Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameiwashia taa nyekundu Kampuni ye Mecco inayojenga Barabara ya Chake-Wete, kwa kile alichodai kushindwa kutekeleza mradi huo kwa mujibu wa mkataba.
Ameonya iwapo kampuni hiyo haitakamilisha mradi huo kama walivyokubaliana kwenye mkataba, itakuwa ndiyo mwisho kupata zabuni za ujenzi kisiwani humo.
Hemed ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 30, 2024 alipofanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kisiwani humo.
Amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo kwani wananchi wanapata shida kubwa kutokana na miundombinu mibovu na kumtaka mkandarasi huyo kuongeza kasi.
“Kumekuwapo na ubabaifu wa hali ya juu kwa baadhi ya makandarasi wanaojenga miradi ya Serikali kwa kutotimiza makubaliano ya mikataba, jambo linaloisababishia Serikali hasara kubwa kwa kutofikia malengo ya kuwaletea wananchi maendeleo,” amesema.
Mkataba wa barabara hiyo ya kilomita 22, utakaogharimu Sh26.6 bilioni, ulisainiwa mwaka 2022 na ulitakiwa kukamilika Agosti 2024.
Hata hivyo, umechelewa na alipewa nyongeza ya miezi mitano hivyo anatakiwa kukabidhi barabara hiyo Januari 2025.
Akizungumza kuhusu kusuasua kwa ujenzi huo, mkandarasi wa kampuni hiyo, Nassor Kolowa amesema wametumia muda mrefu kuondoa udongo usiohitajika na pia kucheleweshewa malipo.
Hata hivyo, amesema watahakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili wamalize ndani ya muda waliopewa.
Akiwa katika mradi wa soko la samaki na mbogamboga lililopo Mzambarau Takao na soko la wajasiriamali Kifumbikai Wete, Hemed ametoa mwezi mmoja kwa wananchi ambao wameshalipwa fidia kuondoka katika eneo hilo kupisha ujenzi.
Amesema kuendelea kuwepo kwa wananchi hao katika eneo hilo kunakwamisha maendeleo ya ujenzi huo ambao kukamilika kwake kutawaondolea changamoto ya kufuata mahitaji mbali.
Amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa kampuni mbalimbali zinazojenga miradi ya maendeleo Zanzibar, ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati katika visiwa vyote vya Unguja na Pemba.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amewataka makandarasi hao kuongeza nguvu kazi na kasi ya ujenzi ili kumaliza kwa wakati miradi hiyo.