Azam kutesti kwa Wydad AC

BAADA ya juzi kulazimishwa sare ya 1-1 na Union Touarga, matajiri wa soka la Bongo, Azam FC leo usiku watashuka tena uwanjani kutesti mitambo mbele ya mabingwa wa zamani wa Morocco na Afrika, Wydad Casablanca ikiwa ni mechi ya mwisho kabla ya kuvunja kambi kurejea nchini.

Azam na Wydad zitaonyeshana kazi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaopigwa kuanzia saa 1:00 usiku mjini Benslimane, ukiwa mchezo wa mwisho kwa Wanalambalamba ambao wataanza safari ya kurudi nchini kujiandaa na msimu mpya wa mashindano.

Kabla ya kurejea nchini kwa ajili ya msimu mpya, Azam itapita Rwanda kwa ajili ya kushiriki tamasha la klabu ya Rayon Sports siku ya Agosti 3 ikienda sambamba na utambulisho wa kikosi kipya cha timu hiyo lililopewa jina la Azamka in Rwanda. Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Amahoro, jijini Kigali.

Juzi usiku timu hiyo ilitoka sare ya 1-1 na Touarga iliyomaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya Morocco, (Batola Pro), ikiwa juu ya Wydad iliyoshika nafasi ya tano, huku Raja Casablanca ikibeba taji, Azam ililazimika kuchomoa bao dhidi ya wenyeji kupitia kwa mshambuliaji mpya, Nassor Saadun aliyesajiliwa mwezi mmoja uliopita akitokea Geita Gold iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu.

Kwa mujibu wa ratiba ya mechi za timu hiyo ni kwamba leo inacheza na Wydad ikiwa ni ya tatu tangu iwe kambini Morocco, ya kwanza iliishindilia US Yacoub Mansour kwa mabao 3-0 kabla ya sare ya juzi.

Mapema kocha wa timu hiyo, Youssouf Dabo aliyepo nchini kwa mafunzo, alisema anaamini mechi hizo tatu ikiwa kambini na ile ya Rayon itaisaidia kuiweka timu katika nafasi nzuri ya kuanza msimu ikipangwa kucheza na Coastal Union mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 3 mjini Unguja.

Dabo alisema mechi ya Amahoro itaisaidia zaidi timu kwa mchezo wa marudiano dhidi ya APR katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Azam itawakaribisha wanafainali hao wa Kombe la Kagame 2024 siku ya Agosti 16 jijini Dar kisha kurudiana nao mjini Kigali, Agosti 23 na mshindi wa jumla atafuzu raundi ya pili na kuvaana na mshindi wa mechi kati ya JKU Zanzibar na Pyramids ya Misri.

Related Posts