WALIMU WAONYWA KUELEKEZA FEDHA ZA MIKOPO KWENYE ANASA

Na Pamela Mollel,Michuzi

Walimu wanaochukua mikopo kwenye taasisi mbali mbali za kifedha wametakiwa kuelekeza fedha hizo kwenye shughuli za uwekezaji na zinazozalisha ili ziwasaidie kulipika kuliko kuzitumia kwenye matumizi ya anasa.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Zainabu Makwinya wakati akifungua kongamano la siku ya walimu maarufu kama ‘Mwalimu Spesho’ iliyoandaliwa na Benki ya NMB ambayo imehudhuriwa na zaidi ya wataalamu 250 wa Elimu.

Zainabu amesema kuwa fedha za mikopo zimekuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya watumishi wakiwemo Walimu, lakini pia wako wanaopata mateso makubwa na fedha hizo kutokana na kutokuwa na matumizi mazuri hasa za kiuzalishaji.

“Niwaambie watumishi wenzangu, usikimbilie kuchukua mkopo na kufanyia starehe au ukiwa bado hujapanga unataka kufanyie nini na manufaa yake ni yapi, kwa sababu kwa kufanya hivyo utapata shida na mateso makubwa hadi kukimbia hata kituo cha kazi wakati wengine wakineemeka na mikopo hiyo” amesema Zainabu.

Alitumia nafasi hiyo kuipongeza Benki na NMB kwa kuwa wabunifu wa bidhaa mbalimbali zinazolenga makundi yote ya watumishi sambamba na mikopo ambayo imekuwa msaada mkubwa katika maandalizi na mahitaji ya kimaisha ya sasa na baadae hata watakapostaafu.

“Hakika mnafanya kazi nzuri ya kuisaidia serikali kutoa Elimu ya kifedha lakini pia elimu ya matumizi sahihi kwa manufaa ya watumishi ambao kwa waliotumia vema wamekuwa na maisha mazuri na bora hali iliyoleta hata utulivu kazini” Amesema Zainabu.

Awali Akizungumza katika Kongamano hilo, Meneja Mwandamizi kitengo cha wateja Binafsi kutoka Benki ya NMB, Queen Kinyamagoha amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kukutana na walimu kujua bidhaa zilizopo kwa ajili yao lakini pia matumizi sahihi ya mfumo wa Kiserikali wa kujihudumia (ESS).

“Mbali na hilo pia tumekuja kuwapa elimu ya kifedha, Bima na ujasiriamali lengo ikiwa ni kupata masuluhisho mbali mbali ya kifedha na pia wapate usalama wa fedha zao kwa ustawi wao binafsi na familia kwa ujumla” amesema Queen.

Amesema katika kongamano hilo wameshirikisha zaidi ya wataalamu 250 wa Elimu kutoka Wilaya ya Arumeru wakiwemo maafisa Elimu, wakuu wa shule na walimu wa kawaida ambao pia watapata fursa ya kuzisema changamoto zao wa kifedha na benki kwa ujumla na kuona namna ya kuziboresha.

Washiriki katika semina hiyo, Afisa Elimu kutoka kitengo cha Elimu maalum halmashauri ya Wilaya ya Meru, Moris Missanga amesema kuwa changamoto nyingi za kifedha kwa sasa zimetatuliwa na taasisi hiyo ya kifedha huku akiwaomba kufikia hadi shule za pembezoni.

“Kiukweli NMB ambayo ndio tunatumia kama benki yetu ya mishahara kwa sasa wana maboresho makubwa sana hasa masuluhisho ya kifedha, kikubwa tunawaomba waongeze nguvu kufikia walimu wanaofanya kazi katika shule za vijijini ili nao wawe wananufaika na huduma zao hasa za ATM mashine” amesema.

Nae Mwalimu Flora Temba kutoka shule ya Akeri, amesema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo kwa sasa ni utapeli wa mitandaoni ambao baadhi ya walimu wasioitambua huduma ya ‘NMB Mkononi’ wamekuwa wakitapeliwa fedha zao na watu wanaojifanya maofisa wa benki hiyo.

“Tunaomba Uongozi wa Benki ione namna ya kulinda fedha za baadhi ya wateja wao ambao bado hawajajua vema matumizi ya mitandao, au wanaokuja maofisini kwao wawe na baadhi ya maswali ya kuuliza wanaotoa fedha ili kujiridhisha kweli ndio muhusika wenye akaunti husika” amesema Flora.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Meru Zainab Makwinya akizungumza kwenye kongamano la Mwalimu Specho

Meneja Mwandamizi kitengo cha wateja Binafsi kutoka Benki ya NMB, Queen Kinyamago akizungumza kwenye kongamano la Mwalimu Specho

 

Related Posts