Lindi. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameziagiza Wizara ya Kilimo na ile ya Viwanda na Biashara kuhakikisha korosho yote inabanguliwa nchini kabla ya kuuza nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Bodi ya Korosho Tanzania, asilimia 80 ya korosho zinazouzwa nje ya nchi ni ghafi, jambo linaloikosesha Serikali na wakulima wa zao hilo mapato ya kutosha kutokana na kuongeza thamani.
Dk Nchimbi ametoa maelekezo hayo leo Jumatatu, Julai 29, 2024 wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea alipoingia mkoani Lindi akitokea Mtwara alikoanzia ziara yake ya siku nne katika mikoa ya Kusini.
Amesema korosho ni mkombozi kwa wakulima wa mikoa ya Kusini, hivyo ni muhimu kuwa na mikakati ya kuwasaidia hasa kwa kuanzisha viwanda vya kubangua korosho ili kuwasaidia kuongeza thamani mazao yao.
“Naielekeza Serikali; Wizara ya Kilimo na ile ya Viwanda, zihakikishe korosho yote inabanguliwa Tanzania, tusiuze korosho ghafi,” ameelekeza Dk Nchimbi huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kumsikiliza.
Mtendaji mkuu huyo wa chama tawala amewataka wananchi kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa kuwa soko lake ni la uhakika na litawafanya wainuke kiuchumi kupitia uzalishaji wao mkubwa.
Awali, mkulima wa zao hilo, Maulid Burhan alieleza changamoto wanayokutana nayo ni upungufu wa mashine za kubangulia korosho, jambo linalowafanya wauze korosho ghafi na kuwakosesha mapato zaidi.
“Tunaomba tujengewe viwanda vya kutosha vya kubangulia korosho ili wakulima tuuze korosho iliyobanguliwa nje ya nchi,” amesema mwananchi huyo wakati akiwasilisha kero yake kwa Dk Nchimbi.
Akijibu changamoto hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred amesema bei za korosho ghafi katika miaka miwili iliyopita hazikukidhi matakwa ya wakulima kutokana na kushuka kwa mahitaji ya korosho katika soko la dunia.
Amesema uuzaji wa korosho za Tanzania zikiwa ghafi kwa zaidi ya asilimia 90 inategemea masoko ya India na Vietnam pekee.
Ili kupanua wigo wa soko, amesema Serikali imedhamiria kuongeza ubanguaji wa korosho na kufungua masoko mapya ya korosho Ulaya pamoja na uanzishwaji wa kongani ya viwanda Maranje.
“Kongani ya viwanda Maranje inajengwa katika eneo lenye ukubwa wa ekari 1,572 lililopo Kijiji cha Maranje, Kata ya Mtiniko, Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara. Serikali tayari imewafidia wakazi wote waliokuwa katika maeneo hayo.
“Katika hatua ya kwanza, Serikali imeanza uendekezaji wa eneo la ekari 354. Uendelezaji huo unahusisha ujenzi wa miundombinu wezeshi katika eneo hilo,” amesema Alfred.
“Miundombinu hiyo ni ujenzi wa barabara, kuweka miundombinu ya maji, ujenzi wa fensi na maghala mawili ya kuanzia. Hadi sasa, tayari umeme umeshapelekwa site, uchimbaji wa kisima umefanyika na mkandarasi wa kujenga ghala tayari amepatikana.”
Amebainisha kongani hiyo ya viwanda itawezesha ubanguaji wa korosho zote zinazozalishwa nchini ifikapo mwaka 2030, lengo ni kuzalisha tani milioni moja.
Pia, amesema katika kongani ya viwanda vitajengwa viwanda vya kuzalisha bidhaa zingine zitokanazo na korosho ikiwa ni pamoja na mafuta ya ganda la korosho, ethanol, sharubati na mvinyo.
“Kongani hiyo ikikamilika itakuwa na viwanda zaidi ya 30 na kuzalisha ajira zisizopungua 35,000. Serikali tayari imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu wezeshi katika eneo hilo,” amesema Alfred.
Awali, Dk Nchimbi akisalimia wananchi wa Kata ya Mpapura, Mtwara Vijijini akiwa njiani kuelekea Lindi, ameielekeza Serikali kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati, kwa bei nafuu pamoja na masoko ya mazao ya wakulima yanapatikana.
Ameipongeza Serikali kwa jitihada inayofanya kuhakikisha wananchi wanapata pembejeo za kilimo ili kuongeza uzalishaji wao. Hata hivyo, amesisitiza pembejeo hizo zitolewe kwa wakati na kwa bei nafuu.
“Serikali ihakikishe pembejeo zinapatikana kwa wakati, kwa bei nafuu na pia ihakikishe masoko ya mazao ya wakulima yanapatikana,” amesema Dk Nchimbi.
Kuhusu Bandari ya Mtwara, katibu mkuu huyo ameeleza kufurahishwa na uboreshaji uliofanyika kwa uwekezaji wa Sh150 bilioni, jambo litakaloongeza mapato ya bandari hiyo kwa Sh23 bilioni.
“Serikali iendelee kufanya uwekezaji kwenye bandari hii, ili kupunguza mzigo kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Tumeona ufanisi wa bandari hii ulivyopunguza mzigo,” amesema Dk Nchimbi.