Nabi: Yanga ni balaa!  Atoa angalizo Simba, Chivaviro asimulia

KOCHA wa Kaizer Chiefs, Nasredine Nabi ameliambia Mwanaspoti kuwa Yanga ina mabadiliko makubwa na chochote kinaweza kumkuta yoyote msimu ujao.

Nabi ambaye ni kocha wa zamani wa Yanga, amekiri kwa uchungu kwamba kilichoomuumiza zaidi kwenye mechi ya juzi ni ukubwa wa kipigo ilichopata timu yake; “lakini tulistahili.”

Yanga tayari ipo nchini na kombe lao la Toyota walilobeba nchini Afrika Kusini ilipoweka Kambi ya muda ya maandalizi ikiichapa Kaizer Chiefs mabao 4-0.

Nabi ambaye hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza kubwa ya kirafiki baada ya kutoka kambini Morocco,alisema hata hivyo Yanga imebadilika na kuwapa shida ya kupoteza mpira kwa haraka wakati wanaumiliki iliyowalazimu wachezaji wake wengi vijana kushindwa kuhimili presha hiyo.

Aliongeza kuwa kitu ambacho imekutana nacho timu yake kinaweza kuikumba timu yoyote ndani na nje ya Tanzania msimu ujao ambayo haijajiandaa sawasawa kukutana na mbinu za namna hiyo za timu inayoweka presha kubwa kwa wapinzani wanapokuwa na mpira.

“Timu yetu ina wachezaji wadogo kidogo ambao hawakuwa tayari kukutana na ugumu wa namna ile, ukiangalia unaona namna ambavyo Yanga ilipokuwa haina mpira iliweka presha kubwa kwetu na vijana kujikuta wanafanya makosa makubwa,”alisema Nabi ambaye ambaye ana uraia wa Tunisia.

“Kuna mabao ambayo mliyaona ni kama yalikuwa zawadi kwao,lakini nadhani tumejifunza nadhani kilichotokea kwetu kinaweza kuikuta timu yoyote ambayo haikujiandaa sawasawa kukutana na mbinu za namna ile,”alisisitiza Kocha ambaye alikiri kwamba bado ana muda wa kuisuka timu yake.

Mshambuliaji Ranga Chivaviro wa Kaizer Chiefs ambaye aliwahi kuwindwa na Yanga akachomoa dakika za mwisho, alisema Yanga iliwaweka kwenye wakati mgumu ambapo nidhamu yao wakati hawana mpira ni ilikuwa  kitu kigumu kwao kuweza kuhimili.

Chivaviro ambaye ana asili ya Zimbabwe, alisema walikutana na kipimo kigumu katika mchezo wa kwanza wa kirafiki tangu waanze maandalizi.

“Ilikuwa ngumu kwetu, ni kama hawakutupa nafasi ya kujipanga wakati tukiwa tuna mpira, walikuwa wanalazimisha haraka tuupoteze uwe chini yao nadhani ndio silaha waliyoitumia kutengeneza ushindi kama ule,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Marumo Gallants.

“Unajua huu ulikuwa mchezo wetu wa kwanza wa kirafiki wenzetu walionekana kuwa wepesi kuliko sisi ilitufanya kuonekana hatukuwa tayari kukutana na watu kama wao, nadhani tutabadilika kwa kuwa tupo chini ya makocha wapya ambao wanaaanza kutupa falsafa mpya.”

Ziara hiyo ya Yanga imekamilika kwa timu hiyo kuonyesha kiwango kizuri ambapo licha ya kucheza mechi tatu ikafunga mabao sita huku ikipoteza mchezo mmoja pekee.

Yanga ambayo ilianza kwa kupoteza dhidi ya Wajerumani FC Augsburg kwa mabao 2-1 kisha ikashinda mechi mbili zilizofuata kwa kuichapa TS Galaxy na juzi kuimaliza Kaizer kwa ushindi huo wa mabao 4-0.

Yanga imerejea nchini leo ambapo itaendelea kwa kambi fupi kuelekea kilele cha wiki ya Mwananchi tamasha ambalo watalitumia kutambulisha wachezaji wao.

Related Posts