BAADA ya ratiba ya mechi za hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka na Azam FC kupangiwa APR ya Rwanda na baadaye Pyramids ya Misri endapo itafuzu uongozi wa klabu hiyo hautaki kurudia makosa.
“Katika misimu miwili iliyopita tulipangwa na timu ambazo tuliziona tunazimudu na tungeweza kuzitoa kirahisi,” anasema Nassor Idrisa ‘Father’, mwenyekiti wa Azam FC.
“Akili zetu tukazielekeza kwa wapinzani wa mbele kabisa bila kuzingatia tuliotakiwa kukutana nao. Matokeo yake tukatolewa mapema,” anaelezea kwa uchungu mwanzilishi huyo wa Azam FC. Hapo Father anakumbuka kilichotokea kwa Al Akhdar ya Libya 2022 na Bahir Dar ya Ethiopia 2023.
Hakuna aliyekuwa akiiwaza Al Akhdar hapo kabla na kila mmoja aliamini Azam FC imepata mteremko. Lakini kilichotokea kiliwahuzunisha wengi. Azam FC ilifungwa 3-0 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani ushindi ambao haukutosha kuivusha.
Endapo ungetosha, Azam FC ingekutana na Plateau United ya Nigeria.
“Hatukuwaona kama kikwazo kikubwa sana Al Akhdar na kuelekeza akili zetu kwa Wanaijeria. Kuja kutahamaki tukawa na mzigo mzito wa kupindua meza kutoka 3-0 ili tusonge mbele, ila ilishindikana,” anasema Zaka Zakazi, mkuu wa idara ya habari.
Mwaka 2023 Azam FC ilipangwa na Bahir Dar ya Ethiopia na baada ya hapo ingekutana na Club Africain ya Tunisia endapo ingevuka.
“Huu mwaka tulikuwa na matumaini makubwa sana kwa sababu tulikuwa na kikosi bora na kambi ya maandalizi ilikuwa nzuri sana kule Tunisia,” anasema Zaka.
Anasema kwa uwezo na maandalizi waliamini wangeitoa Bahir Dar.
“Ratiba ya CAF ilitoka tukiwa Tunisia kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya na wakati tunaondoka kule, tuliamini tungerudi tena kucheza na Club Africain,” anasema.
Lakini hali ikawa tofauti. Azam FC wakapoteza kwa mabao 2-1 na katika mchezo wa marudiano wakashinda kwa idadi kama hiyo. Mchezo ukaingia kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti na Azam FC kutolewa.
“Hatutaki kurudia makosa kama haya safari hii,” anasema Nassor Idrisa. “Akili zetu zote ni kwa APR. Tunaamini kwamba hii ni timu kubwa na bora na tumewaona kwenye Kagame Cup na pia tutawaona kwenye Simba Day,” anasema Zaka.
Kocha wa Azam FC, Yousouph Dabo anasema anawafahamu APR kwa sababu walimtaka msimu uliopita.
“Walitaka kunipa kazi nikiwa katika msimu wangu wa kwanza hapa Azam FC. Sikuwahi kuwajua hapo kabla, lakini baada ya hapo ndipo nikaanza kuwafuatialia,” alisema Dabo mara tu baada ya ratiba ya CAF kutoka.
“Wameshinda ubingwa kwao mara nyingi ikiwa na maana wameshiriki hatua kama hii mara nyingi. Azam haijashiriki mara nyingi.”
Katika kujiandaa, Azam FC imeshacheza mechi tatu za kirafiki, moja Zanzibar na mbili Morocco. Kule Zanzibar ilikuwa dhidi ya KVZ na Azam FC ikashinda 4-0. Hapa Morocco ilikuwa dhidi ya US Yacoub El Mansour iliposhinda 3-0 na dhidi ya UTS ambayo ilimaliza katika nafasi ya nne kwenye ligi ya Morocco msimu uliopita walipotoka sare ya 1-1.
Jumatatu usiku. Julai 30, walicheza na Wydad Casablanca katika mchezo wa mwisho nchini Morocco na kufungwa mabao 4-1. Baada ya hapo watarudi Dar es Salaam na kwenda moja kwa moja Kigali, Rwanda kucheza na Rayon Sport kwenye siku yao maalumu, Rayon Day, Agosti 3 mwaka huu. Kutoka Rwanda, Azam FC itawenda Zanzibar kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Coatal Union na kisha fainali au mshindi wa tatu jijini Dar es Salaam. Mechi hizo zitaisaidia kuwa imara kabla ya kuwavaa APR Agosti 18, dimbani Azam Complex.
“Msimu huu tunataka tufanye vizuri zaidi kimataifa angalau tufike hatua ya makundi,” anasema Idrisa.
“Hii ni hatua ambayo imetutesa kwa miaka mingi na tukiangalia timu zinazofika huko tunaona kabisa hazijatuzidi kitu. Kwa hiyo tunataka kuthibitisha hilo safari hii.”
Azam FC imeshiriki mara moja tu Ligi ya Mabingwa msimu wa 2015/16 baada ya kuwa mabingwa wa Bara 2013/14. Hata hivyo safari haikuwa ndefu kwani walitolewa na Ferroviario Beira ya Msumbiji. Mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam Azam FC ilishinda 1-0 na kupoteza 2-0 ugenini. “Kwa kweli mechi ya ugenini ilikuwa ngumu sana. Uwanja ulijaa maji kutokana na mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha kule,” anasema Zaka.
Miaka takribani 10 baadaye Azam FC inarudi tena kwenye Ligi ya Mabingwa, je nini kitaleta tofauti?
“Ni vigumu kutaja kitu kimoja lakini kimsingi kuna mabadiliko makubwa. Jambo la kwanza ni subira, unamuona Dabo? Ni kocha kuanza msimu na kuumaliza, tangu msimu wa 2011/12 alipofanya hivyo Stewart Hall,” anasema Zaka akielezea ‘chinja chinja’ ya makocha iliyozoeleka Chamazi. “Kwa hiyo kila msimu tulikuwa tunaanza upya. Kwenye pre season kama sasa makocha wanahangaika kuwazoea wachezaji na hali kadhalika wachezaji kwa makocha.”
Zaka anasema sasa ni tofauti. Hii pre season imekuwa bora kwa sababu wachezaji wapo na kocha ambaye wameshamzoea na yeye kawazoea.
“Acha tuone safari hii itakuwaje, lakini picha halisi tutaipata kwa APR,” anamalizia Zaka.
Azam FC ambayo Julai hii imesherehea miaka 20 ya kuanzishwa na 16 ya Ligi Kuu, inataka kuanza safari mpya ya mafanikio kwa kufanya mambo yake yote ambayo yalishindikana kwenye miaka 20 iliyopita.