Kinachosababisha vuta nikuvute kati ya wazazi na watoto

Kila mtoto anapozaliwa anakuwa na kipaji alichopewa na Mungu.

Kimakuzi, vipaji hivyo huanza kuonekana mtoto akiwa mdogo na ndio maana wataalamu wanapendekeza wazazi kuanza kuchunguza vipaji vya watoto katika umri huo.

Ukifuatilia historia za baadhi ya watu maarufu duniani, utagundua kuwa wengi walionyesha mwelekeo wa hicho wanachokifanya sasa tangu wakiwa na umri chini ya miaka 10, huku wazazi wao wakichukua nafasi kubwa ya kulea vipaji vyao.

Utafiti wa mwaka 2013 uliofanywa nchini Finland uligundua kuwa vipaji vya kuzaliwa vina nguvu zaidi kuliko vile vya kujifunzia ukubwani.

Hata hivyo kwa Tanzania, uzoefu unaonyesha wazazi wengi hujiweka kando katika mchakato mzima wa kubaini vipawa vya watoto wao achilia mbali kuviendeleza.

Tatizo zaidi linakuja mtoto anapofika ukubwani na kujikuta akitakiwa kusoma au kufanya kile anachokiamini mzazi, pengine kutokana na mafanikio aliyoyapatia mzazi huyo.

Baadhi ya watu waliopitia masaibu ya vuta nikuvute kati yao na wazazi kipindi cha masomo yao, wanaelezea safari yao ya kimasomo, hasa walipotakiwa kusoma fani ambazo ilibidi wazisomee kwa ushawishi wa wazazi, lakini sio kwa mapenzi yao.

Jovin Robert, mkazi wa Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam, ni mmoja wa waathirika wa janga hilo. Anaelezea mkasa wake baada ya kumaliza kidato cha tano, baba yake alimtaka akasomee udaktari.

“Wakati baba ananiambia nisomee udaktari na mimi nilimshirikisha kile ambacho nilikuwa nakitamani siku zote kuwa, yaani kuwa mhandisi,” anaeleza.

Robert anazidi kufafanua, baada ya kumwambia baba kuhusu hilo hakufurahishwa nalo, alizidi kukazia suala la kusomea kile alichokitaka.

“Nilijitahidi kumsisitiza kuhusu suala langu la kusomea uhandisi, lakini baba hakuwahi kukubadiliana na mimi, mwisho alikataa kunilipia ada ya kusomea kile nilichotamani,” anasema na kuongeza:

“Baada ya ndoto zangu kufifia, ndipo nilipoanza safari nyingine ya kusaka mtaji ili kujikwamua kimaisha’’.

Anasema safari yake ya kujikwamua kimaisha ilianzia Kariakoo kama mtunza stoo kwa muda wa miaka miwili na ndipo alipopata mtaji na kufungua duka la vifaa vya simu ambalo ndilo analitegemea kuilisha familia na kusomesha mtoto wake kwa sasa.

“Nilianza kazi kwa mshahara wa Sh100,000 kwa mwezi, huku chakula kikiwa ni juu ya mwajiri wangu. Nilijituma baada ya miaka miwili niliamua kufungua duka dogo la vifaa vya simu,” anaeleza namna alivyolazimika kupoteza ndoto yake ya kuwa mhandisi kwa msukumo kutoka kwa mzazi.

Naye, Joyce John anatoa ushuhuda baada ya kukumbana na masaibu ya mzazi wake mmoja kushinikiza asomee kile asichokitaka.

“Kipindi nimemaliza kidato cha sita ndoto yangu ilikuwa kusomea biashara au uandishi wa habari, ila hali ilikuwa tofauti kwa baba yangu, yeye alitamani nisomee ualimu au mambo ya kodi, kitu ambacho kilikuwa tofauti kwangu.

‘’Niliwasilisha matamanio yangu kwa wazazi, japo baba hakuwa tayari kwa hilo, ila mama alitamani nifikie ndoto zangu kwa kusoma kile nilichokitamani siku zote, msimamo wa baba ulibaki vilevile.

Anaendelea: “Niliomba nafasi ya masomo kwa fani alizotaka mzazi, lakini pia sikusahau kozi ya ndoto zangu.”

Joyce, ambaye kwa kipindi hicho alikuwa binti wa miaka 20, anasema matokeo yalipotoka alichaguliwa vyuo vitatu ambavyo ni Chuo cha Kodi, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na chuo kimoja cha uandishi wa habari.

Anasema baada ya kuchaguliwa katika vyuo hivyo bila kumshirikisha yeyote, aliamua kwenda chuo cha masuala ya habari.

Safari ya kupambania ndoto zake ikaendelea pale alipowashirikisha wazazi kuhusu ada ya masomo yake ya chuo, lakini baba alisimamia msimamo uleule.

‘Sikuwa nataka kusomea kitu nisichokipenda, hivyo nilizidi kusisitiza nini nakihitaji maishani, mwisho baba alihitimisha kwa kusema hatanilipia ada ikiwa sitasomea alichokitaka,’’ anasema.

