BAADA ya Yanga kuichapa mabao 4-0 Kaizer Cheif ya Sauzi, Mabosi wa kikosi hicho wameshtuka na kuanza hesabu kali za usajili, huku kocha akiwataka kuboresha maeneo matatu.
Yanga ilicheza na kikosi hicho kilicho chini ya kocha Nasreddine Nabi, ambaye aliwafundisha wana Jangwani hao msimu wa 22/23 na kuwatembezea kipigo huku wakibeba Kombe la Toyota.
Awali, Mwanaspoti iliwataarifu mashabiki wa soka kuwa, baada ya matokeo hayo kocha huyo alikiri kuwa walistahili kupokea kipigo hicho na ni wazi kuwa timu yake bado haina msuli wa kupambana na Yanga.
Unaambiwa baada ya matokeo hayo viongozi waliitana chapuĀ na kukaa kikao cha dharura ili kuunda kikosi kipya.
Mabosi wa Kazers wamemhakikishia Nabi kwamba watafanya usajili wa wachezaji wakubwa baada ya kuona kiwango Cha timu yao dhidi ya Yanga.
Kocha huyo ametaka kuongezewa mabeki, viungo na washambuliaji na kila eneo wasipungue wawili ili waweze kuongeza nguvu kwa wale waliopo.
Akizungumza na Mwanaspoti, amesema :”Kikosi changu kina wachezaji waliotoka timu ya vijana wengi, ila haimaanishi hawana uwezo, lakini kuna mabadiliko kidogo yanatakiwa kufanyika katika maeneo matatu ili kujenga timu zaidi.”
“Nataka viungo, mabeki na washambuliaji wenye uwezo mkubwa na uzoefu ili wawe walimu kwa hawa vijana wadogo wanaocheza nafasi hizo.”
Kutokana na hilo juzi kikosi hicho kimeingia mkataba wa miaka mitatu na aliyekuwa beki wa Cape Town Spurs mwenye umri wa miaka 22, Rushwin Dortley iliyomaliza ikiwa nafasi ya tano katika ligi.
Kaizer ilimaliza ikiwa nafasi ya 10 ikiwa na rekodi ya kutobeba ubingwa wa Ligi Kuu Africa Kusini kwa misimu tisa mfululizo.