Dar es Salaam. Upasuaji wa watoto 40 wenye matatizo ya kuzaliwa nayo ya moyo uliofanyika kwa siku nane nchini umeokoa Sh1.2 bilioni ambazo zingetumika kama wangetibiwa nje ya nchi.
Madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka nchini Uingereza kesho Aprili 26, wanahitimisha siku nane za upasuaji wa watoto 40 wenye matatizo hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wamoyo amesema watoto 40 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na mdogo.
Amesema upasuaji huo umeokoa Sh1.2 bilioni, ambazo zingetumika kwenye matibabu ya watoto hao endapo wangepelekwa India au Afrika Kusini.
“India au Afrika Kusini, mtoto mmoja matibabu yake yanagharimu Sh30 milioni, kwa watoto 40 ni fedha nyingi tumeokoa,” amesema. Dk Kisenge amesema hadi leo Aprili 25, 2024 watoto 24 wamefanyiwa upasuaji wa tundu dogo na watoto 12 upasuaji wa kufungua kifua.
Amesema kesho Aprili 26, 2024 watakamilisha matibabu hayo.
Dk Kisenge amesema unafuu wa matibabu umechangiwa na madaktari wa mradi wa Little Heart, shirika unaoendeshwa na Shirika la Misaada la Muntada, kuja nchini na vifaatiba vyao vyenye thamani ya Sh1.5 bilioni.
Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Moyo kwa watoto JKCI, Dk Sulende Kubhoja amesema watoto hao walifanyiwa uchunguzi wakabainika na matatizo yanayohitaji upasuaji huo.
“Wote wanaendelea vizuri, wengine wameanza kuruhusiwa,” amesema.
Meneja wa miradi huo, Kabir Miah amesema kwa ujumla wameshafanya upasuaji kwa watoto 500 mpaka sasa.
“Shirika letu lina miradi mingi ikiwemo ya afya, elimu na maji na linafanya kazi katika nchi mbalimbali katika Bara la Afrika, tunafanya kazi katika nchi 30 ikiwamo Tanzania,” amesema.
Amesema hii ni mara ya tisa kuwapo Tanzania kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo na wameshafanya upasuaji kwa watoto 500.