Takukuru kuchunguza upotevu vifaa vya ujenzi Hospitali Katoro

Geita. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita imeanza uchunguzi wa ujenzi wa awamu ya pili wa Hospitali ya Katoro baada ya kubaini vifaa vyenye thamani ya Sh1.7 bilioni havipo stoo licha ya kununuliwa na kupokewa.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa miezi mitatu wa taasisi hiyo, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita,  Alex Mpemba amesema katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wamebaini baadhi ya vifaa licha ya kununuliwa na kupokewa havijatumika kwenye ujenzi na havionekani.

Mpemba amesema uchunguzi unaofanywa na taasisi hiyo ni kutaka kubaini kama kuna ubadhirifu ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Mbali na uchunguzi wa vifaa hivyo, taasisi hiyo pia inachunguza ujenzi wa nyumba ya watumishi katika Shule ya Msingi Nyamiboga inayojengwa kwa Sh27 milioni ambayo ujenzi wa mashimo ya choo na mfumo wake haujajengwa licha ya vifaa kuwapo eneo la kazi.

Amesema wamebaini mradi huo umekwama kutokana na Sh7 milioni zilizotengwa na Halmashauri ya Geita kwa ajili ya ufundi kutojulikana zilivyotumika.

“Tumemshauri mkurugenzi kuhakikisha fedha za mradi zilizotengwa zinapatikana na kutumika katika kazi husika, tayari tumeanza uchunguzi kwa lengo la kubaini fedha zilipopotelea,”amesema Mpemba.

Akizungumzia ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, amesema miradi 25 yenye thamani ya Sh10.2 bilioni,  miradi mitano kati ya hiyo imebainika kuwa na upungufu.

Katika hatua nyingine, Mpemba amewatahadharisha wananchi wanaotaka kugombea nafasi za uongozi kwenye Serikali za mitaa kutojiingiza kwenye matendo ya rushwa kwa kuwa kufanya hivyo itawaondoa kwenye sifa ya kugombea.

Amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki, usio na vitendo vya rushwa.

Bakari Masanja, mkazi wa Katoro amesema uchunguzi unaofanywa na Takukuru utaibua mengi.

Amesema hospitali hiyo ilitegemewa kupunguza changamoto ya msongamano kwenye Kituo cha Afya cha Katoro, lakini hadi sasa ni zaidi ya miaka mitano ujenzi haujakamilika.

“Wananchi waliaminishwa sana kwenye ujenzi wa hospitali hii, lakini kutokamilika kunawafanya wakose imani na viongozi wao; uchunguzi huu uende mbele uje na majibu ya lini miradi itakamilika,”amesema Masanja.

Irene Mapinda, mkazi wa Butobela ameiomba Takukuru kuhakikisha wanachunguza na kubani mianya ya rushwa kwenye miradi na kuwachukulia hatua wote watakaohusika kwa kuwa vitendo hivyo vinasababisha wananchi kukosa huduma stahiki.

Related Posts