Taa 120 za sola zaibwa Moshi, halmashauri yaja na masharti kuzirejesha

Moshi. Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ipo tayari kurejesha taa za barabarani za umeme wa jua (sola) 120 zilizoibwa katika wimbi linaloendelea la wizi, lakini kwanza inataka kufahamu kiini cha kuibuka kwa uhalifu huo.

Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi wa manispaa hiyo, Mwajuma Nasombe wakati akijibu malalamiko ya wananchi wanaohoji ukimya wa halmashauri kufunga taa mpya na kurejesha taa katika barabara hizo muhimu.

Kwa miaka mitatu mfululizo, Mji wa Moshi na vitongoji vyake umeshuhudia wimbi kubwa la wizi wa taa hizo za sola pamoja na betri zake. Barabara zilizoathirika zaidi ni Sukari, Zara au Tembo na Bonite pamoja na baadhi ya kata.

Uchunguzi wa Mwanachi umebaini taa hizo zimekuwa na soko katika Wilaya ya Rombo ambako husafirishwa kwenda nje ya nchi.

Pia, baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Moshi hununua paneli na betri na kuzifunga katika nyumba zao.

Mbali na matumizi hayo, uchunguzi huo pia umebaini baadhi ya wamiliki wa malori yakiwamo ya mchanga hufanyia urekebishaji wa kiufundi na kuzifunga kwenye magari yao na wengine huzitumia kwenye mitambo.

Nasombe  amesema halmashauri yake ilifunga taa 765 lakini 120 zimeibwa sambamba na taa nyingine zilizofungwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), ambazo idadi yake haikuwekwa wazi.

Amesema moja ya mikakati waliyonayo ni kurudisha taa hizo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinazowekwa sasa, zinakuwa bora zaidi na miundombinu yake haiibiwi kirahisi kama ilivyotokea.

“Kabla ya kufunga taa mpya lazima kwanza tushughulikie na kiini cha uhalifu, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwenye uwekaji wa taa hizo. Tutaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na DC (mkuu wa wilaya) na vyombo vingine,” amesema.

Nasombe amesema kutokana na wizi wa taa hizo, tayari wamefungua kesi 34 na kati ya hizo, 20 bado zipo chini ya upelelezi, tisa zimemalizika mahakamani na wahusika kupewa adhabu mbalimbali, huku tano zikiendelea mahakamani.

Amesema kuanzia mwaka 2019 hadi 2021, manispaa hiyo iliweka taa za barabarani 765 katika maeneo mbalimbali na 120 kati ya hizo ziliibwa na kwamba kwa sasa wanaendelea na jitihada ili kuzirudisha.

“Pia, zipo taa zilizowekwa na Tarura ambazo takwimu zake wanaendelea kukusanya, lakini pia zenyewe nyingi zimeibwa,” ameeleza mkurugenzi huyo wa halmashauri.

Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo amesema taa 240 zitafungwa maeneo mbalimbali ya Mji wa Moshi katika mwaka wa fedha 2024/25, hasa maeneo yenye muingiliano mkubwa wa watu na makazi.

“Kulikuwa na tatizo la kuibwa kwa taa za barabarani kwenye naeneo ambayo, hayana muingiliano wa watu hasa nyakati za usiku, baadhi ya barabara ikiwamo Barabara ya Sukari, Bonite na Barabara ya Tembo zimeibwa sana,”amesema Tarimo.

Walichosema wananchi Moshi

Wakazi wa mji huo, Aloyce Ibrahimu wa Bonite na Hadija Alfan na Anna Kweka, wameelezea namna giza katika barabara ambazo taa hizo zimeibwa linavyohatarisha usalama wao.

Ibrahimu ameiambia Mwananchi kuwa wizi wa taa za barabarani umechangia kuongezeka kwa uhalifu katika maeneo hayo, hususani usiku kutokana na uwepo wa giza na pia kutoa mwanya kwa wahalifu kujificha.

“Kukosekana kwa taa za barabarani kumekuwa ni tatizo kwa kiasi kikubwa, kwamba kwa sasa maeneo ambayo hakuna taa ni vigumu kupita usiku,” amesema.

Hadija Alfan amedai giza limesababisha kuwepo kwa wizi usiku na vitendo visivyo vyema kulinganisha na kipindi ambacho taa zilikuwepo. Ameiomba Serikali kuingilia kati na kuhakikisha taa zote zilizoibwa zinarejeshwa.

“Zamani ulikuwa unatembea usiku bila wasiwasi, lakini sasa ni ngumu kwa sababu ya giza, ukichelewa tu mahali kama huna usafiri, unaanza kuwaza unarudije nyumbani, maana usalama unakuwa mdogo gizani,”amesema Hadija.

Anna Kweka, naye amesema ipo haja kwa Serikali kushirikisha jamii katika ulinzi wa taa za barabarani na kuhakikisha wanaokamatwa kwa kosa hilo wanachukuliwa hatua kali za kisheria, ili iwe fundisho kwa wengine.

Related Posts