TIMU za kriketi kutoka mataifa manane ya Afrika zinaanza kuwasili jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya michezo ya kufuzu ushiriki wa Kombe la Dunia kwa vijana wa umri wa chini ya miaka 19.
Moja ya mataifa hayo ni Nigeria ambayo wataanza kampeni ya kusaka tiketi kwa kucheza na wenyeji Tanzania katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Dar es Salaam Gymkhana siku ya Ijumaa, Agosti 2 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Atif Salim ambaye ni msemaji na ofisa habari na mawasiliano wa chama cha kriketi nchini, TCA, timu zote zinatakiwa kuwepo jijini kuanzia leo Jumatatu.
Ni mashindano yanayoratibiwa na chama cha kriketi duniani (ICC) na yataanza kutimua nyasi juma hili ili kupata timu za Kiafrika zitakazofuzu kucheza fainali ya Kombe la Dunia kwa divisheni ya pili.
Mechi kati ya Tanzania na Nigeria itachezwa siku ya Ijumaa kuanzia saa tatu na nusu kawenye Uwanja wa Dar es Salaam Gymkhana.
Siku hiyo hiyo, kwenye Uwanja wa UDSM, Ghana U19 watakwaana na Msumbjiji U19 na kesho yake siku ya Jumamosi, Agosti 3 mwaka huu, Sierra Leone watavaana na Rwanda katika mechi itakayopigwa saa tatu na nusu asubuhi, wakati uwanja wa UDSM utakuwa tena shuhuda wa mechi kati ya Botswana na Malawi.
Siku ya Jumatatu, Agosti 4 mwaka huu, Nigeria watakuwa tena kwenye Uwanja wa Gymkhana kupambana na Msumbiji wakati wenyeji Tanzania watakuwa wakiumana na Ghana kwenye Uwanja wa UDSM.
“Tumejiandaa vyema kwa mashindano haya makubwa na nina imani na timu yetu kufanya vizuri ili kupata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia kwa vijana walio chini ya miaka 19,” alisema ofisa habari huyo wa TCA.
Wakati huo huo, Tanzania imezidi kuimarisha mkakati wake wa kuandaa timu bora za kriketi kupitia vijana wa shule za sekondari na msingi nchini kote.
Viwanja vya kriketi katika mikoa ya Morogoro na Tanga vilipamba moto kwa mechi mbalimbali za mizunguko 20.
Katika mji wa Gairo, mkoani Morogoro, wasichana wa Shule ya Maghoigwa waliwaadhibu wenzao wa Lukungu kwa jumla ya mikimbio 33 katika mchezo wa mizunguko 20.
Wasichana wa Moghoigwa ndiyo walioshinda kura ya kubeti na wakafanikiwa kutengeneza mikimbio 103 huku wakipoteza wiketi 9 baada ya kumaliza mizunguko yote 20.
Ilikuwa ni alama kubwa sana kwa vijana wa Lukungu kwani jitihada zao ziligota kwenye kwenye mikimbio 70 baada ya wote kutolewa wakiwa wamemaliza mizunguko 15 kati ya 20.
Kezia Simon wa Maghoigwa ndiye alikuwa kinara wa ushindi baada ya kutengeneza mikimbio 32 akifuatiwa na mwenzake Anjela Baraka aliyetengeneza mikimbio 24.
Mjini Tanga, timu ya Shule ya Kwakaeza Boys iliifunga Shule ya Kange kwa wiketi 4 katika mchezo uliochezwa kwenye viwanja vya Popatlal mjini Tanga pia mwishoni mwa Juma.
Vijana wa Kange ndiyo walianza kubeti na jitihada zao ziliwafikisha kwenye mikimbio 53 baada ya wote kutolewa.
Kazi ya kuzisaka alama hizo haikuwa ngumu sana kwa vijana wa Kwakaeza kwani waliweza kuzipata na kuzivuka baada kutengeza mikimbio 56 huku wakipoteza wiketi 6 tu.
Mjini Morogoro, timu ya Mji Mkuu iliwabamiza Wasichana wa Jitegmee kwa wiketi 7.
Jitegemee ndiyo walioanza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 65 baada ya wote kumi kutolewa wakiwa wamekamilisha mizunguko 18.
Haikuwa kazi kubwa sana kwa wasichana wa Mji Mkuu kuyazidi matokeo ya wapinzani wao kwani walitumia wiketi tatu tu kupata mikimbio 71 na hivyo kuwatoa wapinzani wao kwa jumla ya wiketi saba.