BAADA ya kutwaa taji la Toyota Cup Afrika Kusini kikosi cha Yanga kinatarajia kuwasili alfajiri ya kesho.
Yanga imetwaa taji hilo baada ya kuifunga Kaizer Chiefs mabao 4-0 mchezo wa kimataifa wa kirafiki kwa timu zote mbili ambazo zinajiandaa na ligi na michuano ya kimataifa.
Akizungumza na wanahabari, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amewaita mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kuwapokea wachezaji ambao watawasili nchini sasa tisa alfajiri kuamkia kesho.
“Kuanzia saa saba usiku Wananchi mnatakiwa kuanza kujitokeza kwa wingi kuwapokea mashujaa wetu ambao wametwaa kombe ugenini,” amesema na kuongeza:
“Timu ikiwasili itaruhusiwa kuondoka kwenda kupumzika, lakini kombe tutabaki nalo na kutoka nalo uwanja wa ndege hadi makao makuu Jangwani kwa ajili ya kulihifadhi.”
Naye Ofisa Uhamsishaji wa Yanga, Haji Manara amesema Yanga imejitengenezea ubora na inaonyesha ukubwa wake kutokana na ubora wa kikosi ilicho nacho.
“Yanga imejitengenezea ubora na anaamini Kaizer Chiefs haiwezi kufikiria tena kuialika timu yetu kwa ajili ya mechi za kirafiki,” amesema.
Manara ametumia nafasi hiyo kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuujaza uwanja ili kushuhudia raha za kikosi hicho.