Enekia atimkia Mexico | Mwanaspoti

NYOTA wa kimataifa wa Tanzania, Enekia Lunyamila amejiunga na klabu ya Mazaltan inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini Mexico kwa mkataba wa miaka miwili.

Kiraka huyo msimu uliopita alikuwa akiitumikia Eastern Flames ya Saudia ambayo ilimaliza nafasi ya saba kati ya timu nane zinazoshiriki Ligi ya Wanawake nchini humo.

Msimu uliopita Mazaltan ambayo ni timu mpya ya Enekia ilimaliza nafasi ya 14 kati ya 18 zilizoshiriki Ligi hiyo baada ya kucheza mechi 17, ikishinda minne, sare moja na kupoteza 12.

Msimu huu tayari ligi hiyo imeanza, lakini imeanza vibaya kwenye mechi mbili ilizocheza ikipoteza yote na kubaki mkiani mwa msimamo.

Mchezaji huyo baada ya kujiunga na klabu hiyo ataungana na Mtanzania mwenzake, beki wa kati Julietha Singano anayekipiga Juarez ya nchini humo.

Chanzo kimeiambia Mwanaspoti kuwa Lunyamila tayari yupo nchini humo kusaini mkataba wa miaka miwili unaotarajiwa kutamatika Julai 2026.

“Wamemuona ni mchezaji ambaye anaweza kuwasaidia kwenye maeneo mengi amecheza Morocco kwa mafaniko makubwa, na yupo Mexico kwa ajili ya kusaini mkataba huo baada ya kukamilisha taratibu zote,” kimesema chanzo hicho.

Hadi sasa Lunyamila amefunga mabao 110 kwenye ligi mbalimbali, akiwa na Alliance Girls mwaka 2016 alifunga mabao 37, Ruvuma Queens (2018) mabao 27 huku  Ausfaz Assa Zag ya Morocco akifunga mabao 49 mwaka 2021 akiibuka na tuzo ya mfungaji bora na mabao saba akiifungia Eastern Flames ya Saudia.

Related Posts