KUFUNGIWA KIBOKO YA WACHAWI: Serikali, waumini hapajaeleweka

Dar es Salaam. Wakati waumini wa Kanisa la Christian Life, maarufu ‘kanisa la Kiboko ya Wachawi’ wakipinga kufungiwa kwa huduma hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema suala hilo halihitaji nguvu na watalimaliza.

Barua ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia ya Julai 25, 2024 ambayo Mwananchi imeona nakala yake, imewaelekeza Mwenyekiti wa Kanisa hilo na Mchungaji Dominique Dibwe, maarufu Kiboko ya Wachawi’, anayeliendesha kufunga tawi la kanisa hilo lililopo eneo la Buza kwa Lulenge, Wilaya ya Temeke jijini hapa.

Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kile kinachoelezwa mchungaji wake anafanya vitendo ambavyo ni kinyume cha matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Namba 3 ya Mwaka 2019, vyenye athari ya kusababisha kanisa hilo kufutiwa usajili wake na kuondolewa kwenye Rejista ya Jumuiya za Kiraia zilizosajiliwa.

Miongoni mwa sababu zilizotajwa kusababisha kanisa hilo kufungwa ni pamoja na kutoa mafundisho yenye kuleta taharuki katika jamii na mahubiri ambayo ni kinyume cha maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.

Madai mengine ni kutoa mahubiri yanayodhalilisha watu madhabahuni, mahubiri chonganishi na kuhamasisha waumini wa kanisa hilo kuua watu kwa dhana au tuhuma za uchawi au ushirikina.

Barua hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha imetolewa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ilieleza madai hayo yanakwenda kinyume cha imani ya Kikristo, Katiba na kanuni za kanisa hilo, ikiwamo kuweka kiwango cha Sh500,000 kwa waumini  kupata huduma ya maombezi.

Hata hivyo, licha ya katazo hilo, bado Mwananchi Digital imeshuhudia waumini waliofika kanisani hapo leo Jumapili Julai 28, 2024 wakiendelea na maombi huku wakipinga maagizo hayo ya Serikali.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema suala la imani halipaswi kutumia nguvu kulishughulikia na kama watakosa huduma, hawawezi kuendelea kwenda.

“Kanisa limefungwa jana au juzi, kilichotokea kilitarajiwa, watu wamekwenda na wamekuta hakuna huduma, wataambiwa sababu na hadi kufika jioni wote watakuwa wameondoka,” amesema.

Mapunda amesema: “Kukiwa na kondoo halafu hakuna mchungaji, kondoo watatawanyika kwenda maeneo mbalimbali kutafuta malisho…sasa kama kanisa limefungwa na hakuna huduma unategemea nini.”

Naye, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kidagaa lilipo kanisa hilo, Shaban Ramadhan amesema wakiwa wasimamizi wa shughuli za Serikali katika eneo lao, watahakikisha maagizo yaliyotolewa kuhusu kanisa hilo yanasimamiwa.

“Hatuwezi kuwa tofauti na Serikali tunaangalia maagizo yaliyotolewa yanatekelezwa ipasavyo kama kutakuwa na tofauti tutakuwa wa kwanza kutoa taarifa sehemu husika,” amesema mwenyekiti huyo na kuongeza;

“Haya ya muumini mmoja akionekana kufanya hiki na kile kanisani ni ngumu kuyazuia tofauti na shughuli za jumla kama ilivyoelekezwa.”

Hali ilivyokuwa kwa ‘Kiboko ya Wachawi’

Pamoja na mtumishi wao maarufu Kiboko ya Wachawi kutokuwapo kanisani hapo leo Jumapili Julai 28, 2024, waumini walifika mapema sana asubuhi, baadhi wakiwa na taarifa ya kufungiwa kwa kanisa hilo na baadhi walikuwa hawajui wakatana nazo kanisani hapo.

Mwananchi ilifika kanisani hapa saa 3:00 asubuhi na kukuta waumini wamesimama kwenye makundi wakijadili kile kilichotokea, huku wengine wakipiga magoti katika madhabahu ya kanisa hilo wakiomba na kulia.

Wakati waumini wakiendelea kujadiliana, wengine walikuwa wakitoa mapambo yaliyokuwa yamewekwa madhabahuni.

“Watu hawaamini na kungekuwa na viti hapa wangekaa na kujaa, vilitolewa usiku kwa usiku nafikiri kuanzia saa tano,” amesema Mwanahawa Jumbe mama lishe anayefanya biashara yake jirani na kanisa hilo.

Anasema baadhi ya waamini hao wanatoka mikoani na wengine walifika jana na kulala kanisani hapo wakijua leo ibada itaendelea kama kawaida.

“Kama sasa hivi (saa 3:45) chai ingekua inakaribia kuisha, watu wamekunywa wamejaa lakini leo mpaka sasa maandazi yapo nusu ndoo na vitumbua pia, sioni dalili ya kumaliza biashara hii, binafsi nimeathirika kufungwa kwa kanisa hili,” amesimulia Mwanahawa.

Wakati mazungumzo yakiendelea baina ya mwandishi na mamalishe huyo, katika vikundi mbalimbali vya watu walivyokuwa wamesimama waliendelea kujadiliana namna ya kufuta adhabu hiyo.

Baadhi walidai kama kiongozi wao angefuatilia jambo hilo tangu jana, Julai 27, 2024 leo huduma ingeendelea kama kawaida.

