PARIS, UFARANSA: WIKI kadhaa zilizopita, kulikuwa na stori ya Kylian Mbappe kutaka kuishtaki Paris Saint-Germain (PSG) kwa kutomlipa baadhi ya mishahara yake ambapo mama yake alithibitisha.
Timu ya wanasheria wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa iko tayari kuwasilisha kesi mahakamani dhidi ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1), kwa kudai kwamba mishahara ya miezi miwili hakulipwa.
Inaelezwa kwamba Mbappe alitakiwa kupata kiasi cha Euro 80 milioni ndani ya miezi miwili kama mshahara, lakini PSG haikufanya hivyo.
Akizuungumza na tovuti ya La Parisien, mama mzazi wa Mbappe, Fyza Lamari alisema: “Bado suala linaendelea na sasa lipo mikononi mwa wanasheria wa Kylian. Lakini nina imani kwamba kila kitu kitakuwa sawa. Tumepokea barua ya majibu kutoka kwao (PSG), hatupo katika hali nzuri, lakini naamini haya yatapita.”
Mama huyo aliongeza kuwa, “nataka kukumbuka mambo mazuri ambayo tuliyapata (Mbappe) alipokuwa hapo (PSG).”
Vilevile mama huyo alisema ikiwa PSG haitalipa pesa hizo kuna uwezekano wakatinga mahakamani kuishtaki ili kupata haki yao.
“Ikiwa hatuna chaguo (jingine). Ndiyo, bila shaka tutaenda (mahakamani) ila kwa sasa nina matumaini makubwa kwamba mkataba tuliosaini (PSG) miaka miwili iliyopita utaheshimiwa.”
Mbappe na PSG, wamekuwa katika mikwaruzano na sintofahamu kwa muda mrefu na hiyo ilianza wakiwa pamoja na hata baada ya Mbappe kuondoka na kutua Real Madrid katika dirisha hili la usajili barani Ulaya. Haya ni baadhi ya matukio yaliyojiri katika kipindi ambacho wawili haoa wanaachana na sababu za kwanini Mbappe ameondoka PSG.
Wakati msimu uliopita unakwenda kuanza, Mbappe aliwasilisha barua katika ofisi ya meneja wa timu iliyokuwa ikiijulisha PSG kwamba hataongeza mkataba wa kusalia msimu ujao (ambao ndio huu) na badala yake ataondoka mwisho wa msimu.
PSG haikukubaliana na hilo. Ilipinga na katika harakati za kuhakikisha inamshawishi abaki ikajikuta inatumia nguvu na mwishowe Mbappe akaachwa na kikosi cha timu hiyo kilichosafiri kwenda Japan kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Inaelezwa PSG ilikuwa inaamini itapata hasara mara mbili kwa kukubali staa huyo aondoke katika dirisha hilo, kwa sababu kutokana na kukaa ndani ya timu kwa msimu uliopita ilibidi alipwe zaidi ya Pauni 70 milioni mbali ya mshahara.
Hiyo ilikuwa ni bonasi tu ya kwanza, alikaa nje ya timu kwa muda na baadaye aliachwa acheze ingawa alikosa mechi ya ufunguzi na mchezo mmoja wa Ligi Kuu.
Baada ya hapo vuguvugu liliendelea na ilielezwa kwamba PSG inapambana kumshawishi asiondoke, na akubali kusaini mkataba mpya.
Mwaka huu ulipoanza mambo ndio yalizidi kupamba moto. PSG ilimshtumu Mbappe kwamba tayari ameshafanya makubaliano na mabosi wa Real Madrid kabla ya mkataba kumalizika.
Hali hiyo ilisababisha wimbi la mgogoro baina ya staa huyo na mabosi wa PSG, na mara kadhaa lilisababisha awekwe nje ya uwanja.
Mambo yaliendelea hivyo hadi mwisho wa msimu uliopita ambapo aliwekwa nje katika mechi mbili za kufunga msimu na sababu ikiwa kwamba mabosi wa timu hiyo walidhani ameshasaini mkataba wa kuitumikia Real Madrid. Ilikuwa hivyo hadi pale msimu ulipomalizika.
Mbali ya yote, PSG ilikuwa ikijiapiza kwamba haiwezi kuruhusu mchezaji tegemeo katika timu kuondoka bure na ilitumia kila rasilimali ilizonazo kuhakikisha Mbappe anabaki, lakini ilishindikana.
Dirisha hili Mbappe amejiunga na Real Madrid, lakini inaelezwa PSG imegoma kumpa mshahara wa karibu miezi miwili mfululizo.
