Beatrice anayetamani kina Job wa soka la Wanawake Moro

MWENYEWE anasema ndoto aliyonayo ni kutaka kuona Mkoa wa Morogoro unafunika katika soka la Wanawake kama ilivyo kwa vipaji kibao kinavyotawala ndani ya Ligi Kuu Bara.

Huyu ni Beatrice Seleman, Mwenyekiti wa Soka la Wanawake Mkoa wa Morogoro, alichukua kijiti cha Edna Lema, kocha wa zamani wa Biashara United aliyerejea Yanga Princess inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) aliyemaliza muda tangu Desemba mwaka jana.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na bosi huyo wa TWFA- Morogoro na kuweka wazi mipango aliyonayo sambamba na kiu ya kutaka kuona mkoa huo unatamba katika WPL kama inavyofanya katika soka la wanaume nchini wakiongozwa na kina Dickson Job, Nickson Kibabage, Abutwalib Mshery na Kibwana Shomary waliopo Yanga, Shomary Kapombe, Mzamiru Yassin na wengineo waliopo Simba mbali na Shiza Kichuya.

Beatrice anasema kuongoza soka la wanawake sio mgeni kwani alishaanza kujihusisha na masuala ya uongozi tangu mwaka 2003, alipokuwa Katibu Mkuu Chama cha Soka la Wanawake Lindi, lakini baadae aliula na kuwa Katibu Msaidizi wa Chama cha Soka cha Lindi kwa soka la wanaume.

“Mie ni mzoefu wa uongozi wa soka, ndio maana naamini nikishirikiana na wenzangu Morogoro itakuja kufunika katika soka la wanawake kama ilivyo kwa wanaume kutoka mkoa huo,” anasema Beatrice akiumizwa na mkoa huo kutokuwa na timu ya WPL.

Juu ya safari ya kuongoza soka la wanawake Morogoro, anasema ilikuwa ngumu maana kabla ya kuwa mwenyekiti alikuwa katibu mkuu wa chama hicho na anataja sababu zinazokwamisha soka la wanawake Morogoro ni wazazi kutokuwa na mwamko wa kuruhusu watoto wa kike kujishughulisha na soka hilo.

“Katika mikoa yote hapa nchini, Morogoro ndio unaoshika mkia kwa kutochezwa mashindano yoyote yanayowahusisha wanawake, sio soka la wanawake tu, hata michezo mingine kutoka na wazazi wengi kutokuwa tayari kuwaacha watoto kwenda kucheza, husuaani soka lakini nilivyoingia na kuwa mwenyekiti  tumekuwa tukitoa elimu nashukuru kwa sasa tunaweza kucheza ligi na watoto wa kike wakaja kwa wingi.”

Beatrice pia anafichua yeye pia ni Mjumbe wa Chama cha Netiboli Morogoro akiwa pia ni mwamuzi wa kimataifa wa mchezo huo na kitaaluma ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mchikichini A, iliyopo Manispaa ya Morogoro. Juu ya kusimamia michezo tofauti na Uenyekiti wake TWFA Morogoro, anasema bado haiathiri utendaji wake, kwani yote ni michezo na anashirikiana na wenzake kuona kila kitu kinaenda sawa.

Mwenyekiti huyo anasema akiishirikiana na wenzake wana mikakati mingi hasa ikilenga Ligi Kuu (WPL) na kufafanua; “Mkakati uliopo ni kuhakikisha kila wilaya ya mkoa huu inacheza Ligi ya Wanawake ili wachezaji wa kike wawe wengi, na kwa kuwa G-Seven imetwaa ubingwa wa Ligi ya mkoa sasa tutashirikiana na viongozi na wadau wengine kuhakikisha tunaipambani ili ije upada daraja na kucheza Ligi Kuu.”

“Katika kuhakikisha soka la wanawake linakuwa katika mkoa wetu, sisi kama chama tumeshaanza kuongea na wadau mbalimbali wenye vituo vya kulea na kuendeleza vipaji vya soka ili waanzishe programu maalumu za wachezaji wa kike ili tuibue vipoaji vingi kama ilivyo kwa soka la wanaume maana kwa sasa akademi zinazoibua vioaji vya soka la wanawake tuna Home Ifakara Queens na Mteule Queens lengo ni kuona hizi zinaongezeka ili vipaji vikuzwe kwa wingi.”

Juu ya kusaka vipaji kuanzia chini kwa mabinti wadogo anasema wataanzisha mashindano maalumu kwa ajili ya wasichana hao.

