Kitonyo Mwita alimuoa mtoto wake Rhobi na ili kutimiza masharti ya kimila, mrufani huyo akalipa mahari ambayo ni ng’ombe sita.

Kwa bahati mbaya, katika kipindi kifupi cha ndoa yao, mtoto wa Kitonyo alifariki dunia kwa ajali jijini Mwanza na kumuacha Rhobi akiwa mjane, ndipo mrufani alimwendea Rhobi akimshawishi akubali amuoe kama mke wake mpya.

Rhobi akakataa ombi hilo la baba mkwe wake, jambo lililomuudhi Kitonyo Mwita akaamua kumrudisha kwa wazazi wake,  kwa kuwa Rhobi hayuko tena kwenye familia yake, mrufani akataka arudishiwe mahali aliyomlipia mwanaye.

Shahidi huyo akaieleza Mahakama kuwa alifanikiwa kurudisha ng’ombe watano kati ya sita na akaahidi kumalizia ng’ombe aliyebaki atakapokuwa amepata.

Ahadi hiyo inaonekana haikumpendeza mrufani huyo na kwa mujibu wa shahidi huyo alizungumza maneno machafu yaliyomaanisha shahidi huyo wa nne alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mama yake mzazi.

Kauli hiyo ilimuudhi mke wa shahidi huyo, Mary Mugendi aliyekuwepo nyumbani hapo na alimwambia mrufani angewaita polisi, hapo ndipo mrufani alitoa panga na kumjeruhi nalo Mary miguu yote miwili.

Hata hivyo, shahidi huyo alieleza alifanikiwa kumnyang’anya Mwita panga hilo na kumpa mkewe (Mary) aliyekwenda nalo kushtaki polisi.

Baada ya kuona ameshanyang’anywa panga, mrufani alikimbilia barabarani na kurudi na kipande cha nondo alichopewa na mtoto wake, Chacha Kitonyo na kwenda hadi nyuma ya nyumba walikokuwa wakicheza watoto wa Mugendi.

Huko alimshambulia Bhoke Magweiga (6) kwa nondo mara mbili kichwani hadi ubongo ukatokeza nje ya fuvu kutokana na ukubwa wa pigo alilompiga.

Baada ya hapo, mrufani alikwenda kumshambulia kichwani mtoto mwingine, Petro Magweiga (2) na kumpasua fuvu na kutokana na mashumbulizi hayo, Bhoke alifariki dunia papo hapo wakati Petro alifariki alipofikishwa kituo cha afya Ikizu.

Shahidi wa tatu, Dk Methodius Kagumilwa aliyeifanyia uchunguzi miili ya watoto hao, alibaini Petro alikuwa amepigwa na kitu butu kichwani na ubongo ulikuwa ukitoka, vivyo hivyo kwa Bhoke aliumizwa vibaya kichwani na ubongo ulikuwa unaonekana.

Baada ya Mahakama kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa upande wa jamhuri na utetezi wake, Jaji Zephrine Galeba alimtia hatiani kwa mauaji ya kukusudia na kumweleza kuwa adhabu kwa muuaji anayetiwa hatiani huwa ni moja, kunyongwa hadi kufa.

Alivyokata rufaa kujinasua

Baada ya kuhukumiwa kifo, Mwita alikata rufaa Mahakama ya Rufani akiegemea hoja tatu, moja ni kuwa Mahakama ilikosea kisheria kupokea ushahidi usio na uhusiano kutoka kwa shahidi wa nne ambaye ndiye pekee alishuhudia mauaji.

Katika hoja ya pili, Mwita alieleza Mahakama kukataa asitumie maelezo ya shahidi huyo wa nne aliyoyaandika polisi yaliyopokewa mahakamani kama kielelezo, ilikiuka ibara ya 107A2 (e) ya Katiba ya Tanzania na kunyima haki.

Mbali na hoja hiyo, aliieleza Mahakama ilikosea pale iliposhindwa kuwaelezea wazee washauri wa Mahakama wajibu wao kabla ya kuanza kwa kesi ya upande wa jamhuri, hivyo kushindwa kutoa maoni yao kwa mujibu wa sheria.

Rufaa hiyo ilipoitwa kusikilizwa, wakili aliyekuwa akimwakilisha kortini, Daud Mahemba aliiambia Mahakama kuwa wanaachana na hoja hiyo ya tatu na kwamba hoja mbili zilizobaki, atazielezea (arguing) zote kwa pamoja.

Katika kuunga mkono sababu za rufaa, wakili huyo alisema kesi ya upande wa mashtaka haikuthibitishwa kwa viwango vinavyokubalika, huku akisema maudhui ya maelezo ya shahidi wa nne na ushahidi wake kortini unatofautiana.

Kuhusu silaha iliyotumika, wakili huyo alisema uchunguzi wa miili ya marehemu ilionyesha walishambuliwa na kitu butu, lakini kwenye maelezo yake shahidi huyo alieleza polisi kuwa silaha iliyotumika kuwaua ni panga.

Hata hivyo, wakijibu hoja hizo, Isihaka Ibrahim na Agma Haule ambao ni mawakili wa Serikali, walipinga rufaa hiyo wakisisitiza kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila kuacha shaka na kustahili adhabu hiyo ya kunyongwa.

Katika hukumu yao baada ya kusikiliza hoja hizo, jopo la majaji hao watatu walisema dosari na mkanganyiko ulioelezwa na mrufani ni mdogo na hawajaona kitu chochote cha msingi kutilia shaka ushahidi wa shahidi wa nne.

Kama ilivyokuwa kwa jaji aliyemhukumu adhabu ya kifo, majaji hao nao walisema wanaona upande wa mashtaka ulithibitisha shtaka na kwamba ujio wa mrufani nyumbani kwa familia ya Magweiga ulikuwa ni wa shari.

Majaji hao walisema wanakubaliana na jaji huyo kwamba ugomvi ulitokana na shahidi wa nne kushindwa kurejesha ng’ombe aliotoa kama mahari na tishio la mke wa shahidi huyo kuita polisi, kitendo alichoona ni kama kumtukana.

Majaji wakasema mrufani akaamua kuua watoto wasio na hatia, ili kuonyesha haogopi chochote na kwa mrufani yeye aliona ndio njia nzuri kwake bila kujali thamani ya uhai haiwezi kuthamanishwa na ng’ombe wa shilingi milioni moja.

Kulingana na majaji hao, kulingana na ushahidi na mazingira ya kesi hiyo, hakuna kinachoonyesha kuwa mbali na mrufani huyo kuna mtu mwingine aliyefanya mauaji hayo zaidi yake, hivyo wakabariki adhabu ya kifo aliyohukumiwa.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts