Simba yashtuka yavuta kipa mpya

MABOSI wa Simba wameshtuka baada ya kupewa taarifa kwamba kipa Ayoub Lakred aliyeumia kambini Misri atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na fasta wakaamua kuingia sokoni kusaka kipa mpya na tayari mezani wana jina la Moussa Pinpin Camara.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezinasa ni kwamba, mabosi wa Simba wamelazimika kuzungumza na kipa huyo kutoka AC Horoya ya Guinea, ili aje kuziba nafasi ya Lakred wakati wakati akiwa nje ikizingatiwa makipa waliosalia kwa sasa sio wazoefu wa michuano ya kimataifa ambao wamepiga hesabu za fainali.

Lakred aliumia mazoezini katika kambi ya klabu hiyo, iliyopo jijini la Ismailia, Misri huku aliyekuwa kipa namba moja, Aishi Manula hajajiunga na timu tangu alipoumia na kukaa nje ya uwanja katikati ya msimu uliopita, hivyo kusaliwa na makipa wengine kama Ally Salim, Hussein Abel na Ahmed Feruzi.

Kigogo mmoja wa Simba, aliliambia Mwanaspoti kuwa, Camara atatua wakati wowote nchini kuanzia sasa ili kumalizia mazungumzo ya mwisho na kama watafikia mwafaka atasaini na kuisubiri timu inayotarajia kutua keshokutwa Jumatano kujiandaa na Simba Day na mechi za Ngao ya Jamii.

“Mbele yetu kuna mashindano mbalimbali, hivyo kuumia kwa Lakred, kumetupa wasiwasi ndio maana tulikuwa kwenye mazungumzo na Camara ambaye tulikuwa tunamfuatilia kwa muda mrefu, ana uwezo mkubwa akiwa sehemu ya kikosi chetu atakuwa msaada mkubwa,” alisema kigogo huyo.

Aliongeza kuwa, kama dili la Camara likitiki, wachezaji wa kigeni kati ya Willy Essomba Onana na Michael Fred mmoja wapo anaweza akakatwa ili kumpisha kipa hiyo mwenye umri wa miaka 25 na mzoefu wa mechi za kimataifa.

Tangu mwanzo kama Simba ingefanikiwa kuinasa huduma ya winga wa AS Vita, Ellie Mpanzu ambao walikuwa wanatajwa mmoja wapo angepunguzwa ni  Fred na Onana ambaye ilisemekana kapata timu Qatar.

Related Posts