“Kwa kuwaMorogoro tumechelewa katika soka la wanawake tumeshaanza maandalizi ya kucheza mashindano ya Ligi za Vijana kwa wanawake ili tuweze kuwakuza wachezaji wa kike katika mkoa huu waweze kujua soka tangu wakiwa wadogo na mashindano yetu tutaanza na watoto wa kike wa miaka 15 kurudi chini maana tunataka mkoa ukue kwa kasi upande wa soka la wanawake,” anasema Beatrice.

Anasema anapambana na wenzake kuhakikisha wanaondoa dhana potofu juu ya watoto wa kike kucheza soka tofauti na ilivyon kwa watoto wa kiume.

“Kwenye maeneo mengi nchini na duniani kwa ujumla, watu walizoea kuona wanaume pekee ndio wenye nafasi ya kucheza, sasa wanawake nao walipoanza kucheza ikaonekana kama uhuni na utovu wa nidhamu kwa wanawake, lakini kwa sasa soka limekuwa ajira kubwa na wachezaji wengi wa kike wanaendesha maisha kupitia soka,” anasema Beatrice na kuongeza;

“Hivyo sisi kama TWFA Mkoa wa Morogoro tutakuwa daraja kwa wachezaji wa kike kutengeneza maisha kupitia soka maana tunataka usawa na siu sio nyingi tytafika kule wanaume waipo maana wadau wameanza kutuunga mkono.”

“Ndoto yangu katika uongozi wa soka la wanawake mkoani hapa ni kuhakikisha tunapata timu tatu zitakazocheza WPL na kutamba kama ilivyo mikoa mingine hususani Dar es Salaam iliyotawala ligi hiyo tangu ilipoasisiwa mwaka 2016,” anaongeza Beatrice.

Anasema jeuri hiyo inatokana na kuamini Morogoro imesheheni vipaji kwa mchezo wa soka kwa wanaume na wanawake hivyo kiu aliyonayo ni kuona kila wikiendi Uwanja wa Jamhuri unakuwa bize kwa kutumika kwa mechi mbalimbali za soka hususani za wanawake.

“Changamoto kubwa ninayopata katika kukiendesha chama hiki ni fedha, mana ili maendeleo yapatikane lazima fedha iwepo, sasa kwakua changamoto hii sio ya kwangu morogoro pekee, ninaendelea kutengeneza wadau ambao watakuja kutuunga mkono katika kufikia ndoto zetu na tutahakikisha tunapata wadhamini ambao watawekeza kwenye soka la wanawake ili watusaidia kutimiza ndoto za mabinti wengi”

“Kutokana na kuona tatizo la ukosefu wa fedha kwenye chama, na uendeshaji wake ukawa mgumu, mimi kwa kushirikiana na viongozi wenzangu, tuliunda bodi ya wadhamini wa chama cha soka la wanawake  mkoani hapa ambayo itasimama kama mlezi na pale itakapobidi kutusaidia kupata fedha za kuhakikisha shughuli za  soka la wanawake linakua kwa kasi katika mkoa wetu”

Beatrice ametoa ushaurio kwa wachezaji wa kike na pia kukemea tabia ya baadhi yao kupenda kubadilisha muonekano wao mara wanapojiingiza katika soka la wanawake, akisema hiyo ndio inayofanya wazazi wengi kupata wasiwasi, ilihali kinachofanywa ni kasumba kwa baadhi ya mabinti wenyewe kwa ulinmbukeni tu.

“Ili mchezaji aweze kucheza soka na kufikia malengo yake wachezaji nashauri awe na nidhamu ushauri wangu ni kwamba kama mchezaji hana nidhamu hawezi kupata maendeleo hivyo nawashauri wachezaji wote wa kike katika mkoa huu kwamba wajitunze, wasitumie dawa za kulevya na waache tabia ambazo sio nzuri kwa jamii wakifanya hayo watafika mbali,” anasema Betrice na kuongeza;

“Pia sivutiwi kabisa na hizi za tabia za wachezaji wa kike ambao wakicheza soka kidogo wanabadili mitembeo na kutembea kama wanaume, kuongea sauti kama wanaume hilo hatutakubali tunataka mtoto wa kike abakie na jinsia yake ili atimize ndoto zake, mbona kule Ulaya wanasojka wa kike ni warembo mno.”

Kauli ya bosi huyo wa TWFA-Morogoro inafanana na aliyowahi kuitoa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyekemea pia kasumba hiyo ya watoto wa kike wanaocheza soka kujiweka kiume zaidi, ilihali wanaweza kuliamsha uwanjani wakiwa na urembo wao kama walivyo wanamichezo wengine nje ya soka.

Related Posts