BAADA ya straika Mtanzania Athuman Masumbuko ‘Makambo’ kutambulishwa FCA Darmstadt ya Ujerumani juzi, amecheza mchezo wake wa kwanza wa ligi akiitumikia kwa dakika 20 dhidi ya FC Germania.
Mchezo huo ulipigwa katika Uwanja wa Sportplatz Rödermark-Ober Roden, ambapo timu anayoichezea straika huyo ikiwa ugenini ilipoteza kwa mabao 2-1.
Timu anayochezea kinda huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Mashujaa FC inashiriki ligi ngazi ya 7 nchini Ujerumani maarufu ‘Gruppenliga’.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makambo Jr amesema ingawa ni ligi ya daraja la chini, lakini kwa dakika chache alizocheza zinaonyesha ana kazi ya ziada kuonyesha uwezo na kuaminiwa kupewa nafasi kikosini.
“Muda mfupi nimecheza, lakini ni kama nimecheza mechi mbili. Kwanza mpira wa huku una kasi mno hakuna muda wa kupumzika. Ligi ni ngumu inahitaji kuwa ukomavu sana. Tanzania nilijiandaa mno, lakini naona kuna kazi zaidi,” amesema Makambo.