Anasema hakubadili mawazo yake ya kusomea kile anachokitaka mpaka pale mama yake alipobeba jukumu la kuanza kumsomesha.

“Mama alinipambania mpaka nilipomaliza elimu yangu bila baba kushiriki kwa chochote,’’ anasema.

Kuna mitazamo tofauti kwa wazazi. Wapo wanaosema kumpangia mtoto cha kusoma ni kufifisha ndoto na kipaji chake. Lakini wapo wanaooana bado mzazi kwa uzoefu wa kimaisha ana nafasi ya kumshauri na ikiwezekana kumshurutisha mtoto kusomea fani ambayo mzazi anaamini itamsaidia mwanawe.

Abby Kwesa anaamini kuwa mtoto kwa mzazi hakui na kama mzazi, ana nafasi kubwa ya kumuonyesha ukweli wa maisha ambao mtoto anaweza asiuone.

“Chukulia mzazi aliyefanikiwa kwenye udaktari au biashara fulani, na kama mzazi mwenye uchungu lazima atataka mwanawe apite mapito yake kwa kuwa ana uchungu naye,” anasema na kuongeza:

“Sasa kweli nimkubalie mwanangu anayekuja na mawazo ya kusoma vitu ambavyo mimi kwa uzoefu wa kimaisha naviona sawa na kupoteza muda tu? Hapana! Kama mzazi makini siwezi kukubali. Sawa nitamsikiliza lakini anieleze fani au jambo makini, sio kufuata mkumbo. Kuna fani ni shida tu kusomea.’’

John Elias, mkazi wa Manyara, anamshangaa mwanawe anayenga’ng’ania uchezaji mpira ambao hauna tija kwake, licha ya kumshauri sana aendelee na masomo. Kama mzazi alitamani mwanawe afike mbali kimaisha kupita elimu, hasa akizingatia historia aliyopitia.

‘’Mimi nilihimizwa sana kusoma na wazazi wangu na ninaifahamu faida ya elimu, ndiyo maana natamani sana mtoto asome na pengine anizidi mimi baba yake,’’ anasema.

Anasema mtoto wake alionyesha kipaji cha mpira na baada ya kumaliza kidato cha nne, alimpeleka shule ya mpira huku akiendelea kusubiri matokeo yake.

Anasema baada ya matokeo kutoka, alifaulu kwenda kidato cha tano fani ya CBG, lakini mtoto huyo hakuonesha utayari wa kuendelea na masomo, licha ya wazazi kuanza kufanya maandalizi ya kuendelea na masomo.

“Mimi kama mzazi wake sikubahatika kupata nafasi aliyoipata yeye. Nilijisomesha mwenyewe mpaka hapa nilipofika lakini yeye anaichezea nafasi hii. Kwa sasa hajui ni kipi hasa anakitamani katika maisha yake na inaniumiza kama mzazi. Nimejaribu kumshauri japo anatamani vingine, lakini asome pia, yeye kashikilia msimamo wa kucheza mpira tu,’’ anaeleza.

Kwa upande wake, mzazi Sarah Onesmo anasema ni vyema mtoto akajichagulia cha kusoma, kwa kuwa yeye ndiye mhusika na anajua anachotamani maishani.

Mzazi huyo mwenye shahada ya sheria anaeleza kuwa yeye alichaguliwa masomo na baba yake, jambo analosema hataki kulirudia kwa mtoto wake.

“Sitamani nimpitishe mtoto wangu kule nilikopitishwa mimi, maana licha ya kuwa na elimu hii, sijawahi kutafuta kazi kupitia cheti changu, nilisoma kuridhisha wazazi wangu,’’ anasema.

Anaongeza: “Kuna wakati naona nilipoteza muda kusoma nilichokisomea, maana hakijawahi kunisaidia maishani. Mwisho kabisa nawalaumu wazazi”.

Anaeleza kuwa kwa dunia inakoelekea ambapo ajira zimekuwa ngumu, ni busara mtoto akachagua mwenyewe ili siku akikumbwa na kadhia ya kukosa ajira, asitafute mtu wa kumtupia lawama.

Mkufunzi wa maisha na ushauri, Fiona Nkya anasema kwa kuwa watoto wanatofautiana kujitambua, mzazi asimchagulie cha kusoma, bali kumsikiliza na kumuunga mkono kile anachotamani alimradi kiwe na faida.

“Kama mzazi unaamua kumchagulia mtoto, mchagulie kitu kitakachompa ajira na pengine kujiajiri mwenyewe,” anasema na kutaja madhara ya mzazi kumchagulia fani mtoto, ikiwamo mtoto kutozingatia anachosoma kwa sababu alisukumwa na utashi wa mzazi.

Madhara mengine anataja kuwa ni mtoto kujenga chuki kwa wazazi na hata kumwathiri afya ya akili.

“Mtoto akijichagulia fani ya kusoma, anasoma kwa kuzingatia sana, na kutokana na imani iliyopo ndani yake, hilo linamfanya afike mbali,’’ anaeleza.

Related Posts