Yanga yatwaa ubingwa Toyota Cup, ikiipa kisago Kaizer Chiefs

KIKOSI cha Yanga kimetwaa kwa kishindo ubingwa wa mashindano ya Kombe la Toyota, jijini Bloemfontein, Afrika Kusini baada ya jioni ya leo Jumapili kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya wenyeji Kaizer Chiefs.

Mabao yaliyoipa Yanga ubingwa,  katika mchezo huo yamefungwa na Prince Dube dakika ya 24, Clement Mzize dakika ya 62 huku Stephane Aziz Ki akipachika mawili dakika ya 45 na 62.

Kichapo hicho kinakuwa cha kwanza kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi aliyekabidhiwa kikosi hicho hivi karibuni, baada ya kuachana na FAR Rabat ya Morocco aliyoachana nayo kufuatia kukosa ubingwa wa Ligi ya Morocco ‘Botola Pro’.

Nabi mwenye uraia wa Tunisia na Ubelgiji, aliachana na Yanga  Juni 14, 2023, baada ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo kisha kuipeleka fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo.

Kuondoka kwa Nabi viongozi wa timu hiyo wakamteua Muagentina, Miguel Gamondi aliyetambulishwa Juni 24, 2023 huku msimu uliopita ambao ulikuwa wa kwanza kwake, akakipa kikosi hicho ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la FA.

Baada ya michezo hiyo ya Afrika Kusini, Yanga inarejea hapa nchini kujiandaa na Tamasha la Kilele cha Wiki ya Mwananchi ambacho kinatarajiwa kuhitimishwa rasmi Agosti 4, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Tamasha hilo la Wiki ya Mwananchi litakapohitimishwa ndipo macho na masikio yataelekezwa katika mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya timu hiyo dhidi ya Simba utakaopigwa Agosti 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kabla ya mchezo huo, ikiwa Afrika Kusini Yanga ilianza kushiriki michuano ya Mpumalanga International Cup 2024 ambapo ilianza kwa kichapo cha mabao 2-1, dhidi ya Augsburg inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani maarufu ‘Bundesliga’.

Baada ya kichapo hicho, Yanga ikasawazisha makosa hayo kwani mchezo uliofuatia dhidi ya wenyeji, TS Galaxy ya Afrika Kusini ilishinda bao 1-0, lililofungwa na nyota mpya wa timu hiyo, Prince Dube aliyejiunga nayo msimu huu akitokea Azam FC.

Related Posts