“Tatizo jana alikuwa na birthday (kuadhimisha siku ya kuzaliwa)ya mtoto wake akawa ameweka nguvu zake huko vinginevyo leo shughuli zingeendelea kama kawaida,” alikuwa anasimulia mmoja wa waumini mbele ya wenzake.

Wakati watu wakiwa bado hawajui cha kufanya, kelele za kupinga kufungiwa kwa kanisa hilo zilianza kusikika na baadhi ya waumini wakaanza kuimba wimbo ‘Tunamtaka kiboko yetu’ huku wakilizunguka jengo la kanisa hilo, wakishinikiza kufunguliwa.

Lakini baadhi yao walikuwa wakishinikiza maandamano ya kwenda kituo cha Polisi Buza na wengine wakitaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saaam, Albert Chalamila apigiwe simu afike kanisani hapo watoe kilio chao mbele yake.

Wengine walipaza sauti wakitaka watu wachange fedha kidogo ili Sh500,000 ipatikane kwa ajili ya kulipa faini iliyokuwa imetajwa na Serikali wakidai kuwa huenda adhabu itatenguliwa.

Jordan Mwakyusa mkazi wa Dodoma amesema alifika jana kwa ajili ya kupata huduma baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu mchungaji wa kanisa hilo kupitia mitandao ya kijamii.

“Nimekuja huku mimi nina shida zangu, angalau nichukue maji na mafuta yakanisaidie katika mambo yangu, lakini wamemfungia, tunaomba Serikali kama kuna makosa ameyafanya yawekwe wazi au wamsamehe,” amesema Mwakyusa.

Kuhusu kutoza Sh500,000 kwa ajili ya kumuona mtumishi huyo, Mwakyusa ametolea mfano wa manabii wa zamani ambao alisema walikuwa matajiri lakini si kweli kuwa Mungu aliwashushia bali waliupata kutoka kwa wafuasi wao.

“Sijalazimishwa kuja, nimekuja na akili zangu timamu mimi Jordan Mwakyusa,” amesema Mwakyusa.

Mbali naye, baadhi ya watu wanashuhudia kupewa uponyaji wa magonjwa yao ikiwa ni baada ya kufuata huduma kutoka mikoani.

Subira Abdi ambaye awali alikuwa mkazi wa Tanga amesema alikuja jijini hapa mwaka jana kutoka mkoani Tanga akiwa na uvimbe kwenye  tumbo, lakini alipona baada ya kile alichodai alifanyiwa maombezi.

“Niliombewa, nikapewa na msingi (mtaji) wa Sh300,000 kati ya hiyo Sh200,000 nilifanya biashara na nyingine nilipanga chumba, nafanya biashara zangu hapahapa kanisani,” amesema Subira.

Fatuma Jamal ambaye ni mama wa watoto wanne na mkazi wa Mbande Tambani amesema amehudhuria kanisani hapo kwa  wiki tatu lakini tayari ameona miujiza.

“Mtoto wangu alikuwa anakojoa kitandani kwa siku moja hata mara nne, nilipokuja hapa Jumapili ya kwanza nikachukua maji, mafuta na sabuni nikamfanyia vile nilivyoelekezwa amepona, mimi pia nilikuwa nimepooza upande mmoja nimepona,” amesema Fatuma.

Baadhi ya kinamama wao walikuwa madhabahuni wakiomba na kulia kwa machozi kutaka Mungu alikumbuke kanisa hilo na kuwatoa katika kipindi kigumu wanachopitia.

Kila mara kanisani hapa, watu walikuwa wakienda na upepo wa wakati huo mtu alipoanzisha wimbo waliitikia kuimba na alipokuja mwingine kusema waandamane walikuwa tayari, akija mwingine kusema wakaombe wanaelekea madhabahuni jambo linalowafanya kukosa msimamo.

Hata hivyo, wakati yote haya yakiendelea, mchungaji hakuwapo kanisani hapo huku watumishi wake wakigoma kuzungumza chochote juu ya kinachoendelea au alipo kiongozi wao na wengine walilazimika kujificha ili kuepuka kamera za vyombo vya habari.

Ilipofika Saa 6 mchana, baadhi ya watu walianza kuondoka, wengine waliendelea kukaa ndani ya kanisa na wengine waliodaiwa kuwa wagonjwa walikuwa wamelala sakafuni.

Ilipofika Saa 6:30 mchana, gari la Polisi likiwa na askari lilipita kanisani hapo, baadhi ya waumini walipoliona walianza kusambaratika kila mmoja akishika njia yake.

Kabla hili halijatokea, mmoja wa waumini ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake wala kuzungumza na vyombo vya habari, alionekana kusimama sehemu iliyoinuka huku akizungukwa na waumini akiwa amenyanyua simu juu na kuiwekea spika akidai alikuwa anampigia simu mkuu wa mkoa, ambaye hata hivyo simu hiyo haikupokelewa.

Sio mara ya kwanza Kanisa kufungiwa

Tukio la kufungiwa kanisa liliwahi kutokea tena Desemba 2022, waumini wa Kanisa la The Word of Reconciliation Ministries (WRM) lililoko Kivule-Matembele ya pili chini ya Nabii Nicholaus Suguye, pia walijikuta njia panda baada ya huduma kusitishwa.

Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi ili kuzuia huduma yoyote kufanyika kanisani hapo.

Tofauti na Kanisa la Kiboko ya Wachawi kudaiwa kukiuka taratibu za usajili, kwa Suguye ilielezwa kuwa kanisa hilo lilikuwa ni miongoni mwa taasisi ambazo hazijapata usajili rasmi, hivyo lilikuwa likituoa huduma bila vibali.

Related Posts