Kuuzwa soko la Kurasini, viongozi warushiana mpira

Dar es Salaam. Wakati viongozi wa soko la Kurasini, lililopo Mtaa wa Shimo la Udongo, barabara ya GSM jijini hapa, wakieleza wapo hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kuuza soko hilo, uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke umesema hautambui mauzo hayo.

Mbali ya halmashauri, uongozi wa mtaa na wafanyabiashara zaidi ya 160 waliopo sokoni hapo  wamesema hawajashirikishwa hivyo hawajui ni kwa namna gani wataondolewa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Shimo la Udongo, Gerold Manjoli amesema alipata malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu mchakato wa kuuza soko hilo kwa mwekezaji, naye aliyafikisha kwa halmashauri.

Manjoli amesema: “Ni jambo la ajabu soko lipo mtaani kwangu linauzwa sina taarifa, hata viongozi wake hawataki ushirikiano na uongozi wa mtaa. Wanajiona wao ndio wamiliki wa soko hivyo wana uamuzi nalo, hii si sawa na inasikitisha.”

Akizungumza na Mwananchi Digital, Katibu wa soko hilo, Bendickson Bazale amekiri kuwepo kwa mpango huo na kueleza kuwa wameshamaliza hatua zote, wanachosubiri hivi sasa ni kuingiziwa fedha kwenye akaunti ya soko ili wagawane.

“Fedha zimechelewa kwa sababu kuna mambo yamejitokeza yanayofanyiwa kazi na halmashauri, lakini kwa upande wetu tumemaliza kila kitu.”

Hata hivyo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Elihuruma Mabelya, Julai 25, 2024 aliliambia Mwananchi kuwa  hawahusiki na suala hilo na yeye analisikia kama wanavyolisikia wengine.

“Ninavyojua soko hilo na ardhi yake ni mali ya Serikali, taarifa kuwa panauzwa kwa mwekezaji hazina ukweli wowote,” alisema.

Alisema Wilaya ya Temeke ina masoko 29 kati ya hayo 27 yanamilikiwa na Serikali likiwemo la Kurasini na mawili ndiyo ya watu binafsi.

Alisema kama kuna mwekezaji anataka kununua eneo la halmashauri anapaswa kufuata taratibu ikiwamo kupeleka barua ya maombi kwa menejimenti, ambayo ikishajiridhisha hufikisha suala hilo kwa kamati ya fedha.

“Baada ya hapo kamati ya fedha itawasilisha taarifa kwenye baraza la madiwani kwa ajili ya kuridhia na siyo kama inavyoelezwa wamefanya wafanyabiashara huko.”

“Pia tunachojua wafanyabiashara hao ni wapangaji kwetu, hawana mamlaka yoyote ya kuuza soko na kama wamefanya hivyo hayo ni yao na mwekezaji husika wanayemjua wao, sisi tunachofahamu hadi sasa soko letu haliuzwi,” alisema.

Mwonekano wa vibanda vya Soko la Shimo la Udongo Kurasini jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Mabelya alisema jambo lililopo Kurasini ni kwamba, eneo hilo lote lilishatangazwa na Serikali kwa tangazo lake  la mwaka 2002 GN namba 52 kuwa ni kwa ajili ya uendelezaji na upanuzi wa bandari, hivyo mwekezaji yeyote hatapewa kibali cha kufanya shughuli nyingine isipokuwa za bandari.

“Nitumie nafasi hii, kwa mwekezaji yeyote anayetaka kuwekeza kwenye  maeneo yanayomilikiwa na Serikali asiende kufanya mazungumzo na watu binafsi au wafanyabiashara isipokuwa Serikali yenyewe na likitokea la kutokea sisi hatutahusika,” alisema.

Kwa majibu hayo, Mwananchi lilimtafuta tena katibu wa soko ambaye amesema hawezi kumjibu kiongozi huyo kwa kuwa ni mtu mkubwa ila ukweli anaujua kuhusu suala hilo.

“Ndugu mwandishi katika hili naomba nisijibu lolote, mkurugenzi anajua au hajui hiyo ni yeye, nisingependa kujibizana naye kwenye vyombo vya habari kwa kuwa yeye ni mtu mkubwa,” amesema.

Inaelezwa soko hilo dogo lenye eneo la mita za mraba 400 viongozi wamepanga kumuuzia mwekezaji kwa Sh365 milioni wafanyabiashara wakiahidiwa kulipwa kifuta jasho cha kuanzia Sh500,000 hadi Sh2 milioni mwekezaji atakapolichukua.

Katibu wa soko, Bazale amesema wameshampatia mwekezaji huyo ambaye hakuwa tayari kumtaja akaunti ya soko kwa ajili ya kuweka fedha hizo.

Amesema baada ya hapo wataitisha kikao na wafanyabiashara kila mmoja atapata mgawo anaostahili.

Kuhusu malalamiko ya wafanyabiashara kutoonana na mwekezaji huyo, Bazale amesema walizungumza naye kwa niaba yao kwa kuwa ingekuwa kazi ngumu wote kukutana ofisini kwake.

Lucy Trax, mmoja wa wafanyabiashara sokoni hapo akizungumzia suala hilo amesema anachokumbuka waliitishwa kikao Juni mwanzoni na kuelezwa na viongozi wao kwamba soko hilo linauzwa baada ya mwekezaji kupatikana na waliambiwa wajiorodheshe waliohudhuria.

“Kwa bahati mbaya  mahudhurio yale na saini zetu, viongozi ndio wakawa wanatumia kama makubaliano na kumpeleka mwekezaji, ambaye hatujawahi kuonana naye,” amesema.

Amesema walielezwa na viongozi wao kuwa  wamiliki wa vizimba watalipwa Sh2.4 milioni, wafanyabiashara wenye muda mfupi Sh1.2 milioni, huku wapangaji wataondoka na Sh500,000.

Ambroce Alphonce  amesema viongozi wanataka kuwazunguka kwa masilahi yao kwa kutaka kufanya biashara kama soko wanalimiliki wao.

Amesema wanapotaka taarifa kutoka kwa viongozi wao, wamekuwa wakali  jambo linalozidi kuwapa wasiwasi kuhusu kinachofanyika.

Related Posts