Soka ni kama lilikuwa limepumzika baada ya msimu uliopita kumalizika lakini muda mfupi ujao, burudani zinarejea nchini kupitia matukio tofauti yahusuyo mchezo huo.
Na burudani hiyo inakuja kibabe ambapo ndani ya mwezi ujao wa Agosti kutakuwa na idadi kubwa ya matukio ya kisoka ambayo hapana shaka yanasubiriwa kwa hamu na wapenzi wengi wa mchezo huo.
Spoti Mikiki inakuletea matukio ambayo yataufanya mwezi Agosti uwe na mijadala ya kisoka kuanzia mwanzo wake hadi utakapomalizika.
Shughuli itaanza keshokutwa Alhamisi katika Ukumbi wa The Super Dome uliopo Masaki jijini ambako kutatolewa tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), kwa wanasoka waliofanya vizuri katika msimu wa 2023/2024.
İdadi ya tuzo 62 zitatolewa kwa watu walioshinda katika vipengele tofauti ambavyo vinashindaniwa kama orodha ya washiriki walioteuliwa kuingia katika kinyang’anyiro cha mwisho inavyoonyesha.
Baadhi ya vipengele vinavyoshindaniwa vinaonekana kuteka zaidi hisia za mashabiki na wadau wa mpira wa miguu nchini na hilo linachagizwa zaidi na viwango bora ambavyo vimeonyeshwa na washindani wake.
Kipengele cha mchezaji bora wa Ligi Kuu 2023/2024 ndio kitakuwa na ushindani mkali utakaowahusu nyota nane ambao ni Djigui Diarra, Stephane Aziz Ki na Ibrahim Hamad wa Yanga, Feisal Salum na Kipre Junior (Azam), Mohammed Hussein (Simba) na Ley Matampi (Coastal Union).
Kuna kipengele cha kiungo bora wa ligi kuu ambacho kinawaniwa na Aziz Ki, Kipre Junior na Feisal Salum pia kuna cha kipa bora ambacho washindani wake ni Diarra, Ayoub Lakred (Simba) na Matampi.
Pia kuna kipengele cha mchezaji bora wa ligi kuu ya wanawake msimu uliopita ambacho wanaoshindania tuzo yake ni Aisha Mnuka, Violeth Nicholaus na Vivian Corazone wa Simba, Stumai Abdallah (JKT Queens) na Kaeda Wilson (Yanga Princess).
Wachezaji watano wanawania tuzo ya mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB ambao ni Ibrahim Hamad, Kipre Junior, Stephane Aziz Ki, Feisal Salum na Clement Mzize.
Awamu hii kuna ongezeko la vipengele vitatu ambavyo havikuwepo hapo nyuma ambavyo ni mchezaji bora wa kiume wa Tanzania anayecheza nje ya nchi, mchezaji bora wa kike wa Tanzania anayecheza nje ya nchi na tuzo ya soka la ufukweni.
Tuzo ya mchezaji bora wa Tanzania wa kiume anayecheza nje inawaniwa na Mbwana Samatta, Novatus Dismas na Himid Mao wakati tuzo ya mchezaji bora mwanamke anayecheza nje inawaniwa na Aisha Masaka, Clara Luvanga na Opa Clement.
Tuzo ya mchezaji bora wa soka la ufukweni inawaniwa na Jaruph Juma, Yahya Tumbo na Abdillah Mohammed.
Kwa hapa nchini, Simba ina historia ya kuwa muanzilishi wa matamasha ya klabu kila msimu unapokaribia kuanza kwa ajili ya utambulisho wa nyota wapya wa vikosi vya timu ya wakubwa, timu za vijana na timu ya wanawake.
Mwaka 2009, aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali alianzisha tamasha hilo ambalo huendana na matukio mbalimbali kama vile kuchangia damu, kufanya usafi, kutoa misaada kwa makundi maalum na mwisho huwa na kilele chache ambacho kinaenda sambamba na mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya kikosi cha wakubwa cha Simba na timu kutoka nje ya nchi lakini pia na timu za vijana na wanawake nazo hucheza.
Kwa maana hiyo, mwaka huu, tamasha hilo litakuwa la 11 na ingawa bado Simba haijatangaza rasmi, tetesi zinaripoti kuwa timu ambayo itacheza nayo katika kilele cha tamasha hilo ambacho kimepangwa kuwa Agosti 8 mwaka huu ni APR ya Rwanda.
Ni katika kilele hicho ambapo kutakuwa na utambulisho wa wachezaji watakaounda vikosi vya timu zote za Simba kuanzia ya wakubwa, vijana hadi wanawake pamoja na mabenchi yao ya ufundi.
WIKI YA MWANANCHI- 04/08/2024
Mwaka 2019 Yanga nayo ilifuata nyayo za watani wao kwa kuanzisha tamasha lao ambalo walilipa jina la ‘Wiki ya Mwananchi’ ambalo nalo hufanyika kwa malengo yaleyale ya kutambulisha vikosi vya timu zake, kushiriki huduma za kijamii na siku ya kilele chake kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki.
Kwa maana hiyo, tamasha la mwaka huu litakuwa la saba kwa Yanga tangu ilipoanzisha jambo hilo na imepanga kilele chake kifanyike Agosti 4 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Bado Yanga haijatangaza timu ambayo itacheza nayo mchezo wa kirafiki katika kilele cha tamasha hilo mwaka huu.
Jambo la kushangaza, katika kikosi cha Yanga hivi sasa, hakuna hata mchezaji mmoja ambaye alishiriki tamasha la kwanza la ‘Wiki ya Mwananchi’ kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya kikosi ambayo imekuwa ikifanya.
Kabla ya msimu wa 2024/2025 kuanza, kutachezwa mechi nane za mashindano ya Ngao ya Jamii kuanzia Agosti 8 had 11 mwaka huu ambayo yatashirikisha timu nne ambazo ni Yanga, Azam, Simba na Coastal Union.
Timu hizo zilimaliza katika nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi msimu uliopita.
Agosti 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kutakuwa na mechi moja ya nusu fainali baina ya Yanga na Simba na katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kutachezwa mechi baina ya Azam na Coastal Union.
Baada ya hapo kutakuwa na mechi ya fainali na mshindi wa tatu ambazo zote zitachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Uhondo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao utarejea Agosti 16 ambapo timu 16 zitaanza kulisaka taji lake ambalo linashikiliwa na Yanga iliyotwaa msimu uliopita.
Bado ratiba ya msimu ujao haijatoka na timu 16 zitakazoshiriki ni Yanga, Simba, Azam, Coastal Union, Tanzania Prisons, KMC, KenGold, Pamba, Kagera Sugar, Singida Black Stars, Fountain Gate, Namungo, JKT Tanzania, Dodoma Jiji, Mashujaa na Tabora United.
MASHINDANO YA KLABU AFRIKA
Timu tano kati ya sita zinazoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya klabu Afrika zitakuwa na kibarua cha mechi za hatua ya awali ambazo zitachezwa Agosti.
Mechi za kwanza za raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitachezwa kati ya Agosti 16 na 18 na marudiano ni Agosti 23 hadi 25 kama ilivyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga itacheza na Vital’O ya Burundi, Azam itacheza na APR ya Rwanda na JKU itakabiliana na Pyramids FC ya Misri.
Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Uhamiaji itacheza na Al Ahli Tripoli ya Libya na Coastal Union itacheza na Bravos do Maquis ya Angola.