JULAI 9, 2022, ilikuwa siku ya kihistoria kwa mashabiki na wanachama wa Yanga baada ya kumchagua Injinia, Hersi Said kuwa rais wa klabu hiyo huku akiwa ndiye mgombea pekee katika kinyang’anyiro hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi huo, Wakili Ally Mchungahela, alisema katika mkutano huo kwamba, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mgombea akiwa mmoja mkutano Mkuu unapitisha azimio la mgombea huyo kuwa Rais.
“Wajumbe mnaridhia Hersi Said kuwa Rais wa Klabu ya Yanga,” alisema Mchungahela huku wajumbe wakiitikia kwa kauli moja ya ndio, kisha akarudia tena mara tatu huku wakionekana pia wanaunga mkono na ndipo Hersi akatangazwa Rais wa timu hiyo.
Baada ya kuchaguliwa Hersi huku akionekana mwenye furaha, ndipo alipoainisha ahadi sita (6) ambazo atazitekeleza katika kipindi chake.
Ahadi ya kwanza ambayo aliwaahidi wanachama ni miundombinu ya klabu kwa maana ya ujezi wa uwanja wa mechi wenye uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 20,000 uliopo Kaunda Jangwani, marekebisho ya jengo la klabu na kuendeleza kituo cha mazoezi Kigamboni.
Ukiangalia ahadi hizo, unaona tayari Hersi anaishi katika ndoto ambazo aliwaahidi wanachama Julai 9, 2022 kwa sababu kuna mwanga unaonekana hasa maendeleo ya Uwanja wa Kaunda huku marekebisho ya jengo la klabu yakiwa yameshafanyika.
Suala la uwanja linaonekana lipo katika hatua nzuri kwani katika mkutano mkuu wa Yanga uliofanyika Juni 9, 2024, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa alitoa ridhaa juu ya hilo.
“Tumewapa muda wa kuyafanyia kazi yale ambayo tumewaambia kwenye uwanja huo, ila mkishindwa tutawanyang’anya, tumewapa kipimo, hivyo mzingatie iendane na mpango wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa la kisasa,” anasema.
Kauli hiyo ya Mchengerwa, ilionyesha nyuso zenye bashasha kwa mashabiki wa Yanga huku wakiamini ndoto ya uwanja itatimia Jangwani.
Ahadi nyingine ambayo Hersi aliitoa katika mkutano wa uchaguzi, ni kuimarisha uchumi wa klabu kupitia kwa miradi ya usajili wa wanachana, miradi ya usajili wa mashabiki, kuvutia wadhamini mbalimbali na kuvutia wawekezaji jambo ambalo ametekeleza.
Kuimarisha uchumi kwa klabu sio jambo jepesi na kwa mfano mzuri tu, katika mkutano mkuu wa Juni 9, 2024, klabu hiyo ilitangaza kupata hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni kwa mujibu wa ripoti yake ya mapato na matumizi kwa msimu wa 2023/2024.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Yanga uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ilionyesha ilipata Sh21.19 bilioni lakini matumizi yalikuwa ni Sh22.29 bilioni.
Ukiangalia suala hilo utaona ni wazi bado tuna safari ndefu kwa klabu zetu kujiendesha kisasa na kupata faida japo kwa uongozi wa Hersi kuzungumza hasara iliyopatikana kwa msimu wa 2023/2024 ni kuonyesha ukakamavu na weledi kwa kiongozi.
Ukiachana na hilo, Hersi pia aliahidi kujenga kikosi imara kitakachoweza kuleta mataji na kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo kuanzia Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la FA, Ngao ya Jamii na michuano ya kimataifa ya CAF.
Kujenga kikosi imara, ni dhahiri Hersi amefanikiwa kwani katika uongozi wake tayari Yanga imechukua mataji yote ya ndani huku akiiwezesha timu hiyo kufika hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998.
Mbali na hilo, msimu uliopita Yanga ilifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipotolewa kwa penalti 3-2, dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini baada ya timu hizo kutoka suluhu katika michezo yao yote miwili.
Kutolewa kwa Yanga msimu uliopita huku ikishuhudiwa timu hiyo ikinyimwa bao la wazi la Stephane Aziz Ki kwa kigezo cha mpira kutovuka mstari wa kati, ni ishara tosha inayoonyesha kikosi hicho kina wachezaji wazuri na wenye uwezo mkubwa.
Kuthibitisha hilo, msimu ujao tayari timu hiyo imefanya usajili mzuri baada ya kumsainisha kiungo Mzambia Clatous Chama aliyetokea Simba huku ikimuongeza pia kikosini aliyekuwa nyota mshambuliaji wa Azam FC raia wa Zimbabwe, Prince Dube.
Kama haitoshi, ikamuongeza pia kikosini aliyekuwa nyota mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke ambaye msimu uliopita alikuwa anaichezea Al-Ittihad SCS Tripoli ya Libya kwa mkopo akitokea TP Mazembe ya DR Congo ikiwa ni mmoja wa usajili bora.
Licha ya mafanikio hayo makubwa kwa Hersi, moja ya changomoto anayoendelea kukabiliana nayo ni ahadi ya kujenga timu imara za vijana na wanawake kuanzia chini ya miaka 17, 20 na ile ya Yanga Princess ambazo kwa upande huo hajafanikiwa.
Ahadi nyingine aliyoitoa ni ya kuongeza ushirikiano baina ya klabu, wanachama, mashabiki wake na wadau mbalimbali ikiwemo idara za Serikali, sekta binafsi, waandishi wa habari na Watanzania kwa ujumla ambapo hadi sasa tumeona akilitimiza kwa vitendo.
Katika ahadi zote ambazo Hersi alizitoa, licha ya baadhi kuonekana kutokamilika ila ni dhahiri kuna mwanga mkubwa unaoonekana ndani ya kikosi hicho huku akiwa ni mmoja ya viongozi wenye maono makubwa kwenye soka la nchi hadi kimataifa.
Kuonyesha hilo, Desemba Mosi, 2023, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lilizundua Chama cha Klabu za soka Barani Afrika (ACA) huku ikimchagua Hersi Said kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chama hicho chenye makao yake makuu jijini Nairobi, Kenya.
Katika uzinduzi huo uliofanyika Misri na kusimamiwa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe, Jessica Motaung wa Kaizer Chiefs aliteuliwa Makamu Mwenyekiti wa Hersi huku Paul Basset wa Akwa United ya Nigeria akiteuliwa Makamu Mwenyekiti wa Pili.