Kuanzia miaka ya 2010, Waarabu waliamua kuingia kwenye soko la dunia la mpira wa miguu. Walinunua timu nyingi ikiwemo Manchester City wakitumia pesa nyingi kuhakikisha timu hizo zinafanya vizuri.
Mojawapo kati ya timu hizo ni Paris Saint-Germain waliyoinunua 2011. Katika vipindi tofauti PSG imekuwa timu shindani ikisajili baadhi ya mastaa wakubwa kwenye soka.
ilifanikiwa kwa mtu kama Ronaldinho, David Beckham na wengineo. Waarabu wanaoimiliki timu hiyowanatoka Qatar lengo lao ni kuona majina makubwa yanachezea timu yao. Ndio maana walidiriki kumsajili Lionel Messi akiwa anakwenda ukingoni, Sergio Ramos, Kayle Navas na wote walionekana kama wameshamalizana na soka la ushindani na hawana njaa ya mafanikio. Lakini, Nasser Al Khelafi, bosi wa PSG na bodi yake waliidhinisha bajeti ya kuwasajili. Hata wakati wanamsajili Beckham tayari alikuwa anakwenda kwenye nyakati za mwisho za maisha yake ya soka. Wao hawakujali kikubwa zaidi ilikuwa ni kuona mchezaji mwenye jina kubwa kama yeye akikanyaga ardhi ya Parc de Princess akiwa na jezi yao.
Ndiyo maana hawakujali kutoa zaidi ya Euro 150 milioni kwa ajili ya kumsajili Neymar kutoka Barcelona 2017 kwa sababu walitaka kuona jina kubwa la mchezaji mkubwa kama yeye linaichezea timu hiyo.
Huo ndiyo ulevi wao. Wanahisi furaha mioyoni wakiona kuna kundi la wachezaji mastaa wanaotajwa duniani likiwa kwenye uwanja wa mazoezi wa Camp des Loges wakishikana na kutaniana. Hawajali sana kuhusu pesa wanazotumia. Waarabu hao wanainjoi matukio kama hayo.
Kwa muda sasa walikuwa wanamiliki mmoja kati ya wachezaji bora duniani, Kylian Mbappe. Kabla ya kusaini mkataba mpya ilibaki kidogo aondoke atue Real Madrid, lakini PSG ilimbakisha na kumpa pesa nyingi. Hapa ndipo kuna tofauti ya mitazamo, kwani Mbappe hakuwa na furaha ya kuendelea kuichezea PSG kwa sababu hakuwa anaamini kuwa atashinda mataji makubwa au ataonekana ni mchezaji bora duniani akiwa Paris. Ndoto na mawazo ya Mbappe vilikuwa jijini Madrid. Licha ya PSG kuwa na uwezo wa kumpa pesa nyingi zaidi ya zile ambazo Real Madrid imempa, lakini supastaa huyo haonekani kujali sana kuhusu hilo kwani kula wali na maharage kwenye amani ndiyo chaguo lake, kuliko pilau sehemu ambayo hana furaha.
Alipokuwa anasaini mkataba mpya 2022, PSG ilipambana kuhakikisha hilo linafanikiwa. Kuna wakati hadi serikali ya Ufaransa kupitia kwa rais Emmanuel Marcon iliingilia kati na staa huyo akaombwa aendelee kuichezea timu hiyo.
Msimu uliopita staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa amefunga mabao 44 kwenye mechi 48 za michuano yote akiwa ndiye mchezaji aliyetupia mara nyingi zaidi nyavuni licha misukosuko yote aliyokubana nayo klabuni hapo.
Ukiondoa ukweli kwamba mabosi wa PSG wanapenda majina makubwa kutokana na ufahari walionao, pia wamekuwa wakipata pesa nyingi kupitia majina hayo. Mastaa kama Lionel Messi waliipatia timu hiyo pesa nyingi kutoka kwenye mauzo ya jezi ndani ya muda mfupi. Pia kampuni nyingi zikatamani kutangaza na PSG ikiaminika watu wengi watakuwa wanaifuatilia kwa sababu ya kina Messi.
Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa Mbappe. Mbali ya kupoteza nyezo muhimu kwenye timu, lakini pia wamepoteza walau asilimia 10 ya pesa ambazo walikuwa wakizipata wakati staa huyo anaichezea timu yao.
Kuondoka kwa Mbappe pia kunakwenda kuathiri mamlaka za soka nchini Ufaransa kwa sababu Mbappe alikuwa ni taswira ya Ligue 1 na mpira wa Ufaransa. Kitendo cha kuondoka kwake kitaathiri pande nyingi kwenye soka nchini humo na kuna baadhi ya kampuni zilizokuwa zimewekeza ama kutamani kuwekeza kwa sababu ya uwepo wake zitaondoka au kusitisha matangazo.