Butiku ataja yanayofifisha dhamira ya Muungano

Dar es Salaam. Hatua ya Tanzania kupangiwa bei ya kuuza bidhaa zake, kutojitosheleza kwa chakula na kuwa na mapato yasiyolingana na matumizi, yametajwa kuwa mambo yanayoongeza malalamiko ya wananchi dhidi ya Muungano na kuufanya uwe hafifu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) Joseph Butiku, sababu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kujenga nguvu ya pamoja na kuondoa unyonge kwa wananchi.

Mwanasiasa huyo mkongwe, amesema kuendelea kuwepo kwa unyonge unaosababishwa na mambo hayo, kunaifanya Tanzania iendelee kuwa na unyonge na hivyo kufifisha dhamira ya Muungano.

Tanzania kesho Aprili 26, 2024 inaadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa Aprili 26, 1964.

Mataifa hayo yaliungana chini ya uasisi wa Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika na Abeid Amani Karume wa Zanzibar.

Butiku ametoa kauli hiyo leo, Aprili 25, 2024 alipochangia mada ya umuhimu wa Muungano tulipotoka, tulipo na tunapoelekea, katika kongamano la miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililoandaliwa na Chuo cha Ustawi wa Jamii.

Aliwauliza waliohudhuria kongamano hilo kuwa, Muungano ulilenga kuwaondoa wananchi kwenye unyonge, je unyonge huo umekwisha?

“Mimi napenda kuwaambia ukweli kwa sababu sisi wazee tunasema ukweli. Unyonge haujaisha, umekwishaje kama hatujaweza kulima kujitosheleza kwa chakula ingawa tunalima,” amesema.

Kingine alichosema kinathibitisha kuendelea kwa unyonge ni Tanzania kupangiwa bei za karafuu inayolimwa Zanzibar na korosho inayolimwa Tanzania Bara.

Butiku amesema pamoja na mazao hayo kuzalishwa na Tanzania, lakini yanauzwa kwa bei ilivyopangwa na mataifa ya nje.

Ameeleza hilo linafanyika hata kwa bidhaa zinazotoka nje, bei zake zinapangwa na mataifa hayo.

“Kama anayepanga bei ya bidhaa zake na anayepanga bei ya bidhaa anazonunua kutoka kwako ni yuleyule, hapo unyonge umekwisha? Bado upo,” amesema.

Kwa mujibu wa Butiku, mazingira hayo yanasababisha mapato ya nchi yasilingane na matumizi na hata madeni yanaongezeka ingawa kwa sasa kuna unafuu.

“Katika biashara ya kimataifa, sisi bado ni wanyonge. Lingine hizi nguo zote mnazovaa zinatoka wapi, baiskeli za watoto wetu? Hapana huo ni unyonge,” amesema.

Ameeleza sharti la Muungano kudumu bila kutetereka ni kuzalisha mali na vitu tunavyotumia, tuwe na uwezo wa kuvitengeneza.

Kinyume cha kufanya hivyo amesema watu wataendelea kuwa wanyonge na kulalamikiana.

“Siku hizi hamjasikia watu wanasema msije huku hakuna ardhi ya kutosha? Basi mambo haya wakiendelea Muungano wetu unaweza kuwa hafifu,” amesema.

Ametumia jukwaa hilo, kueleza umuhimu wa kuhamisha mijadala kuhusu mataifa mawili yanayounda Muungano, badala yake watoto wamezeshwe umoja uliopo nchini.

Butiku aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongizwa na Jaji Joseph Warioba amesema wakati wa kukusanya maoni ya wananchi kipindi hicho, Zanzibar kulikuwa na sauti kubwa inayotaka serikali tatu na walikuwa na sababu.

Amesema sauti hiyo ilikuja kwenye mapendekezo na kwa sababu walitumwa maoni ya wananchi, walitoa mapendekezo kwa muktadha huo.

Amesema katika maoni hayo, hakukuwa na anayetaka kuvunja Muungano, bali walitaka kuwe na Serikali ya Zanzibar, Tanganyika na ile ya Muungano.

“Na tuliiweka vizuri kabisa kwamba Serikali ya Muungano imepewa vitu vingi, hii yote ni katika kuondoa kero na kuimarisha Muungano wetu,” amesema.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni amesema sababu za kufanyika kwa kongamano hilo ni kujenga uelewa kwa wanafunzi kuhusu Muungano.

Ameeleza sababu nyingine ni kuwafanya vijana wajione kuwa na wajibu katika Muungano.

“Sisi kama chuo kwa nafasi yetu tutahakikisha vijana wanaelewa na kujiona wana wajibu katika Muungano kupitia majadiliano na makongamano kama haya,” amesema.

Related Posts