Phillipe Kinzumbi aibua vita mpya

YULE winga Phillipe Kinzumbi amekuwa akiwaniwa na Yanga kabla ya dili kukwama, ameibua mapya kule DR Congo akikaribia kuziingiza katika mgogoro Raja Athletic ya Morocco dhidi ya klabu yake ya TP Mazembe.

Alichofanya Kinzumbi ni kwamba baada ya kuwabembeleza Mazembe kuilegezea Yanga kisha kumuuza hapa nchini, kisha klabu yake kugoma, akafanya uamuzi mgumu akikubali kuchukua fedha za Raja ambao walijua kwamba jamaa anamaliza mkataba wake msimu uliomalizika.

Kinzumbi alichukua Dola 30,000 (Sh80 milioni) za Raja ili msimu uliopita ukimalizika akasaini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Dola 200,000 (Sh 533 milioni) akibakiza kupewa 170,000 (Sh453 milioni).

Licha ya Kinzumbi kupambana na Mazembe ili wamlainishie kwa winga huyo kununua mkataba wake wa miaka miwili uliosalia, klabu hiyo ikaweka ngumu na sasa anahaha kuhakikisha anarudisha fedha hizo.

Taarifa kutoka Congo ni kwamba wakala aliyepewa dili hilo na Raja kuhakikisha Kinzumbi anatua Morocco kwa Waarabu hao, amepewa kazi ya kumsumbua winga huyo juu ya dili hilo au hatma ya fedha zao hizo.

Wakati huo, Mazembe wao wamekaa mkao wa hasira wakisubiri kupata uhakika wa Raja kufanya mazungumzo na Kinzumbi ambapo inataka kuwaburuza katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

“Sisi tunasikia tu bado hatujapata uthibitisho wa hilo kwa kuwa Kinzumbi tulishamueleza, hatutafanya uhamisho wowote kwasasa alikuja akaomba mara mbili kuwa anataka kuondoka, tukipata uhakika tutakwenda FIFA,” mmoja wa vigogo wa klabu ya Mazembe alisema.

Yanga ilikuwa inatamani kumchukua Kinzumbi, lakini baada ya mabosi wa klabu hiyo kugundua winga huyo bado ana mkataba mrefu, mabingwa hao wa Tanzania wakarudi nyuma katika dili hilo kisha baadaye kuangukia kwa Jean Baleke ambaye walipewa kwa mkopo akitokea Libya.

Related Posts