TIMU ya Young Mvita imeifunga North Mara kwa pointi 46-35 katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Mara uliofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu Tarime.
Katika mchezo huo North Mara iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 9-2, ilhali Young Mvita iliongoza katika robo zote tatu kwa pointi 15-10, 15-6, 14-10.
Katika mchezo huo Prosper Prosper wa Young mvita aliongoza kwa kufunga pointi 14, ilhali upande North Mara alikuwa ni Colman aliyefunga pointi 10.
Kabla ya mchezo wa ufunguzi kuanza mwenyekiti wa Chama cha Kikapu Mkoa wa Mara (Marba), Sylvanus Gwiboha aliziomba taasisi na wadau wa michezo kuchangia ujenzi wa viwanja kila wilaya mkoani humo ili kuukuza mchezo huo.
Alisema serikali imeruhusu mchezo wa kikapu uchezwe kuanzia ngazi ya shule za msingi, hivyo ni wajibu wa wadau kufanikisha miundombinu ili kujenga timu bora.