Dar es Salaam. Shahidi wa saba katika kesi ya mauaji ya dereva wa bodaboda inayomkabili mshtakiwa Ibrahim Othman maarufu Boban, ameeleza Mahakama namna mshtakiwa alivyoshindwa kuondoa GPRS iliyofungwa katika pikipiki aliyoiba na kisha kuitelekeza.
Shahidi huyo, F 5818 Sajent Samwel ametoa ushahidi wake jana Julai 29, 2024 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyokaa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusikiliza shauri hilo.
Boban anakabiliwa na shtaka moja la kumuua dereva Mahmud Peya kwa kukusudia, tukio analodaiwa kulitenda Februari 4, 2023.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo akishirikiana na wenzake baada ya kumkodi dereva huyo kisha kumuua na kuiba pikipiki ambayo baadaye aliipeleka kwa fundi ili iondolewe GPRS, lakini fundi huyo alishindwa kuondoa kifaa hicho.
GPRS ni mfumo wa mawasiliano unaotumika pamoja na mfumo wa ufuatiliaji wa GPS kwa lengo la kutambua mahali kilipo chombo cha usafiri.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali, Frank Rimoy, mbele ya Hakimu Hukumu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya aliyeongezewa mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi hiyo, Sajent Samwel amedai kuwa, Julai Mosi, 2023 akiwa ofisini alipewa maelekezo na Mkaguzi wa Polisi aende mahabusu amchukue Othman anayekabiliwa na shtaka la mauaji ili aje amfanyie mahojiano.
“Nilianda chumba kwa ajili ya kufanyia mahojiano baina ya mimi na mshtakiwa na baada ya hapo nilikwenda kumchukua Othman mahabusu na kisha kuanza kufanya nae mahojiano,” amedai Sajent Samwel.
Amedai kuwa mahojiano yalianza saa tatu asubuhi na yakikuwa ya maswali na majibu, lakini mshtakiwa alianza kueleza historia yake na elimu yake.
“Mshtakiwa huyo alikubali kutoa maelezo yake bila wakili na alianza kueleza tukio la mauaji lilivyotokea na ushiriki wake kwa wakati huo.
“Othman aliniambia alikuwa na wenzake wawili ambao ni Juma Shehe na Abilah ambao walikutana na kupanga mpango wa kwenda kupora pikipili,” amedai.
Alidai kuwa kuwa, Othman ndio aliyekwenda kukodi pikipiki aina ya Boxer iliyokuwa inaendeshwa na Peya na kumuelekeza kuwa anatakiwa ampeleke eneo la njia ya Ngo’mbe lililopo Temeke na alikuwa anakutana na Shehe na Abilah.
“Baada ya kufika eneo walilopanga kukutana na mwenzake, mshtakiwa alimwambia dereva wa bodaboda simama kisha kuchomoa funguo ya pikipiki ile.
“Mshtakiwa baada ya kuchomoa funguo, wenzake walitokea eneo hilo, Juma alimchoma kisu dereva wa bodaboda na kudondoka chini,” amedai Sajent Samwel.
Aliendelea kueleza kuwa, mshtakiwa alichukua bodaboda hiyo na kupanda kisha kuipeleka kwa fundi anayehusika kutoa GPRS.
“Othman alinaimbia aliipeleka bodaboda hiyo kwa fundi wa kutoa GPRS kwenye bodaboda, ambao wenyewe wanamuita Mdudu.
“Alipofika kwa fundi wa kutoa wadudu, Othman alimuelekeza atoe GPRS, lakini fundi huyo alishindwa kutoa kifaa hicho cha GPRS kwenye pikipiki ya Peya,” amedai.
Imedaiwa kuwa, baada ya kushindwa kutoa GPRS, mshtakiwa aliondoka na kwenda nyumbani kwa mpenzi wake aitwaye Hadija, alipofika aliiegesha pikipiki hiyo nje ya nyumba kisha kuingia ndani na kupumzika na mpenzi wake.
“Baada ya muda mfupi, kundi la bodaboda wakiwa na askari polisi walifika eneo hilo na kuichukua bodaboda hiyo,” amedai Sajent Samwel.
Hata hivyo, baada ya siku kadhaa kupita, mshtakiwa huyo alikamatwa na Jeshi la Polisi akiwa eneo la Sinza na kupelekwa Kituo cha Polisi Chang’ombe kwa ajili ya mahojiano.
Katika mahojiano yake Polisi, mshtakiwa alidai hajahusika na mauaji hayo, bali aliyehusika ni Juma Shehe.
Shahidi huyo alimtambua mshtakiwa mahakamani hapo na kuomba Mahakama ipokee maelezo ya onyo ya mshtakiwa.
Mshtakiwa apinga maelezo ya onyo
Shahidi baada ya kueleza hayo, upande wa utetezi ukiongozwa na Seleman Almas akishirikiana na Hassan Kiangio, ulipinga ombi hilo kwa madai kuwa mteja wao alichukuliwa maelezo yake nje ya muda unaotakiwa.
Wakili Almas amedai mteja wake anadaiwa kupigwa na kuteswa na alilazimishwa kusiani maelezo bila kujua yanahusu nini.
Hakimu Lyamula baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 9, 2024 kwa ajili ya kusikiliza kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi.
Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la mauaji linalomkabili kutokuwa na dhamana.