Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uimara na uendelevu wa Muungano uko mikononi mwa vijana.
Kutokana na hilo, amesema: “Ninawasihi sana vijana wote wa Tanzania muwe walinzi wa Muungano wetu. Kumbukeni kuwa Muungano huu ni urithi na tunu ya Taifa letu, na ni tunu ya Afrika kwa ujumla.”
Samia amesema hayo jana alipohutubia Taifa katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amesema matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonyesha idadi kubwa ya Watanzania ni vijana. Tanzania ina watu milioni 61.741.
Mbali ya hilo, amewasihi wanasiasa kukumbuka kwamba, Muungano ni wa watu. “Nitoe rai kuwa siasa zetu zijikite kwenye kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano, na tudhamirie kufanya siasa zenye kuleta maendeleo, kuwaunganisha watu, kuthaminiana, na kudumisha misingi ya utawala wa sheria.
Akizungumzia baadhi ya matunda ya Muungano amesema umewaimarisha zaidi Watanzania kama Taifa.
“Muungano wa Taifa letu unahitajika leo, kama ambavyo tuliuhitaji mwaka 1964. Hivyo basi, hatuna budi kuulinda Muungano huu kwa manufaa ya Watanzania wa kizazi cha sasa na wa vizazi vijavyo,” amesema.
Kuhusu wananchi, Rais Samia amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni moja tu duniani na ndiyo inayozaa Watanzania. “Jamhuri hiyo ni yetu na Tanzania ndiyo kwetu hatuna kwingine katu, abadan. Ninawasihi kudumisha uzalendo kwa kuzidisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Tukifanya hivyo, tutaweza kuurithisha Muungano huu kwa vizazi vyetu, ukiwa imara zaidi,” amesema.
Amesema ili kujenga Muungano ulio imara zaidi, Serikali imekuja na falsafa ya maridhiano, kustahimiliana, kuweza kubadilika, na kwa pamoja kujenge upya Taifa (maarufu kama R4).
“Kupitia falsafa hiyo, tumefanya mapitio ya mfumo wa haki jinai, kuhakikisha uhuru wa kujieleza, na vyama vya siasa kufanya shughuli zao kwa uhuru,” amesema.
Rais Samia amesema kupitia mazungumzo na ushirikishwaji, wamefanya mabadiliko kwenye sheria za uchaguzi, sheria ya vyama vya siasa na sheria ya Tume ya Uchaguzi.
“Katika diplomasia, Muungano umeiwezesha Tanzania kuwa na ushawishi mkubwa zaidi kikanda na kimataifa. Tumeweza kunufaika na kukuza uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi yetu na nyingine, na nchi yetu na taasisi za kimataifa kwa manufaa ya pande zote za Muungano,” amesema.
Amesema kupitia mwelekeo wa sasa wa diplomasia ya uchumi, Taifa limevutia mitaji, uwekezaji, teknolojia na kupata soko la bidhaa na huduma.
Rais Samia amesema jitihada zilizofanywa ndani ya miaka 60 ya Muungano zimesaidia kukuza Pato la Taifa kufikia Sh170.3 trilioni kwa takwimu za mwaka 2022, na pato la mtu mmoja mmoja kufikia wastani wa Sh2.8 milioni kwa mwaka 2022.
“Nafarijika kwamba, kwa sasa nchi yetu imefikia uchumi wa kati, katika ngazi ya chini, na jitihada zetu zote sasa ni kufikia uchumi wa kati, ngazi ya juu,” amesema.
Rais Samia amesema Serikali zote mbili zimeendelea kuibua na kutekeleza programu na miradi inayolenga kupunguza umasikini wa kipato na kuinua ubora wa maisha na ustawi wa jamii kwa pande zote mbili za Muungano. Miongoni mwa hizo alisema ni Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), uliotekelezwa kwa awamu 3. “Tathmini inaonyesha uwezo wa kaya kumudu gharama za mahitaji ya msingi umeongezeka, vilevile matumizi ya pembejeo yameongezeka na hivyo kuongeza tija kwenye kilimo, matumizi ya huduma za afya pia yameongezeka, na mahudhurio shuleni kwa watoto nao umeongezeka,” amesema.
Amesema umoja wowote hauachi kuwa na changamoto. “Kumekuwa na changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii ambazo zilihitaji kutafutiwa ufumbuzi. Serikali zetu mbili zimeweka mwongozo rasmi wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano, mambo mengi yametafutiwa ufumbuzi,” amesema.
Rais Samia amesema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya pamoja mwaka 2006, kumekuwa na mwenendo mzuri wa utatuzi wa changamoto zinazoibuka, na majadiliano ya Kamati hiyo yameimarisha zaidi Muungano.
Rais Samia amesema katika kipindi cha miaka 60 nchi imeendelea kuimarisha mawasiliano kupitia vyombo vya habari, simu za mkononi na mitandao ya kijamii.
“Wakati tunaungana njia kuu za mawasiliano za haraka tulizokuwa tukitegemea ni simu za mezani na zilikuwa katika familia chache. Leo hii kupitia Muungano wetu tumeweza kuimarisha mawasiliano, na hadi sasa takriban kila familia ina mtu mwenye simu ya mkononi na watoa huduma za simu wameongezeka,” amesema.
Amesema kwa sasa inakadiriwa jumla ya laini za simu zinazotumika ni zaidi ya milioni 72 na watoa huduma wameongezeka hadi watano ambao wameshaanza kutoa huduma zenye kasi ya 5G.
“Zaidi ya kutumia laini hizo kwa mawasiliano, vilevile kiasi cha laini milioni 53 zimesajiliwa kutumia huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, hivyo kuwarahisishia Watanzania kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii,” amesema.
Amesema maendeleo hayo yamechangiwa na uamuzi wa Serikali kuanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wenye jukumu la kuimarisha miundombinu ya mawasiliano vijijini.