RAIS wa Kenya, William Ruto ameahidi kuwatafutia kazi pamoja na kuwalipia nauli ya ndege Wakenya waliopata kazi ughaibuni kwa lengo kuwatuliza vijana ambao wamekuwa wakimshinikiza ajiuzulu kwa kutotimiza ahadi alizotoa kabla ya kuchaguliwa 2022. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa… (endelea).
Akizungumza katika Kaunti ya Taita Taveta jana Jumapili, Rais alitangaza kuwa ana mpango wa kuharakisha kutolewa kwa pasipoti kwa wale ambao wanataka kufanya kazi nje ya nchi.
“Nimefanya kazi yangu, nimetafuta kazi mataifa ya nje. Nimepanga kuwa wale ambao wanaenda kufanya kazi hizo ng’ambo wapate pasipoti zao ndani ya wiki moja. Hata hawatahitaji pesa za kununua tiketi za ndege, tugharimia safari hizo,” alisema.
Ahadi yake imekuja wakati Idara ya Uhamiaji nchini humo ikipambana kuandaa na kuwapa Wakenya pasipoti zao baadhi wakiwa wamesubiri kwa zaidi ya miezi 12.
Kumekuwa na uhaba wa karatasi na mashine za kuchapisha na kuandaa pasipoti hizo.
Inadaiwa kuwa ufisadi na kiburi kwa wanaofanya kazi kwenye idara hiyo ni kati ya sababu nyingine ambazo zimefanya Wakenya wasipate pasipoti zao kwa wakati.
Novemba 2023, Rais Ruto alisema angetia saini mkataba na serikali za Ujerumani, Ufaransa, Saudi Arabia na mataifa ya Uarabuni ili Wakenya wasiokuwa na ajira wafanye kazi huko.
Hata hivyo, haikubainika ni nafasi ngapi za ajira ambazo zingetokea kutokana na maelewano hayo.
Jana Jumapili, Rais Ruto alisema serikali imewasaidia zaidi ya vijana 400,000 kupata kazi ng’ambo.
Aliwataka wabunge waandae vijana kwenye maeneo yao kujihusisha na mpango wa ajira nje ya nchi.
“Kila wiki vijana 1,000 huhamia nchi za nje. Taita Taveta sasa wanatakiwa wajiandae kwa zamu yao.
“Kwa wabunge, nimefanya kazi yangu ya kusaka kazi ng’ambo. Nimepanga kuwa kila mtu ambaye angependa kufanya kazi ughaibuni, anapewa pasipoti na stakabadhi nyingine ndani ya wiki moja,” alisema Rais.
Mbali na ajira za nje ya nchi, Rais Ruto alisema mpango wa kuanzisha ajira mitandaoni ambapo vijana watafanya kazi katika kampuni za mataifa ya nje wakiwa nchini mwao.
“Kwenye mpango wangu nataka vijana wawe na ajira ya maana. Hii ndiyo maana nimeanzisha mipango kama ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, ajira mitandaoni, Wakenya kufanya kazi nje ya nchi, viwanda ili kuwapa vijana wetu ajira ndipo tujenge taifa,” akasema.
Kiongozi wa nchi alieleza amekubaliana na wabunge kujenga vituo vya teknolojia kwa kutumia Hazina ya Fedha ya Kustawisha Maeneo bunge Nchini (CDF).
Serikali nayo itanunua kompyuta, kulipia intaneti na kuwalipa wakufunzi kwa vijana ambao watakuwa wakifanya kazi kwenye kampuni za ng’ambo na kulipwa dola za Marekani.