UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kama tunataka kombe la Afrika tupunguze usela

NDOTO ya klabu za Simba na Yanga kwa sasa ni kuja kutwaa ubingwa wa Afrika. Safari hiyo siyo mbali sana wala karibu sana. Ni kama tumeshasogea pa kubwa na ni kama bado tuko mbali.

Baada ya Simba na Yanga kucheza karibu na wakubwa wote wa soka la Afrika, matokeo sio mabaya sana wala sio mazuri sana. Kuna mahali tumesogea. Kuna mahali bado tupo mbali sana.

Baada ya timu zetu walau kuwa na uhakika wa kucheza robo fainali kuna mahali tumesogea. Kuna mahali bado tupo nyuma kidogo. Mpira wetu bado una usela mwingi.

Mpira wetu bado una matukio mengi ya kihuni. Kama tunataka kombe la Afrika usela inabidi upungue. Kama tunataka kombe la Afrika inabidi weledi uchukue nafasi yake. Usajili wetu umejaa usela sana.

Usajili wa wachezaji ni mwendo wa kuviziana tu. Hakuna anayefuata taratibu kwa asilimia 100. Kuna mahali tu utaona kuna rafu zimechezwa. Wachezaji wengi hapa nyumbani wanashawishiwa na klabu nyingine kabla hata ya kupata ridhaa ya klabu zinaowamiliki.

Wachezaji wanavunja mikataba kiselasela. Klabu zinasajili wachezaji kiselasela. Hakuna dirisha la usajili  linalofungwa bila vituko vya usajili.

Kama Simba na Yanga wanataka ubingwa wa Afrika inabidi huku tutoke. Huwezi kutwaa lombe lolote Afrika kwa njia za kisela.

Kwa namna yoyote usajili wa Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoka Yanga kwenda Azam FC ulifanyika kisela. Hii sio njia halali itakayotupatia kombe la Afrika.

Usajili wa Prince Dube kutoka Azam FC kwenda Yanga umegubikwa na usela mtupu. Huku inabidi tutoke kabisa. Haya na mengine mengi yamefanyika sana siku za nyuma.

Ndiyo maana klabu zetu na wachezaji wetu wa zamani  wanajitapa sana kuwa na uwezo mkubwa, lakini hakuna kombe lolote la Afrika lililokuja nyumbani.

Usela mwingi bado upo kwenye usajili wa wachezaji wetu. Kama tunataka kombe lolote la Afrika tupunguze usela.

Siasa zetu za ndani zisivunje taratibu za usajili. Tunatengeneza wachezaji wengi ambao watatusumbua hapo baadaye.

Msimu huu tu peke yake Simba imelalamikiwa karibu na klabu tatu.

Bado hakuna uhakika wa moja kwa moja, lakini hii inaleta ukakasi.

Kwanini kila mchezaji inayemsajili ziibuke kelele kwenye klabu anayotoka? Maana yake tatizo ni ama lipo Simba au wamiliki wa mchezaji. Huu wote kwangu ni usela tu.

Kwa sababu taratibu za kuuza na kununua mchezaji zipo dunia  nzima sioni sababu ya hizi sarakasi kuendelea kuwepo. Haiwezekani kila mchezaji anahama kwa migogoro.

Haiwezekani msimu mmoja kuwe na klabu tatu zina mgogoro na Klabu moja juu ya kusaini wachezaji.

Unakumbuka usajili wa Clatous Chama kutoka Simba kwenda Yanga?

Kulikuwa na habari za chini kwa chini kuwa  inasemekana alisaini pia kabla mkataba wake na Simba kumalizika.

Inasemekana. Kwa hayo yote yanayoendelea  huwezi kushangaa.

Chama alitangazwa na Yanga siku moja tu baada ya mkataba wake na Simba kumalizika wakati mchezaji mwenyewe akidaiwa kuwa nchini Zambia.

Yaani siku moja tu baada ya mkataba wake na Simba kumalizika, siku hiyo alisaini Yanga. Siku hiyohiyo akafanya upigaji wa picha na siku hiyo hiyo kutangazwa?

Inawezekana lakini inafikirisha sana. Ndiyo mpira wetu ulivyo. Kivyetuvyetu. Kama tunataka kombe la Afrika haya masarakasi inabidi tuyapunguze.

Hatuwezi kuendelea na usajili wa kuviziana. Huku inabidi tuondoke.

Klabu zimefanya sana uhuni siku za nyuma na hazikushinda chochote Afrika. Wachezaji wamefanya sana uhuni hapo nyuma na hawakushinda chochote. Hatutakiwi kurudi huko tena.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inapaswa kuwa na kazi ndogo sana wakati wa usajili. Dunia imebadilika ni lazima tuwe na weledi mkubwa kwenye usajili.

Mambo ya kizamani yanatuchelewesha. Inabidi tutoke huko haraka sana. Tufungue milango ya biashara ya kuuza na kununua wachezaji wakiwa na mikataba. Tukiifanya biashara hii kuwa rasmi  itapunguza kelele za usajili.

Baada ya Feisal na Dube kufanya usela, naona dalili ni zilezile kwa Kibu Dennis kwa Simba. Ni mchezaji aliyesaini mkataba mpya hivi karibuni tu. Ni mchezaji aliyeongezwa thamani kubwa sana na Simba.

Hii dhambi mpya kwenye mpira wetu hivi karibuni ilivyoanzisha na Feisal na baadaye Dube imeanza kumea. Kila mchezaji siku hizi anaona anaweza kufanya chochote. Wachezaji wameanza kuwa masela. Wachezaji hawaheshimu tena mikataba.

Kama tunataka kombe la Afrika, huku ni lazima tutoke. Tupunguze sana kushambikia huu usela. Nakumbuka wakati Feisal analazimisha kuondoka Yanga, mashabiki wengi wa Simba walishadadia hili jambo. Mashabiki wengi wa Simba walisimama na Feisal.

Naona baada ya hili la Kibu na Simba, mashabiki wengi wa Yanga wako na Kibu. Ni mwendo wa kushabikia usela. Hii haisaidii mpira wetu. Inatuumiza kama nchi. Hawa wachezaji wanatakiwa kufuata taratibu. Huu ushabiki maandazi una gharama kubwa.

Kama tunataka kombe la Afrika inabidi tupunguze usela. Njia rahisi ya kulitatua hili ni kuajiri wataalamu kwenye maeneo mengi ya utendaji na uendelezaji wa mpira wetu. Kesi karibu zote kwa klabu zetu zikishtakiwa Fifa huwa hazitoboi. Mara nyingi tunakutwa na makosa.

Sababu ni nini? Mojawapo ni kukosa watu sahihi kwenye uendeshaji na usimamizi wa klabu. Tuache usela, haujawahi kutusaidia chochote tangu na tangu.

Related Posts