None selected
Picha Mkuu wa wilaya ya Tunduru ambaye pia Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Simon Chacha,akizungumza na wataalam wa idara ya kilimo na ushirika wa wilaya hiyo(hawapo pichani) kwenye moja ya kikao kazi kilichofanyika ofisini kwake mjini Tunduru,katikati ni Afisa umwagiliaji kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji mkoa wa Ruvuma Mhandisi Lusia Chaula na kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Chiza Marando.
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
WANANCHI na viongozi wa vijiji wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,wameonywa kutouza ardhi kwa wageni ili kupata fedha za haraka,badala yake wahakikishe wanaitunza na kuitumia kwenye shughuli za kilimo na ufugaji ili kujiletea maendeleo.
Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa wilaya hiyo Simon Chacha,wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Nambarapi kata ya Masonya wilayani humo.
Chacha alisema,hivi sasa kumeanza tabia kwa wananchi na hata viongozi wa vijiji kuuza ardhi kwa watu wanaotoka mikoa mbalimbali hapa nchini bila kutambua kuwa huo ndiyo urithi wa watoto wao na vizazi vyao.
Ameonya,kama wananchi wataendelea na tabia hiyo kuna hatari kubwa miaka ijayo kuwa watumwa kwa kukosa maeneo kwa ajili ya kufanya shughuli zao za uzalishaji mali na kwenda kulalamika kwa viongozi ilihali walikuwa na maeneo mengi.
“mara kwa mara nitakuwa mkali sana juu ya suala la kuuza ardhi holela katika wilaya yetu,kumekuwa na tabia isiyopendeza baadhi ya wananchi kwa kushirikiana na viongozi waliopo wa vijiji kuuza maeneo kwa wageni wanaonunua ardhi kwa bei ndogo,jambo hili sitolivumilia na nitakuwa mkali kweli”alisema Chacha.
“kuweni na huruma mtawaachia nini watoto wenu,ardhi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo yenu,msikubali kuuza kwa wageni kwani kwa kawaida ardhi uwa haiongezeki bali watu ndiyo wanaoongezeka nawaomba sana muwe na uzalendo na wilaya yenu”alisisitiza Chacha.
Mkuu wa wilaya alisema,wilaya ya Tunduru inapakana na nchi jirani ya Msumbiji,hivyo wananchi wanatakiwa kuwa makini kwa kutouza ardhi kwa mtu asiyekuwa raia wa Tanzania kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kwa mujibu wa Chacha,sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999,inatakaza mtu asiye raia wa Tanzania kumilikishwa ardhi kama siyo mwekezaji na mtu yoyote aliyeingia hapa nchini kwa njia isiyo stahili hata kama amekuwepo katika eneo hilo kwa muda mrefu hatomilikishwa ardhi.
Afisa Mahusiano na uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa(TANAPA)kanda ya kusini kituo cha Kalulu Stephen Mpondo alisema,Tanapa kwa kushirikiana na shirika lisilo la Kiserikali la FZS limefanya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vinane na kutoa hati miliki za kimila 2,723.
Alisema,lengo la mpango huo ni kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wanaotoka hifadhini na kwenda kwenye makazi ya binadamu na mashamba.
Aidha alisema,kwa kushirikiana na shirika la GIZ imetoa elimu ya namna ya kutengeneza dawa ya uzio ya harufu na kufungwa kwenye mashamba na mapito ya tembo katika vijiji vinne vilivyopo katika wilaya hiyo.
Mpondo alisema,uzio huo umeonyesha mafanikio chanya kwenye baadhi ya vijiji ambapo baada ya kufungwa kwenye maeneo ambayo yalikuwa mapito ya tembo,wanyama hao wamebadilisha njia na wananchi wamepata nafasi ya kufanya shughuli zao hasa za kilimo.
Mkuu wa idara ya ardhi maliasili na mazingira wa wilaya hiyo Dunia Almasi,amewataka kuepuka kuuza ardhi kwa bei ndogo kwani hiyo ndiyo rasilimali muhimu,kwani watashindwa kufanya shughuli za kiuchumi na kama wanataka kuuza waende ofisi za Halmashauri ili wafanyiwe tathimini.
Diwani wa kata ya Masonya Said Bwanali,amewaomba wananchi wa kata hiyo kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan,aliyejitolea kuwasaidia wananchi wa Tunduru ambao kwa muda mrefu walibaki nyuma kimaendeleo.