Simulizi ya aliyefungwa kwa kumkashifu Rais baada ya kuachiliwa

Bariadi. “Maisha yangu yamebadilika. Mfumo wangu wa maisha wote umerudi nyuma, kwa sasa ni kama naanza upya kwa kuwa shughuli zote nilizokuwa nazifanya, ikiwemo kusimamia kandarasi ya majengo mbalimbali zimesimama.”

Huyo ni Levinus Kidanabi (35) almaarufu kama ‘Chief Son’ aliyehukumiwa kifungo cha miaka saba jela na faini ya Sh15 milioni kwa makosa matatu, likiwamo la kumkashifu Rais Samia Suluhu Hassan, akisimulia madhara aliyoyapata baada ya kutoka kifungoni.

Oktoba 19, 2022 akitoa hukumu hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Simiyu, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Matha Mahumbuga alieleza kuwa mtuhumiwa alitoa taarifa za uongo kinyume cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015.

Awali, Wakili wa Serikali, Daniel Masambu ilieleza kuwa Chief Son alikuwa anashtakiwa kwa kosa la kuchapisha taarifa za uongo katika Jukwaa la Mtandao wa Whatsapp la ‘Simiyu Breaking News’.

Aprili 18, 2024 Kidamabi ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Bariadi, aliachiwa huru bila masharti yoyote baada ya kupunguziwa adhabu.

Akizungumza na Mwananchi Aprili 23, 2024, katika Kijiji cha Mwaunkwaya, Kata ya Banemhi Mkoani Simiyu, Kidanabi amesema anaamini kufungwa kwake jela kunatokana na fitina za kisiasa.

“Chanzo cha lile kosa nadhani ni fitina za kisiasa. Kwa mfano niligombea ujumbe wa halmashauri kuu CCM Wilaya ya Bariadi ilhali kesi ipo mahakamani. Nilichukua fomu, kesi ikiwa mahakamani na kamati ya maadili ya chama ilikaketi ikapitia jina langu na kulirudisha.

“Na kamati ya chama ikirudisha jina ina maana gani? ina maana kwamba huyu mtu ni msafi hana doa. Ilitoaje jina alafu nipatikane na hatia ya kumkashifu mheshimiwa Rais? Inaonesha kabisa ni suala ambalo lilitengenezwa kwa nia ovu ya kunichafua nionekane mimi sifai,” amesema.

Huku akimshukuru Rais Samia akiamini kwamba ndio sababu ya yeye na familia yake kuungana, baba huyo wa watoto wawili, anasema baada ya kutoka jela hali ya maisha imekuwa ngumu kwa kuwa tenda za usimamizi wa majengo alizokuwa akizifanya zote zimeyeyuka.

“Awali katika shughuli zangu za utafutaji nilikuwa na tenda za ujenzi wa miradi ya madarasa ikiwemo katika Shule ya Msingi Ng’hesha na katika Kituo cha Kulelea wazee wasiojiweza kilichopo Matongo, pia nilisimamia miradi kadhaa ikiwemo ya ujenzi wa jengo la kufulia la ‘Miswaki Laundry’, tenda hizo zote walizitaifisha, lakini namshukuru Mungu nimetoka gerezani na sasa niko huru,” anasema Kadanabi.

Azungumzia ukosoaji wa viongozi

Akizungumzia umakini unaotakiwa kufanywa, hususan na vijana wanapokusudia kukosoa jambo fulani ambalo haliko sawa kwa viongozi, Kadanabi anasema wasiogope, cha msingi ni wao kuwa na uhakika na kile wanachokikosoa mitandaoni.

Kidanabi anasema mitandao ipo kwa ajili ya kuliwezesha Taifa kupata taarifa mbalimbali zikiwamo za kukosoa na kuelekeza nini kifanyike kwa afya ya nchi.

Anasema hapa nchini vijana wengi hutumia mitandao ya kijamii kukosoa, jambo wanaloona haliendi sawa lakini baadhi hujikuta wakiingia matatizoni.

Hata hivyo, anakiri wapo baadhi ya vijana hutoa taarifa za uchochezi kwa Taifa kupitia mitandao ya kijamii.

“Hili hata mimi sikubaliani nalo ni kosa linalotakiwa kuchukuliwa hatua,” amesema.

Hivyo, amewataka vijana kuacha kutumia nafasi walizonazo mitandaoni kuwasema vibaya viongozi wote bila kujali ni wa ngazi gani bali watumie nafasi hizo katika mitandao kujadili masuala yenye tija kwao na Taifa kwa ujumla.

Mama mzazi wa Kidanabi, Hollo Manyilizu alisema kuachiwa huru kwa mwanawe kumerejesha tumaini kwa familia hiyo.

Anasema kifungo cha miaka saba alichohukumiwa mwanawe kilimuacha njia panda asijue afanye nini, mkwewe na watoto wa Kidanambi.

Anasema siku alipopata taarifa kwamba mtoto wake kahukumiwa kwenda jela miaka saba alichanganyikiwa kwa sababu ndiye aliyekuwa akiihudumia familia yao.

“Moyoni mwangu nilikuwa namuomba sana Mungu atusaidie siku moja atoke akiwa salama, aje tuungane naye tuendelee na maisha na kweli Mungu amesikia kilio changu,” anasema James.

Mke wa Kidanabi, Aisha Ramadan anasema mumewe alipokuwa anafungwa alimuacha akiwa na ujauzito.

“Nilichanganyikiwa, sikujua cha kufanya, huku kijijini hatukuwa na biashara, nilimtegemea yeye na kazi zake alizokuwa anafanya, hivyo lilipotokea tukio hilo lilinichanganya mimi na mama mkwe hatukujua tufanye nini,” anasema Aisha.

Hata hivyo, anasema anamshukuru Mungu mumewe ametoka gerezani na amemkuta ameshajifungua mtoto ambaye ana mwaka mmoja na nusu sasa.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mayunga Ndongo anasema tangu aanze uongozi hajawahi kupokea kesi yoyote inayomtuhumu Kidanabi kutenda kosa kabla ya hili alilohukumiwa nalo.

Anasema kijana huyo mara zote alikuwa ni mtu mwenye kushirikiana na wenzake, taarifa za kukamatwa kwake zilimshtua.

“Kwa kweli taarifa hizo zilituchanganya kama viongozi wa eneo hili kwa sababu tuliishi naye vizuri na alikuwa kiongozi ndani ya chama chake cha siasa, lakini ndiyo hivyo, yaliyotokea ni hayo na leo yuko huru, tunamshukuru Mungu,” amesema mwenyekiti huyo.

Related Posts