Human Rights Watch imeutaka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuunda tume ya pamona ya kulinda raia nchini Sudan, wakati ambapo vita vya zaidi ya miezi 15 kati ya jeshi la kundi la RSF havionyeshi dalili za kukoma.
Katika ripoti mpya yenye kichwa cha ‘Khartoum Siyo Salama kwa Wanawake,’ shirika hilo la kuteteta haki za binadamu limerikodi ushuhuda wa wafanyakazi 42 wa afya na watoa huduma ya kwanza kuhusu vurugu za kingono na ndoa za kulazimisha na za watoto, tangu kuzuka kwa vita Aprili 2023, kati ya Jeshi la Sudan na kundi la Rapid Support Forces, RSF.
Soma pia: Marekani yaandaa mazungumzo ya kusitisha mapigano Sudan
Kati ya Aprili na Februari 2024, taasisi 18 huduma za afya ziliwatibu manusura 262 wa vurugu za kingono katika mkoa mkubwa wa Khartoum, ambao unajumlisha mji wa Omdruman ulioko mkabala wa Mto Nile.
Hata hivyo kulingana na watoa huduma ya kwanza, idadi ya visa vilivyoripotiwa ni sehemu ndogoi tu ya idadi halisi, huku manusura wengi zaidi wakikosa au kutokuwa tayari kutafuta huduma ya dharura.
RSF wamebaka, kubaka kimakundi na kuwalaazimish wanawake na wasichana wasiohesabika katika maeneo ya makaazi ya mji mkuu wa Sudan kuolewa, alisema Laetitia Bader, naibu mkurugenzi wa Human Rights Watch barani Afrika, na kuongeza kuwa kundi hilo limewaogofya wanawake na wasichana, na kwamba pande zote mbili zimekuwa zikiwazuwia waathirika kupata huduma za msaada, hali inayozidisha madhila wanayokabiliana nayo, na kuwafnaya wahisi kwamba hakuna mahala salama.
Tuhuma hizi za ubakaji zimetolewa pia na shirika la msaada la Madaktari wasio na Mipaka, MSF, ambalo katika ripoti yake ya tarehe 22 mwezi huu wa Julai lilizishtumu pande mbili zinazopigana kutothamini maisha ya binadamu na kutoheshimu sheria ya kimataifa.
Matukio ya ubakaji hayaripotiwi ipasavyo
Mkurugenzi Mkuu wa MSF Uholazi Vickie Hawkins, alisema matukio ya ubakaji na vurugu za kijinsia haviripotiwi ipasavyo kwa hofu ya waathirika kulipiziwa kisasi.
“Vurugu za kingono na kijinsia zimeenea pakubwa, lakini zinaripoti kidogo sana kutokana na hofu ya unyanyapaa, kunyamaza kwa hofu ya kulipiziwa kisasi na ukosefu wa huduma na nafasi za faragha. Data kutoka vituo vya MSF vinavyowasaidia wakimbizi wa Sudan nchini Chad zinaonyesha matumizi makubwa ya dhulma za kingono kama kipengee cha mzozo, hasa zikiwalenga wanawake na wasichana.”
Ripoti ya Human Rights Watch yenye kurasa 88 pia inaainisha mazingira ambayo yanaweza kuhesabiwa kama utumwa wa kingono. Ingawa vurugu za kingono zimetambuliwa hasa kama silaha inyotumiwa na RSF, kumekuwaa na ripoti za vurugu za kingono zinazofanywa na wanajeshi wa serikali.
Soma pia: Daglo akaribisha mazungumzo ya kusitisha mapigano Sudan
Human Rights Watch inasema kumekuwa na ongezeko la visa vilivyoripotiwa tangu jeshi lilipotwaa udhibiti wa mji wa Omdurman mapemwa mwaka 2024.
Kote nchini Sudan, manusura wameripoti majeraha mabaya ya kimwili kutokana na mashambulizi ya kingono, yakiwemo wanayofanyiwa na wapiganaji kadhaa mara moja. Miongoni mwa waliotibiwa na wahudumu wa afya ambao Human Rights Watch ilizungumza nao, wanawake wasiopungua wanne walifariki kutokana na majera yao.