Waandamanaji wampinga Maduro, Venezuela | Mwananchi

Caracas. Kufuatia matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, maelfu ya wananchi wameyapinga na kuzua vurugu katika Jiji la Caracas.

Hasira za umma ziliongezeka baada ya Baraza la Taifa la Uchaguzi (CNE) Jumatatu kutangaza rasmi kuwa, Maduro alichaguliwa tena na wapiga kura wengi kuwa Rais kwa muhula mwingine wa miaka sita (2025-2031), akimpita mpinzani wake Edmundo Gonzalez.

CNE ilisisitiza kwamba, Gonzalez Edmundo alishindwa uchaguzi wa urais kwa kupata asilimia 44 ya kura ikilinganishwa na asilimia 51 za Maduro.

Hata hivyo, CNE, inayodhibitiwa na wafuasi wa Maduro, haijatoa matokeo kutoka kwenye vituo 30,000 vya kupigia kura nchini Venezuela, jambo linaloongeza mvutano wa kisiasa katika Taifa hilo la Amerika Kusini.

Katika mkutano na waandishi wa habari jioni ya Jumatatu Julai 29 2024, kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado alidai kuwa, muungano wake ulikuwa na zaidi ya asilimia 70 ya kura zilizohesabiwa na kuwekwa katika kanzidata mtandaoni.

“Wanaonyesha tuna Rais mteule, na mtu huyo ni Edmundo Gonzalez,” alisema Machado, akimgeukia mgombea wa urais, aliyekuwa amesimama kando yake.

Vyama vya upinzani vilijiunga nyuma ya Gonzalez katika jaribio la kumng’oa Rais Maduro baada ya miaka 11 madarakani, huku kukiwa na kutoridhika kwa kiasi kikubwa kuhusu mgogoro wa kiuchumi wa nchi hiyo.

Vikosi vya usalama nchini humo vimefyatua mabomu ya machozi na risasi za mpira kwa waandamanaji wanaopinga ushindi wa Maduro.

Maelfu ya watu walikusanyika jioni ya Jumatatu, wengine wakitembea maili kutoka mitaa ya mabanda kwenye milima inayozunguka jiji, kuelekea Ikulu ya Rais, wakiimba “uhuru, uhuru!” na kudai Serikali ianguke.

Picha zilionyesha matairi yakiteketea barabarani na idadi kubwa ya watu mitaani, huku polisi wakiwa kwenye pikipiki wakifyatua gesi ya kutoa machozi.

Katika baadhi ya maeneo, mabango ya Rais Maduro yalichanwa na kuchomwa moto huku matairi, magari na takataka pia zikichomwa.

Polisi wenye silaha, wanajeshi na wanamgambo wa mrengo wa kushoto wanaounga mkono Serikali walipambana na waandamanaji na kufunga barabara nyingi karibu na katikati ya jiji.

Serikali ya Venezuela pia imetangaza kusimamisha kwa muda safari za kibiashara za anga kwenda na kutoka Venezuela na Panama na Jamhuri ya Dominika.

Katika hotuba yake kwenye televisheni ya Serikali ya Venezuela, Maduro amesema ni wajibu wake kuwaambia ukweli.

“Sote tunawajibika kusikiliza ukweli, kuwa na subira, utulivu na nguvu kwa sababu tunafahamu hali hii na tunajua jinsi ya kukabiliana nayo na jinsi ya kushinda vurugu hizi.”

Maduro ameituhumu upinzani kwa kuitisha mapinduzi kwa kupinga matokeo.

“Hii sio mara ya kwanza tunakabiliana na kile tunachokabiliana nacho leo.

“Wanajaribu kulazimisha mapinduzi ya kijeshi ya kibeberu na ya kupinga mapinduzi nchini Venezuela,” amesema.

Wakizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), katika eneo lenye watu wengi lijulikanalo kama La Lucha likimaanisha mapambano, baadhi ya waandamanaji wamedai kuwa upinzani umeshinda.  

