Dar es Salaam. Washiriki wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika wametakiwa kuwasilisha miswada yao kwa ajili ya shindano la mwaka 2024, huku waandishi wanawake wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki.
Uwasilishwaji wa miswada unaanza kesho Julai 30, 2024 ambapo waandishi kutoka Afrika Mashariki na duniani kote wanaoandika kwa Kiswahili wanahimizwa kuwasilisha miswada yao na kushiriki katika shindano hilo.
Shindano hilo linatarajiwa kufanyika Julai, 2025 na washiriki wametakiwa kupeleka miswada ambayo haijachapishwa kwa njia yoyote katika tanzu ya riwaya, ushairi, mkusanyiko wa hadithi fupi, tamthilia, wasifu na riwaya za picha.
Katika ugawaji wa zawadi wa shindano hilo, mshindi wa kwanza atapata Dola 5,000 za Marekani, mshindi wa pili na wengine watapata Dola 2,500 za Marekani kila mmoja.
Uwasilishwaji wa miswada hiyo umekuja ikiwa imepita siku 22 tangu kufanyika kwa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili ambayo yanafanyika Julai 7 ya kila mwaka, huku Julai 27, 2024 kulikuwa na maadhimisho ya miaka 10 ya Watetezi wa Kiswahili Tanzania (Wakita) yaliyofanyika katika ukumbi wa Nkurumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Julai 29, 2024 na mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya tuzo hizo, Abdilatif Abdalla amesema tangu ianzishwe imekuwa ikiwasaidia waandishi wanaoshiriki, maandishi yao kuchapishwa vitabu kwa kushirikiana na kampuni ya uchapishaji vitabu ya Mkuki na Nyota na zaidi ya miswada 24 iliyoshinda imeshachapishwa vitabu.
“Ni jambo la kutia moyo kuona kila mwaka idadi ya washiriki kutoka nchi za Afrika na pia kutoka diaspora, inaongezeka,” amesema Abdilatif.
Amesema mwaka jana, jumla ya miswada iliyoshindanishwa ilikuwa 259 ambao ni ushahidi mmojawapo wa kuthibitisha jinsi Kiswahili kinavyozidi kuenea na kupata umaarufu duniani.
Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika ilianzishwa mwaka 2014 na Dk Lizzy Attree na Dk Mukoma wa Ngugi, ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe, na pia kutafsiri maandishi muhimu ya lugha nyingine kwa lugha za Kiafrika.
Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa ALAF Tanzania, Hawa Bayumi amesema wamejikita katika shughuli za kijamii katika nyanja nne ambazo ni afya, elimu, mazingira na makazi, hivyo tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika ipo chini ya nguzo ya elimu.
“Tunajivunia kuendelea kuiunga mkono tuzo hii yenye lengo la kukuza Fasihi ya Kiswahili na lugha za Kiafrika kwa jumla. Kiswahili ni lugha mojawapo inayokua kwa kasi zaidi duniani na inatumika katika nchi kadhaa za Afrika,” amesema Bayumi.
Amesema wanatambua umuhimu wa lugha kama zana muhimu ya maendeleo ya kitamaduni, kijamii na kiuchumi, hivyo wataendelea kukuza ukuaji wa Fasihi ya Kiswahili kupitia tuzo hiyo.