TANZANIA imepata pigo lingine katika Michezo ya Olimpiki ya Paris inayofanyika Ufaransa baada ya muogeleaji Collins Saliboko kushindwa kufuzu hatua inayofuata kwenye mashindano ya mita 100 freestyle, baada ya leo Jumanne Julai 30, 2024 kukamata nafasi ya 71 kati ya waogeleaji 79 alioshindana nao.
Kabla ya hapo, jana Jumatatu Julai 29, 2024, mchezaji wa judo wa Tanzania, Andrew Mlugu, aliondolewa hatua ya 16 baada ya kupoteza kwa alama 10-0 dhidi ya Mfaransa, Joan Benjamin Gaba katika pambano lililokuwa la upande mmoja.
Saliboko, aliyekuwa kwenye kundi la pili lenye waogeleaji nane, alishika nafasi ya saba baada ya kurekodi muda wa sekunde 56.38 kati ya wachezaji nane walioshiriki kwenye bwawa la kuogelea la Paris La Defense Arena.
Muda wake ulikuwa nyuma ya sekunde 1.16 kutoka ule aliokuwa amejiwekea.
Ovesh Purahoo kutoka Mauritius alishika nafasi ya kwanza kwa muda wa sekunde 52.95, akifuatiwa na Nixon Hernandez wa El Salvador aliyerekodi sekunde 52.73.
Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Antoine de Lapparent kutoka Cameroon, aliyerekodi sekunde 52.95, huku Irvin Hoost kutoka Suriname akishika nafasi ya nne kwa muda wa sekunde 52.99.
Muogeleaji kutoka Bangladesh, Islam Samiul Rafi, alishika nafasi ya tano kwa muda wa sekunde 53.10, wakati Hemed Samir Issa Al Adawi wa Oman akishika nafasi ya sita kwa sekunde 53.19. Yousef Abubakar wa Libya alishika nafasi ya mwisho kwenye kundi kwa muda wa sekunde 56.19.
Kutokana na matokeo ya jumla, Saliboko amepangwa nafasi ya 71 kati ya waogeleaji 79, akiwa na pointi 676. Ili kufuzu, Collins alihitaji kuwa miongoni mwa wachezaji 16 bora kati ya waogelaji 79 alioshindana nao.
Matumaini ya Tanzania ya kushinda medali sasa yanabaki kwa wawakilishi watano ambao ni muogeleaji wa kike Sophia Latiff atakayeshiriki katika mita 50 freestyle mnamo Agosti 3, 2024.
Wengine ni wanariadha Alphonce Felix na Gabriel Geay watakaoshiriki katika mbio za marathon kwa wanaume mnamo Agosti 11 na wanariadha wa kike Magdalena Shauri na Jackline Juma Sakilu watakaoshiriki katika mbio za marathon kwa wanawake mnamo Agosti 10. Wote hao watakimbia umbali wa kilomita 42.