Paola Sarzalejo(41), alisema, “tulishinda kwa asilimia 70, lakini walitufanyia jambo lile lile tena. Walitupora uchaguzi tena. Tunataka maisha bora kwa vijana wetu, kwa nchi yetu.”

Naye Miguel (64), alikubaliana na Sarzalejo akisema: “Aliyeshindwa uchaguzi, hana haki ya kuwa pale sasa.

 “Tunataka maisha bora kwa vijana kwa sababu kama sivyo wataondoka nchini. Ikiwa vijana wote wataondoka, wazee tu ndio watakaobaki Venezuela, wazee pekee.”

Cristobal Martinez, akiwa amejifunika bendera ya Venezuela, amesema uchaguzi ulikuwa na udanganyifu.

Amesema vijana wengi walipiga kura katika uchaguzi uliokuwa muhimu sana kwa vijana kwa kuwa wengi wao hawana ajira wala elimu.

“Ilikuwa mara yangu ya kwanza kupiga kura maishani mwangu. Nilikuwa pale kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa tatu asubuhi na niliona watu wengi wakijikusanya barabarani. Watu wengi walishiriki kwa ajili ya mabadiliko,”amesema Martinez.

Amesema ingawa Rais Maduro amekuwa madarakani kwa muda mrefu hakuleta mabadiliko yoyote na hali imekuwa mbaya zaidi tangu Rais Hugo Rafae Chavez alipofariki dunia.

Martinez amewalaumu baadhi ya wazee wanaounga mkono Serikali kwa kuishi kwa bonasi au misaada ya chakula.

“Sisi tunataka mabadiliko, tunataka kazi nzuri, maisha bora kwa nchi yetu.”

Mwanasheria Mkuu wa Venezuela alionya kuwa kuziba barabara au kuvunja sheria zozote zinazohusiana na vurugu kama sehemu ya maandamano kutakabiliwa na nguvu zote za sheria.

Amesema watu 32 wamekamatwa kwa tuhuma kuanzia uharibifu wa vifaa vya uchaguzi hadi kuchochea vitendo vya vurugu.

Nchi za Magharibi na Amerika ya Kusini, pamoja na mashirika ya kimataifa ikiwamo Umoja wa Mataifa wameitaka Serikali ya Venezuela kutoa rekodi za upigaji kura kutoka vituo vya kupigia kura.

Argentina ni mojawapo ya nchi zilizokataa kuutambua ushindi wa Maduro katika uchaguzi na imewaita wanadiplomasia wake kutoka Buenos Aires.

Wanadiplomasia kutoka nchi nyingine sita za Amerika ya Kusini – Chile, Costa Rica, Panama, Peru, Jamhuri ya Dominika na Uruguay – pia wameondolewa kwa kile Waziri wa Mambo ya Nje Yvan Gil alichotaja kwenye mitandao ya kijamii kama “vitendo na matamko ya kuingilia kati.”

Wakati huohuo, maofisa wakuu wa utawala wa Marekani walisema kuwa matokeo yaliyotangazwa, “hayalingani na takwimu waliyopokea kupitia mifumo ya haraka na vyanzo vingine.

“Vyanzo vinaonyesha kuwa, matokeo yaliyotangazwa yanaweza kupingana na jinsi watu walivyopiga kura.

“Ndiyo maana tunawaomba mamlaka za uchaguzi za Venezuela kutoa data za msingi zinazounga mkono namba walizotangaza hadharani.”

Hata hivyo, Marekani haijajibu bado kuhusu matokeo hayo yanamaanisha nini kwa sera zao za vikwazo dhidi ya Venezuela.

Shirika la Nchi za Amerika (OAS) lilitangaza litafanya mkutano Jumatano wa baraza lake la kudumu kuhusu matokeo ya Venezuela.

Chanzo: BBC News, Aljazeera.

Related Posts