Kilwa. Baadhi ya wakulima wa zao la ufuta kutoka kijiji cha Zinga Kibaoni ambao ni wanachama wa Kibaoni Amcos wilayani Kilwa mkoani Lindi, wamelalamika kucheleweshewa malipo yao baada ya mnada wa ufuta kufanyika.
Wakulima hao wamesema wanashangaa na hawaelewi ni kwa nini wanacheleweshewa malipo ilhali wanaona kila siku magari yanakwenda kuchukua ufuta katika ghala lao.
Wameyasema hayo leo Julai n28,2024 kwenye mnada wa saba wa zao hilo uliofanyika katika Kijiji cha Zinga Kibaoni katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
Mwananchi imezungumza na Mwenyekiti wa Kibaoni Amcos, Bakili Kilete ambaye amekiri malipo ya wakulima hao kuchelewa kutokana kuwapo kwa uchache wa wafanyakazi wanaoshughulikia uhakiki na ulipaji wa fedha hizo.
“Tunachelewa malipo sio tatizo la chama kikuu cha Lindi Mwambao na wala sio benki, ni sisi wenyewe. Tuna wafanyakazi wachache. Mnada unapofika, tunaweza kuwa na tani 800 hadi 1,000, hivyo tunachukua muda mrefu kufanya uhakiki hadi kufikia katika malipo.”
Lakini amesema wanapambana kuona kero hiyo inamalizika na wakulima wanalipwa kwa wakati.
Kilete amesema kuna baadhi ya Amcos wakulima wake walishalipwa fedha za minada mitatu lakini Amcos yao imeshalipa fedha za minada mitano.
Awali akizungumza na Mwananchi, mkulima wa ufuta, Ramadhani Haji amesema wanakumbana na changamoto ya kucheleweshewa malipo yao na hawafahamu shida ni nini.
“Nimepima ufuta tokea tarehe 20 mwezi huu lakini sijalipwa na sijui ni kwa nini. Magari yanafika kuja kuchukua ufuta na mnada unafanyika lakini majina ya wanaostahili kulipwa yanarudi machache, hili linatushangaza,” amelalamika Ramadhani.
Naye Kurwa Masigani amesema mkulima kucheleweshewa malipo ni kumrudisha nyuma kwa sababu anapokwenda kupima ufuta anatarajia apate fedha zake aanze maandalizi ya mashamba lakini pia, kununua mahitaji mengine ya familia.
“Sasa kama mtindo huu utaendelea, itawavunja moyo wakulima katika msimu ujao,” amesema Masigani.
Akizungumzia bei, mkulima Mwanaidi Hashimu amesema bado ni nzuri licha ya changamoto ya malipo wanayokumbana nayo sasa.
“Mkulima anapolima anatarajia apate pesa. Sasa anapocheleweshewa inakuwa sio vizuri kwa sababu unamuondoa katika malengo yake. Hivyo watulipe kwa wakati ili tukafanye mambo yetu tuliyoyapanga,” amesema Mwanaidi.
Katika mnada huu wa saba unaoendeshwa kwa njia ya mtandao ukisimamiwa na ofisi ya uendeshaji biashara ya soko la bidhaa Tanzania (TMX) pamoja na chama kikuu cha Lindi Mwambao, kilo moja ya ufuta imeuzwa kwa bei ya juu Sh3,480 na bei ya chini ni Sh3,200.